top of page
  • C-Sema Team

Watoto wadogo huuliza mama zao zaidi ya maswali 300 kila siku


Wengi mtakubaliana nasi kuwa watoto wadogo hasa wale wanaonza kujua kuongea (miaka miwili hadi miaka minne) huwa na maswali chungu nzima wakiwa na shauku kubwa ya kujua mambo. Utatfiti uliofanywa nchini Uingereza na kuchapwa katika makala ya gazeti la The Telegraph mwaka 2013 ulibaini kwamba kwa wasatani watoto wa umri huu huwauliza mama zao maswali zaidi ya 300 kwa siku. Vilevile tafiti mbalimbali za makuzi ya watoto zinaonyesha uwezekano wa maswali kukaribia 400 kwa siku. Ungana nasi kujua ni nini watoto hutaka kujua?


Ukweli ni kwamba wasichana na wavulana hutofautiana kwani utafiti huu pia uligundua wasichana huwa wenye shauku kubwa ya kujua mambo zaidi ya wavulana kiasi ambacho kwa wastani wao huwa na swali kila dakika, kwa wastani maswali 390 kwa siku!


Toka wanapoamka akina mama huanzwa na maswali na watoto huwa na maswali mengi zaidi wakati wa kula chakula. Maswali mkiwa njiani kuelekea dukani. Hata wakati mtoto anakwenda kulala bado huwa anauliza maswali hadi usingizi unapomzidia. Ingawa yapo maswali magumu kwa uchache, mengi ya maswali ya watoto huwa rahisi kujibu mfano, wanataka kujua kivuli kinatoka wapi? Majina ya vitu vipya wanavyoviona mara ya kwanza, mama hii ni nini? Majina ya watu/mahusiano, huyu ni nani?


Jambo la kushangaza ni kwamba ingawa akina baba nao hupata maswali toka kwa watoto hawa, zaidi ya asilimia 80 ya watoto hawa hupendelea zaidi kwenda kwa mama wakiwa na maswali. Moja ya sababu zilizotolewa na tunakubaliana nazo ni kuwa watoto wanajua wakienda kwa baba na maswali yao, baba zao hujibu muulize mama yako. Sababu nyingine ni ya kimahusiano. Watoto wengi wa umri huu wanakaa zaidi na mama zao zaidi ya baba zao. Hivyo mahusiano baina yao yako-kirafiki na yenye ukaribu zaidi ya ule walionao na baba zao.


Jambo zuri hapa ni kuwa watoto wadogo huja na kurasa zisizo na maandishi ya aina yeyote. Hii ni fursa nzuri mno kwa wazazi makini kuanza kuandika ndani ya vichwa vyao aina ya binadamu wanayemtarajia toka kwa huyo mtoto wao. Iwapo mtoto anakuuliza maswali na majibu yako si ya staha basi unamuandaa kuwa na tanuru la lugha zisizofaa na kutukana kusikoisha. Badala yake iwapo utaitumia fursa hii kumuelekeza kwa weledi na kujenga misingi ya nidhamu, utalitendea haki jukumu la malezi.


Tabia za kusema watoto wa siku hizi hawana nidhamu ziendane na wazazi wa siku hizi hawafundi nidhamu. Nidhamu na maadili mema kwa binadamu havipatikani kwa nadharia ya ajali. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, kwamba ukosefu wa nidhamu ni matokeo ya malezi ya aina hiyo.


Pongezi za dhati tunazitoa kwa akina mama wasiochoka kukaa na viumbe hawa wenye kila aina ya swali. Pongezi za kipekee ni kwa akina mama wanaojitahidi kujibu maswali kadiri wanavyoweza. Hasa wale wanaowaambia watoto ukweli iwapo swali wanalouliza hawalijui jibu lake. Watoto wanajifunza kujua kwamba mama//baba hajui kila jambo na kwamba kutokujua jambo si kosa. Kamwe usidanganye, akijua atapoteza Imani juu yako jambo ambalo ni baya kabisa katika malezi.


Akina baba nanyi tunao ujumbe kwenu. Kweli mmeshindwa kupata walau vijidakika katika siku nzima walau kujibu hata maswali 10 tu ya mtoto? Mpunguzie mama zigo la malezi kwa kujenga mahusiano na mtoto. Jitihada zako za kulipa ada na kununua unifomu hazitafaa lolote iwapo hazitoandamana na ujenzi wa tabia kupitia mahusiano, mazungumzo na malezi makini kwa ujumla. Yapo maswali unaweza kujibu bila hata ya kusema ‘nenda kamuulize mama yako.


Wanajamii tutoe wito. Unapopata fursa ya kukutaana na mtoto mdogo iwe dukani, shuleni na hata mtaani tumia fursa hii kujenga taifa makini kwa kufunda maadili kupitia mazungumzo na mtoto wa umri huu.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.

3 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page