Sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inatoa ufafanuzi kuwa mtoto ni mtu aliye na umri chini ya miaka 18. Kimsingi, ndoa za utotoni ni muungano ambapo kati ya bibi au bwana harusi mmojawapo huwa chini ya umri wa miaka 18. Ndo hizi huchochewa na baadhi ya tamaduni, dini na mara nyingine huwa ndoa zisizo rasmi. Mara nyingi mhanga huwa ni binti mdogo anayeozeshwa kwa mwanaume mwenye umri wa kumzidi binti huyo.
Inasikitisha sana kuwa kwa kiasi kikubwa, bado haki za watoto hukiukwa duniani kote ikiwemo kuwaozesha watoto. Licha ya sheria na mikataba mbalimbali ya Kimataifa kukataza ndoa za utotoni, ndoa hizi zimethibitika kuwa bado ni tatizo katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania. Takwimu za Utafiti wa Demografia ya Afya wa mwaka 2016 hapa nchini (TDHS), zilionyesha kuwa asilimia 36 ya mabinti wenye miaka 20 hadi 24 waliolewa kabla hawajatimiza umri wa miaka 18.
Tafiti mbalimbali zimeonesha ndoa za utotoni ziko zaidi vijijini, pindi zinapotokea mijini basi hutokea hasa kwa familia masikini sana na katika familia zenye imani kali za kidini na kimila. Kwa ujumla, wasichana kutoka familia zenye kipato cha chini sana wana uwezekano mkubwa wa kuolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 kuliko wasichana wanaotoka kwenye familia zenye kipato cha juu.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia ya Afya nchini (TDHS) wa mwaka 2010 mikoa yenye viwango vikubwa vya ueneaji wa ndoa za utotoni hapa nchini ni Shinyanga (59%), Tabora (58%), Mara (55%) na Dodoma (51%). Hii ni sawa na kusema kuwa kwa wastani, wasichana wawili kati ya watano huolewa kabla hawajatimiza umri wa miaka 18.
Umasikini pamoja na ubaguzi wa kijinsia (mtoto wa kike) ndiyo hasa huchochea vitendo hivi ambavyo vina madhara makubwa. Aidha, ndoa za utotoni ni suala linaloathiri haki za wasichana zaidi na kwamba haki hizi zinapuuzwa huku matokeo yanayotokana na vitendo hivi yakizidi kuumiza idadi kubwa ya mabinti. Ndoa hizi ni za kulazimisha na hupelekea idadi kubwa ya watoto wa kike kukatishwa masomo yao ili wakaolewe huku mabinti hawa wakinyimwa nafasi ya kuzungumza chochote katika uendeshaji wa maisha yao wenyewe.
Ni muhimu kutambua kwamba ndoa za utotoni haziwaathiri watoto wa kike pekee, bali zina madhara kwa familia, jamii na nchi kwa ujumla. Wasichana wasio na elimu au ujuzi wa kitaalamu wana uwezekano mdogo sana wa kuongeza kipato katika familia na huendeleza mzunguko wa umasikini ambao utaathiri maendeleo ya watoto, familia zao na Taifa kwa ujumla.
Vilevile, ndoa za utotoni huweza kupelekea athari za kiafya kwa mabinti kwa kuwa wengi hupata mimba wakiwa bado na umri mdogo huku miili yao ikiwa haijapata uwezo wa kubeba mimba na kujifungua salama. Hii huweza kuhatarisha maisha ya mama na hata kichanga chake.
Zipo jitihada mbalimbali za kuhamasisha mabadiliko ya sera zinazomkandamiza binti ili kuhakikisha kuwa usawa baina ya watoto wa kike na wa kiume unapatikana kuanzia ngazi ya familia. Kama wazazi, walimu, walezi na wanajamii, tunayo nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko kwa kuelimishana kuhusu athari ya ndoa za utotoni, kukemea na kushtaki pale tuonapo mtoto anakatishwa masomo na kulazimishwa aolewe.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania