Vipimo vya ujauzito.
Vipimo vya ujauzito vinaweza kukusaidia kujua kama wewe ni mjamzito au la. Hapa kuna maswali yatakayokusaidia kujua jinsi vinavyofanya kazi na utafaidika navyo kwa jinsi gani? Tembea nasi katika makala haya hapa.
Je, kipimo cha ujauzito kinafanyaje kazi?
Kipimo cha ujauzito hupima kiwango cha kichocheo (hormone) cha hCG (human chorionic gonadotropin) kwenye mkojo au kwenye damu. Kichocheo hiki hutengezwa na mwili wako baada ya yai lililorutubishwa kujipandikiza katika ukuta wa mji wa mimba.
Mchakato huu hutokea siku ya sita (6) baada ya kurutubishwa kwa yai. Kiwango cha kichocheo cha hCG huongezeka kwa haraka sana, yaani huongezeka mara mbili kila baada ya siku 2 au 3.
Je, ni vipimo vipi hutumika kutambua ujauzito?
Kuna vipimo vya aina mbili kuu vinavyotumika kupima ili kutambua kuwa mwanamke ni mjamzito navyo ni kipimo cha mkojo na kipimo cha damu.
Kipimo cha damu.
Hivi siyo vipimo vilivyozoeleka kupima ujazito kwani hapa Tanzania mara nyingi ujauzito hupimwa kwenye mkojo. Moja ya manufaa ya kipimo cha damu ni kuwa kinaweza kutambua ujauzito mapema zaidi, yaani siku 6 mpaka 8 baada ya kutungwa kwa mimba. Hata hivyo majibu yake huchukua muda kidogo kuliko yale ya kipimo cha mkojo cha nyumbani.
Aina mbili za vipimo vya damu vya kutambua ujauzito ni kama ifuatavyo:
Kupima uwepo wa kichocheo (hormone) cha hCG (human chorionic gonadotropin). Hiki hupima uwepo wa hCG kwenye mkojo. Kama hCG ipo basi ujauzito upo na kama haipo basi ujauzito haupo. Madkatri hutuma maabara za kipimo hiki ili kujiridhisha kama kuna ujauzito au la. Kipimo hiki huonesha uwepo wa ujauzito siku 10 baada ya kutungwa kwa mimba.
Kupima wingi wa kichocheo cha hCG. Kipimo hiki hupima wingi wa vichocheo vya hCG vilivyopo kwenye damu na kinaweza kuonyesha hata kiwongo kidogo mno cha hCG kilichopo kwenye damu. Kipimo hiki pia kinaweza kugundua matatizo kipindi cha ujauzito. Daktari wako anaweza kukitumia pamoja na vipimo vingine kutambua kama ujauzito ulitungwa nje ya kizazi, n.k.
Kipimo cha mkojo.
Kipimo hiki kinaweza kufanyika nyumbani au hata maabara.
Pamoja na kuwa kipimo hiki ni rahisi na cha faragha pia ni kipimo cha haraka. Ni kipimo ambacho ni cha uhakika kama utafuata kanuni zake rahisi. Kumbuka vipimo vyote hivi hufanya kazi katika mfumo mmoja. Unapimaje sasa? Fanya yafuatayo.
Weka mkojo wako kwenye kikopo safi kisicho na mafuta au kemikali yeyote ile. Kisha weka sehemu ya kupimia kwenye mkojo wako ndani ya kikopo (sehemu ya kupimia kama ilivyooneshwa / elekezwa kwenye kipimio).
Shika sehemu ya kupimia ya kipimio chako kisha ukiwa unakojoa kiweke kwenye mtiririko wa mkojo ili kilowane.
Baada ya kufanya hivyo kusubiri kwa muda wa dakika kadhaa ili kuona majibu. Baada ya kupata majibu unahitaji kuyathibitisha kwa kumwona daktari wako atakayekufanyia vipimo zaidi.
Je, vipimo hivi vya kupima ujauzito ni sahihi kwa kiwango gani?
Vipimo hivi vya mkojo ni sahihi kwa asilimia 99. Kisha vipimo vya damu vya kupima ujauzito ni sahihi zaidi ya asilimia 99.
Fahamu mambo yanayoweza kuhafifisha ufanisi matokeo ya vipimo vya ujauzito vinavyofanyika nyumbani.
Umakini wakati wa upimaji kwa kuzingatia hatua moja kwenda nyingine kama inavyotakiwa. Soma maelekezo ya kipimo chako na yafuate kwa usahihi.
Ni lini yai lilipopevuka na ni mapema kiasi gani ambapo yai lililorutubishwa lilijipandikiza kwenye mji wa mimba (uterus).
Inategemea ni mapema kiasi gani baada ya mimba kutungwa umepima kipimo chako cha ujauzito.
Wepesi wa kipimo hicho cha ujauzito kutoa majibu.
Je, ni wakati gani muafaka kufanya kipimo cha kutambua kama ni mjamzito?
Baadhi ya vipimo vya ujauzito huweza kutambua uwepo wa kichocheo cha hCG hata kabla hujakosa kuona siku zako (hedhi). Inashauriwa ili kupata matokeo ya uhakika zaidi ni bora kupima ujauzito kuanzia siku moja baada ya kukosa kuona siku zako (hedhi).
Matokeo yanawe
za kuwa mazuri zaidi kama utachukua kipimo chako asubuhi kabla hujaanza kufanya kitu chochote kwani wakati huo kiwango cha kichocheo cha hCG katika mkojo wako kiko juu zaidi.
Je, ni wapi nitapata kipimo cha ujauzito cha nyumbani?
Unaweza ukanunua stripu kwa ajili ya kupima ujauzito kwenye duka la dawa bila ya kuandikiwa na daktari. Gharama ya kipimo inategemea ubora wa kipimo chenyewe. Vipimo vya aina nyingi huwa siyo ghali.
Je, nitaweza kusoma majibu na kuyaelwa?
Majibu huonekana kwa kutokea kwa mistari miwili yenye rangi au kwa alama ya chanya (+) au hasi (-). Vipimo vya ujauzito vya kidijitali huonesha neno (pregnant, ‘ujauzito’) ama (not-pregnant, ‘hakuna ujauzito’). Muhimu ni kujua maana ya majibu chanya au hasi n.k.
Kama utapata majibu chanya, wewe ni mjamzito. Bila kujali kiwango cha mstari au alama kama kimekolea rangi au la – wewe ni mjamzito. Ukishapata majibu chanya unaweza kwenda kwa daktarin ili kujadiliana naye hatua zinazofuata. Anaweza kukupima tena kujiridhisha kuwa u-mjamzito.
Mara chache sana unaweza kupata majibu chanya yasiyo sahihi. Hii inamaanisha kwamba ingawa kipimo kinasema ewe ni mjamzito, kiualisia huna ujauzoto. Unaweza kupata majibu chanya yasiyo sahihi kama mkojo wako utakuwa na protini au kuwa na damu. Baadhi ya dawa kama vile dawa za kifafa, degedege na dawa za kusaidia urutubishaji wa mayai zinaweza kusababisha ukapata majibu chanya yasiyo sahihi.
Kama majibu yako ni hasi, inawezekana wewe sio mjamzito. Hata hivyo bado unaweza kuwa mjamzito endapo:
Kipimo kimeshapita muda wake wa kufanya kazi (kipimo ‘kime-expaya’).
Uligeuza kipimo wakati wa kupima ukapimia sehemu isiyo sahihi.
Ulipima mapema sana baada ya kuwa mjamzito.
Kipimo chako kina maji mengi kwa sababu ya kunywa vinywaji vingi kabla ya kufanya kipimo.
Kama unatumia baadhi ya dawa mathalani dawa za shinikizo la damu la juu (za kiudiuretiki kama Lasix) au dawa za antihistamines kama vile piritoni na n.k.
Kama umepata majibu hasi, jaribu jaribu kupima tena ndani ya wiki moja. Baadhi ya vipimo kutoka katika kampuni kadha wa kadha hupendekeza kurudia kupima mara ya pili bila ya kujali maijbu yako ya awali yalikuwa vipi.
Iwapo utapima mara ya pili na ukapata majibu tofauti na yale ya awali, inashauriwa umuone daktarin ili kupata kipimo cha damu. Namna hii itathibitishwa pasi na shaka juu ya swala la ujauzito wako.
Kama una swali lolote lile kuhusu kipimo cha ujauzito au majibu wasiliana na daktarin ama nenda hospitali.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org
Comments