top of page
  • C-Sema Team

Zijue adhabu zinazotolewazo sheria ya mtoto inapovunjwa

Makala haya yanaangazia baadhi ya adhabu chache zinazogusa maisha ya wazazi / walezi na hata watoto katika kutimiza majukumu yao ya kila siku. Ingawa adhabu zipo nyingi katika Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 ya Tanzania Bara, sisi tutakupa adhabu tatu kama ifuatavyo.Mtoto anapopatikana na hatia.


Sheria ya Mtoto inazuia mtoto kufungwa kifungo chochote kama vile vifungo vya watu wazima pale anapokutwa na kosa la kuvunja sheria za nchi. Badala yake sheria inatoa aina ya adhabu na matunzo kwa ajili ya kumrekebisha mtoto na kumrudisha katika mazingira ya uadilifu kama watoto wengine waadilifu. Adhabu hizi hupewa mtoto: kupewa muda maalum wa kujirudi kupitia uangalizi wa mzazi mlezi, ndugu au afisa ustawi wa jamii; kulipa faini, fidia au gharama kwa kupitia kwa mzazi, mlezi; au ndugu na kupelekwa katika shule maalumu katika kipindi maalumu kwa ajili ya matunzo.


Kuvunja sheria na taratibu za ajira kwa mtoto / watoto. Mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka 14 ana haki ya kufanya kazi nyepesi na kupata malipo stahiki. Ieleweke kuwa, kazi nyepesi ni zile ambazo haziathiri afya ya mtoto, hazikwamishi maendeleo yake kielimu au makuzi yake. Hii ni pamoja na kazi ambazo hazina madhara katika utendaji wa kazi za kimasomo zinazotolewa ili azifanye akiwa nyumbani, haki yake ya kucheza, au kazi ambazo haziathiri uhuru wake wa kushiriki katika mafunzo ya kijamii na zile zisizomtaka mtoto kufanya kazi nyakati za usiku ambazo huanza muda wowote kati ya saa mbili za usiku hadi saa kumi na mbili za asubuhi.


Hivyo basi, kila mwajiri ambaye ameajiri watoto, anatakiwa kuhakikisha kwamba kila mtoto aliyeajiriwa kihalali anapewa ulinzi dhidi ya mazingira yoyote ya unyanyasaji au vitendo vyovyote vinavyoweza kumwathiri kulingana na umri wake au uwezo wake wa kufanya kazi. Mtu yeyote atakayevunja masharti hayo anaweza fungwa kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini isiyopungua shilingi laki moja au vyote kwa pamoja.


Uuzaji wa vileo kwa mtoto. Sheria inaweka marufuku kuuza sigara, pombe, madawa, vileo au mvinyo wowote kwa mtoto. Na mtu yeyote atakayepatikana na kosa hili atahukumiwa kifungo kisichozidi mwaka mmoja au kulipa faini isiyopungua shilingi milioni moja za Kitanzania au adhabu zote kwa pamoja. Pamoja na maonyo kwa wamiliki au wapangaji wanaoendesha biashara ya disko, baa au klabu za usiku kutotakiwa kumruhusu mtoto kuingia ndani ya jengo hilo au sehemu ya biashara hiyo. Wauza maduka vilevile wamo hatarini wanapowauzia watoto bidhaa za vileo.


Wazazi na walezi pia tuache kuwatuma watoto madukani kununua vilevi.Ingawa adhabu tulizokupa hapa zinaonekana za kawaida ni rahisi kwa mzazi / mlezi na mwanajamii yoyote kuzipokea katika maisha ya kawaida ya kila siku pasi kudhamiria. Mfano mzuri ni watoto wanaotusaidia kazi za nyumbani. Wengi wetu waajiri tunavunja hasa sheria ya muda wao wa kazi kwani wanatakiwa kutofanya nyakati za usiku ambazo huanza muda wowote kati ya saa mbili za usiku hadi saa kumi na mbili za asubuhi.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

2 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page