Ni dhahiri kwamba malezi tuwapatiayo watoto huwa ndiyo msingi wa mustakabali wao. Maisha ya mtu hutegemea sana msingi wa malezi aliyopata tangu angali mchanga. Pia mtu kuacha tabia aliyoizoea katika kipindi cha makuzi yake mara nyingi humuwia vigumu. Kama wazazi, tunaweza kuwaandaa watoto wetu kuwa wasomi wakubwa, madaktari bingwa au hata wafanyabiashara maarufu, lakini pia tunaweza kuwaandaa watoto wetu kuwa wezi, majambazi, wabwia unga na machangudoa.
Kuna wakati ambapo wazazi huwanyima majibu sahihi, kuwafokea au hata kudanganya pindi watoto wanapojaribu kuwahoji au kuwauliza maswali mbalimbali. Hayo ni makosa kwani huo ndiyo muda ambao watoto huutumia kuvumbua mambo mapya zaidi. Si jambo la ajabu sana kushuhudia matukio kadha wa kadha wanayofanyiwa watoto ikiwemo ukatili, mateso, unyanyasaji, udhalilishaji na uonevu ndani ya familia na jamii tunazoishi katika sehemu mbalimbali.
Kama wazazi, ni muhimu kutambua kuwa katika makuzi yao, watoto hujaribu kufanya vitu ambavyo vitawasaidia kukuza maarifa na vipaji vyao, ingawa kwa namna moja ama nyingine njia wanazochagua huweza kuonekana ni mbaya kwa wazazi na pengine nia yao si kufanya makosa bali ni katika harakati za kujifunza au kujifurahisha. Ndiyo maana hata katika kipindi cha uchanga, mtoto huweza hata kula kinyesi chake, au hata kushika moto. Jukumu la kuzitii na kuziheshimu haki za watoto ni la wazazi, kwani ndiyo msingi wa kuwajengea watoto uelekeo bora wa maisha yao, kikubwa ni kupata uelewa mzuri katika kujenga nia na dhamira yenye hamasa ya kutekeleza kwa vitendo.
Baadhi ya machapisho yamekwisha zungumzia kwa kina juu ya maana ya haki za watoto likiwemo chapisho la Azimio la Kimataifa juu ya haki za watoto. Haki za watoto ni haki za binadamu na stahiki za msingi za ulinzi na huduma wanazostahili watoto. Mathalani, haki ya kuishi na kupatiwa mahitaji ya msingi kama vile afya, elimu na chakula, haki ya kulindwa na haki ya kushirikishwa. Ifike wakati wazazi tubebe jukumu la kuheshimu haki za watoto kwa vitendo ili kuwajengea dira wototo kwa manufaa tarajiwa kama ifuatavyo:-
Ni wazi kuwa matukio kama kushurutishwa kufanya kazi, kunyimwa chakula, udhalilishaji, kupigwa, kuteswa pamoja na kudhulumiwa tumekuwa tukiyashuhudia kila kukicha. Hivyo, kama wazazi ni jukumu letu kukemea vitendo hivi kwa nguvu zote.
Haki za watoto ni maalum wakati wote. Hii ni kwa sababu watoto hawapewi fursa ya kujisemea. Yapo mambo mbalimbali yanayoweza kudhihirisha umaalumu wa haki za watoto. Hebu fikiri; Baba akinyimwa chakula na mama nyumbani - anaweza kupika akala au hata kwenda hotelini kula. Lakini hii ni tofauti kwa mtoto wa umri wa miaka mitatu au minne akinyimwa chakula na mama ataweza kupika mwenyewe akala? Atakwenda kula hotelini? Ni wajibu wetu wazazi kuwa mstari wa mbele kulinda na kuheshimu haki zao bila kujali rangi, umri, ama jinsia.
Kama wazazi, ni muhimu sana kuamua kwa vitendo kuwaheshimu watoto tangu wakiwa wadogo, hii itawafanya watoto kukua huku wakifahamu kwamba dunia ni sehemu salama ya kuishi na hivyo kuzifanya akili zao kujikita zaidi katika shughuli za maendeleo kama uzalishaji na kusoma kwa bidii. Vilevile, watoto wakiheshimiwa angali wadogo watajifunza kuheshimu watoto wenzao, watu wazima na kuwa watu wenye kuheshimu wenzao hata ukubwani.
Kuheshimu haki za watoto ni kuwapa nafasi ya kutimiza ndoto za maisha yao, kushiriki katika maamuzi yatakayowaathiri yanayohusu nyanja mbalimbali za kimaisha na kuboresha maslahi yao kwa upana. Watoto ni tunu ya wazazi, jamii na taifa. Tuwaendeleze.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org