top of page
  • C-Sema Team

Usalama wa mtoto wako wakati wa dharura

Kama mzazi, afya na usalama wa mtoto wako unavipa kipaumbele. Kila siku, unahakikisha kuwa mtoto wako anakula vizuri, anapumzika vya kutosha, anakunywa maji ya kutosha na ana muda wa kucheza. Natumai kuwa unampeleka kupima afya yake mara kwa mara.



Watoto wengi wanapenda kucheza na kugundua mambo mapya, na wakati mwingine hupenda kujaribu mambo ambayo huweza kuwadhuru kiafya. Mikwaruzo ya hapa na pale ni kawaida na kwa watoto watundu sana, si ajabu mtoto kuvunjika kiungo angali mdogo katika harakati za kucheza.



Lakini je, dharura ikitokea umejipanga vizuri kuhakikisha mtoto anaweza kutibiwa haraka na kwa usalama iwezekanavyo hata kama wewe uko mbali?


Mara nyingi dharura ikitokea sio rahisi kukumbuka taarifa muhimu. Hivyo ni vyema kuandika taarifa muhimu kuhusu afya ya mtoto wako sehemu zinapoweza kusomeka kirahisi. Unaweza kuweka taarifa zipi? Tuna mapendekezo machache.


Magonjwa & Mzio(Allergy) Je, mtoto wako ana pumu, kisukari au anemia (upungufu wa damu)? Taarifa kuhusu magonjwa yoyote ni muhimu sana na zinaweza kuwasaidia madaktari kufanya maamuzi hasa wakati wa dharura. Ni muhimu pia kuwa na taarifa za kiafya za familia hasa kama kuna historia ya matatizo ya kiafya. Taarifa hizi zitawasaidia madaktari kujua vipimo vya kuchukua na kufanya maamuzi ya haraka.


Kuna dawa zinazomuathiri mwanao? Usiache kuweka taarifa hiyo pia. Baadhi ya watoto huathiriwa na dawa za aina fulani kwa sababu ya viambato vilvyomo. Hakikisha unaweka kumbukumbu kama kuna dawa iliyomuathiri mtoto wako ili kuepuka matumizi ya dawa hiyo baadaye.


Mzio unaweza pia kusababisha uvimbe, kuwashwa sana, na matatizo ya kupumua. Orodha ya vitu vinavyomsababishia mwanao mzio inaweza kuwasaidia madaktari au walezi kujua ni kitu gani kinamsumbua mtoto.


Mwanao Anatumia Dawa Yoyote kwa Sasa? Ni muhimu kuongeza taarifa hii pamoja na vipimo, muda wa matumizi ya dawa na sababu ya kumeza dawa hiyo. Hii itawasaidia madaktari kujua dawa ya kumpa mtoto wako. Kama mtoto wako amefanyiwa upasuaji, unaweza pia kuweka taarifa hizo.


Taarifa nyingine Inashauriwa pia kuweka kumbukumbu za chanjo ambazo mtoto wako ameshapata. Kama haujahifadhi kumbukumbu hizi, jaribu kuzifuatilia kwa daktari. Usisahau kuweka umri, uzito na aina ya damu ya mtoto wako. Daktari anaweza kukushauri zaidi kuhusu taarifa nyingine muhimu za kuorodhesha.


Kama mtoto wako sio mdogo sana, unaweza kumshirikisha ukiwa unaandika taarifa hizi ili na yeye awe na ufahamu wa taarifa hizi muhimu. Na wakati unafanya hivyo, kwa nini usiandike taarifa zako pia? Mtoto wako anaweza kuzihitaji ili kukusaidia siku moja.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.

0 views

Recent Posts

See All

Comentários


bottom of page