top of page
  • C-Sema Team

Yajue magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kwa watoto


Chanjo wanazopata watoto

Makala haya yanachambua maandiko mbalimbali toka Mpango wa Taifa wa Chanjo ulioanzishwa ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa chanjo katika maisha ya mtoto.


Nchini Tanzania magonjwa yanayokingwa kupitia kwa chanjo ni polio, kifua kikuu, pepopunda, dondakoo, kifaduro, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, surua, nimonia na rotavirus. Huduma za chanjo ni mkakati muafaka katika kutokomeza maradhi tajwa hapo juu na kupunguza vifo vya watoto na akina mama nchini Tanzania. Hivyo basi chanjo ni muhimu katika uhai na maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla. Kila mzazi/mlezi hana budi kuhakikisha mtoto anapatiwa chanjo zote ili kumkinga na magonjwa yanayokingwa kwa chanjo.


Kifua kikuu ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya bakteria na huenezwa kwa njia ya hewa. Mtu mwenye maambukizi ya kifua kikuu akikohoa, kupiga chafya au kutema mate ovyo husambaza vijidudu hivyo hewani na huweza kumwambukiza mtu mwingine. Ugonjwa huu unakingwa kwa chanjo ya kifua kikuu (BCG), ambayo hutolewa mara tu mtoto anapozaliwa au anapofika kliniki kwa mara ya kwanza. Iwapo kovu halitajitokeza chanjo irudiwe katika kipindi cha miezi 3. Mzazi au mlezi hakikisha kila mtoto anapozaliwa anapata chanjo ya kuzuia kifua kikuu kwani itamkinga dhidi ya ugonjwa huu.


Ugonjwa wa polio husababishwa na virusi vya polio, ambavyo huenezwa kwa njia ya kula na kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi. Unaweza kuwapata watu wa rika zote lakini watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 ndio wanaoathirika zaidi. Ugonjwa huu hushambulia mishipa ya fahamu hatimaye husababisha kupooza kwa misuli, hasa ya miguu, mikono au yote kwa pamoja, na pengine misuli ya kiwambo (diaphragm) na kusababisha kifo. Kila mtoto mwenye umri chini ya mwaka mmoja ni lazima awe amekamkilisha chanjo ya kuzuia ugonjwa wa polio kwa kupata matone mara nne ili kupata kinga kamili. Yaani chanjo ya kwanza mara tu azaliwapo, ya pili akiwa na wiki sita, ya tatu katika wiki ya 10 na ya nne akiwa na wiki 14.


Pepopunda ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya bacteria vinavyoitwa clostridium tetani. Vimelea hivi huingia mwilini kupitia kwenye kidonda au jeraha. Ugonjwa huu huwapata watu wa rika zote. Kwa watoto wachanga toka kuzaliwa hadi kufikia umri wa siku 28, vimelea huingia mwilini kupitia kwenye kitovu kilichokatwa kwa kutumia kifaa chenye maambukizi, kama vile wembe, mabua na usinge au kuwekwa vitu vichafu kama vile kinyesi cha ngombe, vumbi la kizingitini na kadhalika.


Je, unajua kwamba ugonjwa wa pepopunda hauna tiba? Ugonjwa huu unaua takribani watoto wote wanaoupata! Ni muhimu wanawake wote wenye umri wa kuzaa kati ya miaka 15 hadi 49 wapate chanjo kamili dhidi ya ugonjwa wa pepopunda, ili kumkinga mtoto atakayezaliwa. Zingatia usafi wakati wa kuzalisha, kukata na kutunza kitovu. Kuzuia maambukizi, kitovu cha mtoto kisiwekwe kitu chochote. Wazazi/walezi watunze kadi ya chanjo ya pepopunda kwa ajili ya kumbukumbu.


Kifaduro ni ugonjwa unaoambukiza na kusababishwa na vimelea vya bacteria ambavyo huitwa Bordetella pertusis. Ugonjwa huu huenezwa kwa njia ya hewa na huwapata hasa watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja. Kifaduro huzuiwa kwa chanjo yenye mchanganyiko wa chanjo za kuzuia dondakoo, pepopunda, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo na kichomi yaani DTP-HepB-Hib ambayo kwa kitaalamu hujulikana kama Pentavalent. Chanjo ya kwanza hutolewa katika umri wa wiki sita, ya pili ni katika wiki 10 na ya tatu akiwa na umri wa wiki 14.


Hii ni sehemu ya kwanza ya makala haya juu ya chanjo. Juma lijalo tutaendelea na chanjo za surua, kichaa cha mbwa, dondakoo, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, nimonia, na kadhalika.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.

2 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page