top of page
C-Sema Team

Zijue njia rahisi za kuhudumia ngozi ya mwanao.

Watoto wachanga na wadogo huwa wanaweza kupata magonjwa ya ngozi kwa urahisi kwani ngozi yao ni laini, nyororo ambayo inaweza kushambuliwa na vimelea vinavyosababisha magonjwa kwa urahisi. Tunakupa vidokezo vya jinsi ya kuhudumia ngozi ya mwanao.



Vipele kwa watoto wachanga.

Pamoja na kwamba ngozi za watoto wachanga hushambuliwa kirahisi vingi vya vipele vinavyowatokea mara nyingi hupotea vyenyewe bila matibabu yeyote. Hata hivyo pale unapokuwa na wasiwasi juu ya vipele katika ngozi ya mwanao, jiulize maswali haya; -

  • Nifanye nini kupunguza uwezekano wa mwanangu kuwa na vipele?

  • Je, tatizo alilonalo linahitaji ushauri na tiba ya kitabibu?

  • Je, tatizo alilonalo linaweza kupata suluhu hapa nyumbani?

Epuka vipele vipele vya daipa au nepi.

Hivi ni vipele vyekundu vinavyowasha vilivyo maeneo unayofunga daipa au nepi. Mara nyingi vipele hivi husababishwa na daipa au nepi zenye mkojo alizokaa nazo muda mrefu. Pia daipa au nepi ambazo zimembana sana. Vilevile tatizo hili linaweza kusababishwa na baadhi ya daipa zenyewe (ubora wa daipa au nepi). Ili kuepuka ugonjwa huu mwoshe mwanao kwa maji ya vuguvugu na sabuni laini, badilisha daipa za mwanao mara kwa mara na anza kumwacha uchi ili maeneo hayo yapigwe na hewa. Kama vitaendelea tafadhali pata ushauri wa daktari.


Chunusi za utotoni.

Zipo chunusi za utotoni au vipele vyeupe ambazo hazifanani na zile za vijana walio katika balekhe. Hizi huwa zinatokana na fangasi na wala siyo mafuta. Chunusi hizi huonekana puani na shavuni mara nyingi. Huna haja ya kuhangaika kwa ajili ya vipele hivi kwani huwa vinapotea vyenyewe baada ya muda.


Alama za ngozi za kuzaliwa nazo.

Katika kila watoto kumi mmoja huwa ana alama za kuzaliwa nazo. Mara nyingi alama hizi za kuzaliwa nazo huwa zinatokea wakati wa kuzaliwa na si za kurithi. Mzazi huna haja ya kuwa na hofu yeyote. Ingawa pale ambapo wasiwasi utazidi basi muone daktari kwa ushauri zaidi.


Ekzema (Eczema).

Huu ni ugonjwa unaowashambulia zaidi watoto wanaotoka kwenye familia zaenye asili ya magonjwa ya mzio, pumu au magonjwa ya ngozi. Ugonjwa huu huanza kutokea usoni na kwenye sehemu zenye mikunjo kama vile uvungu wa kiwiko, goti na pia hutotokea kwenye kifua. Hivi ni vipele vyekundu au vibakabaka vinavyoanza kwa kuwasha na kisha huwa vijeraha vinavyotoa majimaji. Baadae vipele hivi hukauka na kuacha magamba makavu na kisha madoa meusi.


Ili kuutibu epuka vitu vinavyosababisha mtoto kuanza kuwashwa (vianzisha mzio). Vitu kama vile baadhi ya sabuni, mafuta ya kujipaka na n.k. Hivyo matibabu yake huhusisha kuepuka sabuni na mafuta yanayomletea shida, mathalani sabuni zenye kemikali, n.k. Kuvitibu mkande kwa maji baridi, viache vichomwe na mwanga wa jua. Kama hakuna nafuu mwone daktari.


Ngozi kavu.

Kawaida ngozi ya mtoto huwa ni nyororo na iliyo n unyevunyevu. Lakini unaweza kukutana na ngozi kavu na inayotoka magamba hii mara nyingi hutokea kwa watoto waliopitiliza muda wa kuzaliwa. Ngozi yake ya ndani huwa ni nyororo na yenye unyevunyevu wa kutosha. Tatizo hili linaweza kuisha lenyewe lakini kama mwanao anendelea kuwa na ngovu kavu kwa muda mrefu tafadhali nenda kwa daktari.


Mba za kichwani.

Mba za kichwa huanza kutokea katika mwezi wa kwanza au wa pili baada ya kuzaliwa na huisha ndani ya mwaka mmoja. Mba hizi kwa kiwango fulani husababishwa na mafuta mengi kichwani mwa mtoto lakini pia husababishwa na kutoosha kichwa cha mtoto vizuri. Ugonjwa huu huwa unajitokeza kama tabaka la njano na kama nta na ngozi inayozunguka tabaka hilo huwa ni nyekundu na inayowasha. Pamoja na kutokea kichwani pia hutokea kwenye kope za macho na pembezoni mwa masikio.


Matibabu yake hujumuisha kuosha kichwa cha mwanao kwa kuondoa mba yote pamoja na tabaka lake. Ili kuosha vizuri loweka taulo laini ndani ya maji ya vuguvugu kisha mfunge nalo kichwani ili kuloanisha matabaka ya mba. Baada ya kufanya hivyo kwangua tabaka hilo. Kisha mpake mwanao kwa shampoo au mafuta.


Vipele vya joto.

Wakati mwingine joto likiwa kali mwanao anaweza kupata vipele vya joto. Vipele vinavyoanza kama vipele vidogo vidogo vyekundu kama vya surua. Huanza kama vidoa vyekundu na hatimaye huja kuwa kama vilenge vilenge vidogo visivyo na usaha. Mara nyingi hutokea kwenye sehemu ya mwili zinazopendelea kutoka jasho kama vile mikonjo ya ngozi, kwapa, shingo na kwenye mikunjo ya paja na nyonga.


Kwa sababu vipelel hivi vinasababishwa na joto kama jina lake lilivyo, kumvalisha mwanao nguo zenye kuruhusu hewa na kumvalisha mwanao nguo nyepesi ni moja ya vitu muhimu katika matibabu ya ugonjwa huu. Kumbuka hata wakati wa baridi vipele hivi vinaweza kutokea na hivi ni kwa sababu ya joto jingi kutokana na nguo nyingi anazovalishwa mtoto. Hivyo katika mazingira kama hayo unahitaji kumvua nguo au kumpunguzia nguo anapokuwa ameanza kutoka jasho. Kama baada ya kufanya hivyo vipele bado vinaendelea muone daktari.


Matumizi ya poda kwa watoto wadogo.

Ngozi ya watoto wachanga huwa haina ulazimu wa kutumia poda, na hata hviyo watoto wachanga wanaweza wakameza chembe za unga ule ambavyo vitakapoingia ndani ya mapafu vinaweza kumsbabishia matatizoa ya mapafu. Hivyo ni heri ukaepuka matumizi ya poda kwa mwanao kwani siyo muhimu.


Maambukizi ya mba kwa watoto.

Ugonjwa wa mba kwa watoto hujitokeza katika muonekano tofauti kutokana na sehemu mba zenyewe zilipo, mathalani mba zinazotokea mdomoni na huonekana kama maziwa yaliyoganda na zile zinazotokea kwenye sehemu zenye mikunjo ya daipa hujitokeza kama vipele vyekundu. Mwone daktari wako kwa ushauri zaidi.


Usafi.

Usafi huchangia kumwepusha mwanao kuwa na vipele ambavyo vitamfanya awe na fya na tabasamu. Osha matandiko yake, nguo zake na chochote kile kinachogusa ngozi yake kwa kutumia sabuni. Kwa kufanya hivyo utapunguza uwezekano wa kuwashwa unaochangangia baadhi ya magonjwa kuanza.


Manjano.

Manjano ni rangi ya njano inayoonekana kwenye macho na ngozi ya mtoto siku ya 2 mpka ya 3 baada ya kuzaliwa na huwa inatokea zaidi kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati. Hii ni rangi inayosababishwa na kiwango kikubwa cha kemikali ya bilirubini inayotokana na kuharibiwa kwa kiwango kikubwa kwa chembe nyekundu za damu. Matibabu katika hali hii yanaweza kujumuisha tiba kupitia mwanga (phototherapy) na kunyonyesha mtoto mara kwa mara.


Dalili za hatari katika hali ya manjano ni pale ambapo manjano imeanza siku ya kwanza ya kuzaliwa au manjano imeendelea zaidi ya siku ya 14. Tafadhali mara moja onana na daktari.


Chunguza kama mwanao amebabuka kwa miale ya jua.

Mtoto mchanga au mdogo anaweza kuathirika kwa urahisi kwa miale ya mwanga wa jua. Katika kumkinga mtoto unaweza kuepuka kumuweka mwanao juani katika miezi 6 ya kwanza. Pia unaweza kutumia bidhaa za kumkinga mwanao dhidi ya miale ya jua kama itakavyoelezewa hapo chini.


Bidhaa za kumkinga mtoto dhidi ya miale ya jua.

Unapotaka kumkinga mwanao dhidi ya miale ya jua unaweza kumpaka zinki oxide kwenye pua, masikio, mdomo na sehemu nyingine ambazo hazijafunikwa na nguo. Funika sehemu kubwa ya mwili wa mwanao kwa nguo na kofia pana. Linda macho yake toka kwenye miale ya jua ambayo hudhuru.


Bidhaa za ngozi kwa watoto.

Kuwa mwangalifu pale unapofanya manunuzi ya bidhaa za kutumia kwa ngozi ya mwanao kwa sababu ngozi yake inaweza kupata maradhi kwa urahisi. Angalia bidhaa zisizo na rangi, harufu / marashi na kemikali kama parabens au phthalates zinazowekwa kwenye bidhaa nyingi za viwandani kama vile dawa za meno, shampoo, losheni na nyingine nyingi kwa ajili ya kuzikinga bidhaa hizo zisiharibike. Kemikali hizi zinaweza kusababisha kuwasha au madhara kwa ngozi ya mtoto au afya kwa ujumla. Kama una wasiwasi na bidhaa Fulani basi wasiliana na daktari kabla ya kuinunua.


Je, utaepukaje magonjwa ya ngozi wakati wa kumwogesha?

Kumbuka ngozi ya mtoto mchanga ni nyororo na inaweza kuharibika kwa haraka. Hivyo tunza ngozi ya kichanga chako kwa kuiachia unyevunyevu baada ya kumuogesha na maji ya vuguvugu kwa dakika 3 mpaka 5. Epuka kumuacha mwanao kwenye maji ya sabuni kwa muda mrefu au kukaa au kucheza kwa muda mrefu kwenye maji. Mpake mwanao losheni ya watoto au mafuta kama yapo punde tu baada ya kumuogesha.


Kumchua mtoto.

Endapo vipele vya mwanao vinamsababishia mwano kuwasha na kumkosesha raha. Mchue mwanao kwani kumchua mwanao siyo tu kutamletea mapumziko lakini kutamsaidia kuacha kulia na kumpatia usingizi.


Je ni wakati gani nikamuone daktari wa watoto?

Mwisho kabisa kama bonsai. Matatizo mengi ya ngozi kwa watoto huisha yenyewe. Kama mwanao anatapika kila kitu, ana degedege, amelegea hawezi kukaa bila kuegemea, anapumua kwa shida muone daktari mara moja. Muone daktarin iwapo mwanao ana homa, anaharisha, ngozi yake ina vilengelenge vya njano vinavyoambatana na homa. Pia kama hajaweza kukaza shingo mpka miezi 6 muone daktari. Mwisho kama hawezi kukaa mpaka miezi 9 au kutembea mpaka mwaka na nusu muone daktari.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org

1,402 views
bottom of page