top of page
C-Sema Team

Njia za kuimarisha uwezo wa mtoto wa kike hizi hapa.

Mara kadhaa tumezungumzia umuhimu wa wazazi na jamii kuwapa watoto nafasi sawa bila kujali jinsia. Leo tunawaletea mawazo tuliyopewa na waalimu wa shule mbili za sekondari wilayani Bunda na Kahama. Waalimu hawa wametushirikisha changamoto wanazopitia wanafunzi wao wa kike na wamependekeza njia za kuimarisha uwezo wa mtoto wa kike kujiamini na kujithamini.



Mwalimu Msemakweli alitueleza kuwa siku moja baada ya kuzumguza na wanafunzi wake kwa muda aliwauliza swali, 'Nani maishani mwake anatamani angezaliwa mwanaume?' Cha kusikitisha ni kwamba kati ya wasichana 76 wa kidato cha kwanza, zaidi ya nusu walinyoosha mkono.


Sababu waliyotoa mabinti hawa ni mwanamke kutothaminiwa katika jamii. Mmoja alieleza kuwa mara nyingi ameshuhudia baba, wajomba, na hata kaka zake wakiwapiga wake zao hata kwa makosa madogo na ya kawaida yanayofanywa na wanaume pia. Mwingine alieleza kuwa hapendi namna wavulana wanavyomfuata na kumtongoza tena kwa vitisho sana kana kwamba kuna walichochangia katika mwili wangu.


Binti mmoja alieleza namna mama yake alivyotukanwa na kupigwa makofi na manesi wakati anajifungua. Aliumia sana na kuwaza kuwa hata yeye ni mwanamke hivyo haya yote yanamngojea. Laiti angelikuwa mwanaume, angeweza epuka hili. Sababu nyingine ni nafasi ndogo wanayopewa watoto wa kike kujisomea na kupigania ndoto zao kama ilivyo kwa watoto wa kiume.


Watoto wa kike wanakabiliwa na changamoto nyingi. Kiini cha changamoto hizi ni kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika jamii nyingi hasa za kiafrika kati ya watoto wa kike na wa kiume kuanzia ngazi ya familia.


Ipo dhana potofu katika jamii ambapo wengi huamini kuwa mtoto wa kike hawezi kufanya kitu cha muhimu ukilinganisha na mtoto wa kiume. Dhana hii hutokana na mfumo dume uliotawala katika jamii nyingi. Jamii zimekuwa zikiamini kuwa mtoto wa kiume ni muhimu sana kuliko wa kike na hivyo hupewa kipaumbele na fursa katika nyanja zote ikiwemo kupata elimu.


Hata hivyo changamoto zinazowakabili watoto wa kike zinatatulika. Mwalimu Theresia anapendekeza mambo yafuatayo ili kuwasaidia watoto wa kike kuimarisha uwezo wao na kujiamini.


Mosi, ni lazima suala la elimu lipewe kipaumbele kwa mtoto wa kike. Waalimu wanatakiwa kufanya bidii ili kuleta usawa baina ya wavulana na wasichana kwenye suala la elimu. Kuwahamaisha kupenda elimu na kumpa moyo katika masomo yake ni mojawapo ya mbinu za kumuimarisha mtoto wa kike, kwani itamfanya ajione yuko sawa na mtoto wa kiume.


Pili, elimu ya utambuzi ni muhimu sana. Mtoto wa kike anatakiwa kukumbushwa kuwa yeye ni sehemu ya jamii na hivyo kazi yake sio kuzaa pekee. Nasema hivyo kwa sababu baadhi ya maeneo kama Kanda ya Ziwa mwanamke alikuwa hasomeshwi, kisha akikua kazi yake ni kuolewa na kuzaa watoto. Hii sio sawa, mtoto wa kike anatakiwa aelimishwe anawajibika kuijenga jamii yake kwa namna nyingi sio kuzaa pekee. Anatakiwa kutambua mchango wake kwa jamii upo kiuchumi na kadhalika, aeleza Mwalimu Theresia.


Tatu, kampeni zinaweza kusaidia wanajamii kuondokana na dhana potofu ya kuwa mtoto wa kike hana thamani sawa na mtoto wa kiume. Asasi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali kama vile FEMINA HIP, TAMWA, TGNP zinaweza kutoa elimu kwa jamii ya thamani ya watoto wote; wa kike na wa kiume. Vilevile, wazifahamishe jamii namna ya kuripoti matukio yanayohusu unyanyasaji wa mtoto wa kike.


Mwisho, mwalimu Theresia anapendekeza ajira ya wasishana wa ndani ipigwe vita nchi nzima. Inatakiwa kuwepo sheria inayoelekeza au kutoa mwongozo wa ajira za wasichana wa ndani. Kwamba sheria itamke wazi kuwa msichana aliye chini ya miaka 18 asiajiriwe kufanya kazi za ndani. Hii itachangia sana jamii nzima kumthamini mtoto wa kike na kumuongezea nafasi mtoto wa kike kufikia ndoto zake.


Baada ya kuona changamoto zinazowakabili watoto wa kike na kuona jinsi wanafunzi wake walivyofadhaishwa na changamoto hizi, Mwalimu Msemakweli ameanzisha programu ya kuwasaidia wajitambue na waanze kufurahia kuwa mabinti. Anawashirikisha watoto wote; wa kike na wa kiume, katika programu hii ili kuwajengea dhana ya usawa, kujiamini na kuheshimiana wakiwa bado wadogo.


Mwalimu Theresia amalizia kwamba mtoto wa kike anatakiwa kuthaminiwa katika nyanja zote na apewe nafasi kushiriki kama haki yake kikatiba (na kibinadamu). Wito wetu kwa msomaji wa leo: tumia nafasi uliyonayo iwe nyumbani, shuleni, kazini, ama katika jamii; kuondoa changamoto zinazomkabili mtoto wa kike kutokana na ubaguzi. Usisite kuzungumza na waalimu maana wao hutumia muda mwingi sana na wanafunzi na wanaweza kuwajengea watoto dhana chanya ya usawa wa kujinsia wakiwa na umri mdogo.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

29 views
bottom of page