top of page
C-Sema Team

Shule ya kwanza ya mtoto ni nyumbani

Updated: Aug 30, 2023


Utakubaliana nasi kuwa shule ya kwanza katika maisha ya mtoto ni nyumbani wazazi, ndugu wa familia tandaa, majirani na marafiki wa familia husika. Kupitia mzazi/mlezi mtoto anapata nyenzo zitakazoongoza maisha yake yote heshima, utii, unyenyekevu na kadhalika. Yaani wema au ubaya wa mtu mara nyingi ni matokeo ya aliyojifunza nyumbani.


Nyumbani ndiko msingi hujengwa. Bahati nzuri ualimu wa nyumbani unatokana na matendo zaidi ya maneno. Mtoto uko naye kila uchao hivyo badala ya kutumia muda mwingi kutoa maelekezo ya tabia njema. Ishi kwa mfano. Unamwambia mtoto sala na ibada ni muhimu katika maisha wewe unasali? Je, unahudhuria pamoja naye katika ibada? Kupitia maisha unayoishi utamjengea mtoto misingi ya kiakili na kiimani ili kama ilivyo kwa chakula bora awe na uwiano sawia katika maisha.


Fursa ya kujenga tabia na kukuza vipaji. Anapotoka tumboni mwa mama mtoto huwa na kurasa zilizo wazi pasi na tabia za aina iwayo-yote. Isipokuwa kwa vipaji na tabia za kurithi mzazi/mlezi wewe unalo jukumu la kuunda tabia na kukuza vipaji vya mtoto. Ukiwa kama mwalimu wa kwanza wa mtoto mwandae kwa ajili ya elimu ya shule (awali, msingi, sekondari, nk.). Bahati mbaya wazazi/walezi wengi huingia katika shughuli hii wakiwa ndiyo kwanza bado vijana. Lugha za ujana na misemo iliyo mingi huwa bado inazo chembe za utovu wa nidhamu. Ukiwa mzazi mtoto anakusikia, anakuiga. Chagua maneno.


Umoja wa wazazi/walezi ni muhimu sana. Baba na mama wawe wamoja katika kulea. Pale inapotokea tofauti baina yao kuhusu namna ya kutoa maelekezo kwa mtoto basi na wasibishane mbele za mtoto. Ikiwa kwa mfano mama anamwadhibu mtoto na baba hakubaliani na adhabu inayotolewa muombe mama faraghani na mzungumze juu ya hili. Ukomavu namna hii utasaidia kutomchanganya mtoto na jumbe zinazokinzana. Kamwe msikwaruzane mbele za watoto. Tofauti zenu zivumiliwe mpaka mpatapo faragha mbali na watoto.


Elimu ianze umri gani hasa? Elimu inaanza akiwa tumboni kupitia mazungumzo ya mama mtoto anaandaliwa kuzijua sauti za watu wake wa karibu kama baba, mashangazi nk. Hii inakwambia kwamba malezi yanaanza mara tu uwapo mjamzito. Punguza maugomvi yasiyo-lazima na ikiwezekana jenga mazingira rafiki kwa kuwa mwenye furaha wakati mwingi. Mara tu unapomtia mikononi mwako kichanga wako anza kumsemesha. Elimu ya lugha unayotumia ndiyo lugha atakayoanza kuifahamu kichanga wako. Jenga msamiati wenye lugha za staha ili mtoto naye ajifunze hivyo.


Jifunze miongozo ya malezi. Sote tunafahamu kuwa malezi hayana shule eti ukajifunze upate kujua mbivu na mbichi. Nyakati nazo zimebadilika na watu hasa waishio mijini hawakai pamoja na familia tandaa. Hii inamnyima mzazi mpya fursa ya kupata maelekezo ya namna bora ya kulea toka kwa mama au baba yake yeye mwenyewe. Pamoja na changamoto hizi zipo fursa za kujielimisha kupitia vitabu, majarida na makala mfano wa haya. Fursa nyingine adhimu ni mtandao wa intaneti wenye maandiko ya kitaalamu na toka kwa wazazi wa matabaka, makabila na lugha mbalimbali kote ulimwenguni. Jisomeshe.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

2 views
bottom of page