Hii ni sehemu ya pili ya makala haya juu ya chanjo. Makala haya yanachambua maandiko mbalimbali toka Mpango wa Taifa wa Chanjo ulioanzishwa ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa chanjo katika maisha ya mtoto. Leo tutaendelea na chanjo za surua, kichaa cha mbwa, dondakoo, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo na nimonia.
Surua ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoenea kwa haraka. Ugonjwa huathiri watu wa rika zote, lakini watoto wenye umri chini ya miaka mitano huathirika zaidi. Ugonjwa wa surua huenezwa kwa njia ya hewa hasa pale mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya na maambukizo huwa ni ya haraka sana hasa sehemu zenye msongamano. Ugonjwa wa surua kwa watoto huzuilika kwa chanjo ya surua. Mtoto hupata sindano mbili za kumkinga na surua ambayo hutolewa kwenye bega la kushoto akamilishapo umri wa miezi tisa na marudio baada ya mtoto kutimiza miezi 18.
Kichaa cha mbwa ni ugonjwa unaowapata paka au mbwa endapo mnyama wa porini mwenye ugonjwa atamuuma mbwa au paka ambaye hajapata chanjo. Watoto na hata watu wazima wanaweza kuambukizwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa baada ya kuumwa na mbwa au mnyama wa porini mwenye ugonjwa huo. Wapatie chanjo ya kuzuia ugonjwa wa kichaa cha mbwa wanyama wa nyumbani kama vile mbwa na paka kila baada ya miezi 6 ili wasipatwe na maradhi haya.
Dondakoo ni ugonjwa unasababishwa na vimelea vinavyoshambulia sehemu za koo na huenezwa kwa njia ya hewa, mate au majimaji yanayotoka kwenye sehemu za maambukizo. Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kuwa na vidonda kooni, kutoa kamasi iliyochanganyika na damu na kuwa na maumivu wakati wa kumeza chakula. Ugonjwa huu unawapata watoto wadogo. Hakikisha mtoto anapata dozi tatu za chanjo ya kuzuia Dondakoo ili kumpa kinga kamili.
Homa ya uti wa mgongo na kichomi husababishwa na vimelea aina mbalimbali na huathiri zaidi watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Magonjwa haya huambukizwa kwa njia ya matone ya mate yenye uambukizo kutoka kwa mtoto anayekohoa au kupiga chafya. Vilevile huenea kwa kubadilishana vitu vya kuchezea kama vile midoli na vitu vingine vilivyowekwa mdomoni. Muda wa maambukizo mpaka ugonjwa ujitokeze ni siku 2 - 4, hapo ndipo dalili za awali hutokea. Magonjwa haya ni hatari kwani huathiri mfumo wa fahamu na kupelekea madhara kama kutosikia vizuri, upofu, mtindio wa ubongo na hata kusababisha kifo cha mtoto. Hakikisha mtoto anapata chanjo ya kuzuia magonjwa haya.
Nimonia huenea kwa njia ya hewa wakati mtu mwenye vimelea anapopiga chafya au kukohoa. Ugonjwa huu pia unaweza kuambukizwa kwa njia ya kugusa sehemu zenye vimelea vya maradhi haya kama nguo, leso, vikombe, vitu vya kuchezea watoto nk. Mpeleke mtoto akapate chanjo ya nimonia akamilishapo umri wa wiki sita.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.