top of page
  • C-Sema Team

Zifahamu changamoto tano za malezi ya mtoto katika balehe (miaka 12 - 14)

Huu ni wakati ambao mabadiliko mengi katika mwenendo wa maisha ya mtoto hujitokeza; madiliko haya hutokana na homoni ambazo hupelekea mabadiliko ya kimwili, kibaiolojia, kiakili, kihisia, na mahusiano yake kijamii pia. Kibaiolojia, wavulana huanza kuota ndevu na nywele makwapani, nk. na sauti zao kuwa nzito. Wasichana nao huota nywele makwapani nk, kunawiri, matiti kukua na huanza kupata hedhi. Mara nyingi watoto hupatwa na wasiwasi kuhusu mabadiliko haya na jinsi jamii inavyowachukulia.


Changamoto za malezi ya mtoto katika balehe

Huu ndio wakati ambapo shinikizo rika huwakumba watoto wengi na kupelekea kujihusisha na tabia zisizofaa kama kutumia pombe, sigara, shisha, dawa za kulevya na hata ngono kutokana na vishawishi kutoka kwa makundi rika. Tabia hizi huibua changamoto nyingi kama vile kupoteza hamu ya kula, msongo wa mawazo, n.k. Katika umri huu, watoto hufanya maamuzi wenyewe kuhusu marafiki, michezo wanayoipenda, mavazi, vitabu watakavyo kusoma, na shule waitakayo; hisia za kujiamini na kujitegemea huongezeka maradufu, ingawa bado uangalizi wa wazazi ni muhimu sana.Muonekano.


Huu ni wakati ambao watoto wanajali muonekano wao wa nje; mavazi, kimo chao, unene/wembamba na mavazi. Yaani mtoto sasa anataka kuwa na staili ya kunyoa/kusuka ya kipekee inayomfurahisha na kumpa kujiamini. Hii ni fursa kwako mzazi kumpa majibu ya kweli kuhusu maadili, haiba, mtazamo halisi wa jamii juu ya muonekano wake, mahusiano, ngono, matumizi ya madawa ya kulevya n.k. Usimungunye maneno anajua.


Usununu (moody) usokuwa na sababu. Mwanao ghalfa tu anakuwa mkali au mkimya na mkorofi asiyetaka kukusikiliza. Humjui tena! Usikate tamaa onyesha kujali kwa dhati mambo yanayohusu maisha yake, shule nk. Mwongoze kufanya maamuzi sahihi huku ukukubaliana na kusimamia maamuzi yake. Muhimu sana ajue kwamba unamsikiliza na unatekeleza makubaliano yenu. Vitendo. Anaegemea zaidi ushawishi wa makundi-rika. Haonekani nyumbani na hata unapokutana naye huwa na wenzake katika mambo yao.


Panga kukutana na wafahamu rafiki zake. Wataalamu wa malezi wanashauri uweke bidii katika kuwafahamu marafiki wa mtoto wako kwani mustakabali wake uko juu ya maamuzi yao. Ukiweza kupenyeza na kuwasoma basi sehemu kubwa ya wasiwasi wako imejibiwa. Wafanye sehemu ya familia na nyumbani kwako iwe kijiwe chao.Mtoto kukata tamaa na kukosa ari ya kusoma. Msongo wa mawazo unaotokana na kutojua majibu ya maswali mengi aliyonayo mtoto hupelekea kupoteza mwelekeo na hata kukata tamaa. Zungumza naye huku ukijiepusha na makaripio.


Namna hii atapata faraja na kuelewa kuwa yuko katika umri wa mpito na kuwa sasa utu uzima unaingia na majukumu yanazidi kuwa mengi. Afahamu kuwa wewe ni kimbilio lake na anaweza kukueleza changamoto zake na ukakubaliana na mapendekezo ya namna ya kuzitatua toka kwake.Afya. Wataalamu wa malezi wanashauri kuwa michezo inaweza kuwa sehemu nzuri ya kupunguza msongo na upweke waupatao watoto wa rika hii. Acheze shuleni na hata mtaani panapo fursa ya kufanya hivyo.


Anaweza pia kufua nguo, kufyeka/kusafisha uwanja wa nyumbani alimuradi yuko katika shughuli mojawapo ya kuamsha viungo. Punguza muda unaomruhusu kutizama runinga au kutumia kompyuta isizidi masaa mawili tu kwa siku.Mwisho, afya ya mtu awaye-yote hutegemea chakula anachokula. Muda wa kuketi mezani kupata chakula ni wa muhimu sana kwa mtoto umri huu kwani utakusaidia kumhimiza kula vyakula sahihi. Ifahamike kuwa watoto umri huu hutamani kula vyakula waonavyo katika sinema, matangazo ya bishara na runinga. Vyakula namna hii mara nyingi huwa havina uwiano wa mlo kamili.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

1 view

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page