top of page
  • C-Sema Team

Uchungu wa uzazi.

Uchungu wa uzazi hutokana na kubana na kuachia (tena kwa kurudiarudia) kwa misuli katika tumbo la uzazi. Misuli hii inavyobana na kuachia taratibu husababisha kufunguka kwa mlango wa tumbo la uzazi. Baada ya mlango kufunguka sasa mtoto anaweza kutoka nje ya tumbo la uzazi na hatimaye nje kabisa kupitia uke wa mama yake.


Kubana na kuachia kwa misuli huanza polepole wakati wa siku za mwisho za ujauzito. Mkazo au mbanano wa tumbo la uzazi mwanzoni hauchukui muda mrefu. Huachia mama anapopumzika.


Unapokaribia kujifungua hapo ndipo uchungu wa uzazi wa kweli huja kwa nguvu. Uchungu huu huanza taratibu na kila baada ya dakika chache. Hauachii hata mama akilala chini au kupumzika.


Kupasuka kwa mfuko wa maji ya uzazi.

Mfuko wa maji ya uzazi unaweza kupasuka na kuachia maji mengi ghafla au kuachia maji kidogo kidogo. Kuachiwa kwa maji ya uzazi kunaweza kuwa ndiyo dalili ya kwanza ya uchungu wa uzazi kabla ya misuli haijaanza kubana na kuachia kwa wajawazito wengine.

Wapo wajawazito ambao maji mengi huachiwa ghafla wakati wa uchungu wa uzazi. Mwisho wapo wengine ambao mtoto huzaliwa kwenye mfuko wa maji bila mfuko huo kukatika. Hali zote hizi ni za kawaida na hazina sababu ya kukuogofya.


Je, mfuko wa uzazi ni nini na unatoka wapi? Mfuko huu upo ndani ya tumbo la uzazu na humlinda mtoto dhidi ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa. Baada ya mfuko kuvunjika vijidudu hivyo vinaweza kusababisha maambukizi kwenye tumbo la uzazi na kwa mtoto. Hivyo ifahamike kuwa hatari ya maambukizi huongezeka kutegemea urefu wa muda ambao mfuko huo utabaki ukiwa umevunjika. Usiweke chochote ukeni baada ya mfuko wa maji ya uzazi kuvunjika.


Iwapo mfuko utavunjika na saa 12 au Zaidi zikapita bila uchungu wa uzazi kuanza basi nenda hospitali mara moja ambapo uchungu unaweza kuanzishwa kwa kutumia dawa.


Kusaidia kuanzisha uchungu wa uzazi

Inayumkinika kwamba unaweza kusaidia uchungu wa uzazi uanze au kuuongeza kasi kama umekuja polepole mno katika hali zifuatazo:

  • Ujauzito ambao umepitiliza siku. Ujauzito wa zaidi ya wiki 41 unaweza kusababisha matatizo kwa mtoto.

  • Mfuko wa maji ya uzazi kuvunjika. Baada ya mfuko wa uzazi kuvunjika saidia kuanzisha uchungu wa uzazi ili kuepuka maambukizi iwapo uchungu haujaanza.

  • Uchungu wa uzazi ambao unaendelea taratibu mno. Saidia kuanzisha au kuongeza kasi ya uchungu wa uzazi ili mama asiishiwe nguvu.

Tumia njia hizi kwa kuanza na njia ya kwanza na kama haitafanikiwa, jaribu njia inayofuata:

  1. Mhimize atembee, kucheza, au kupanda ngazi za ghorofa au kupanda kilima / kimuinuko.

  2. Viringa chuchu zake kama vile unakamua maziwa. Hayo yanapaswa kusisimua misuli kuanza kubana na kuachia.

  3. Changanya robo ¼ kikombe / glasi ya mafuta ya mbarika (castor oil) na aina yoyote ya juisi ya matunda kisha mpe mjamzito anywe. Hii mara nyingi husababisha kuharisha kukiwa na maumivu, lakini pia inaweza kuchochea mwenendo wa misuli kuanza kubana na kuachia.

Huenda kukawa na dawa za mitishamba ambazo hutumika katika familia na jamii inayokuzunguka kuchochea uchungu wa uzazi kuanza. Baadhi ya dawa hizi zinaweza kuwa salama lakini zingine siyo salama. Kabla hujazitumia jiulize kwanza, je mimea hii iliwahi kuwasaidia wanawake wengine kuanzisha uchungu wa uzazi? Vipi upo Ushahidi wa wanawake hawa kupata matatizo ya kiafya baada ya kutumia dawa hizi? Je dawa hizi zimekuwa zikitumika kwa muda mrefu au zimeanza kutumika hivi karibuni? Je uko tayari kuzijaribu – ama unahitaji ushauri wa daktari na wakunga kwanza?


ANGALIZO. Kamwe usijaribu kuanzisha uchungu wa uzazi kama mtoto amekaa upande katikati ya njia ya uzazi. Vilevile usipoteze muda kujaribu kuanzisha uchungu wa uzazi anza safari mapema kuelekea hospitali.


Kamwe usimpe mama mjamzito dawa za oksitosini, misoprosto, au dawa zingine za kiasasa kuanzisha uchungu wa uzazi nyumbani. Dawa hizi ni kali mno –zinaweza kusababisha kifo.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org


Picha ni kwa hisani ya WHO.

35 views

Recent Posts

See All

Comentários


bottom of page