top of page
  • C-Sema Team

Namna ya kuwalinda watoto dhidi ya ukatili mtandaoni

Mwanzoni mwa wiki hii kwa kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tulizindua tovuti maalumu ya kutoa taarifa za picha na video zenye maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto. Watumiaji wa intaneti Tanzania bara na Zanzibar sasa wana uwezo wa kutoa taarifa za unyanyasaji wa kingono kwa watoto mtandaoni, pasi kujulikana.


Mara nyingi tumeona picha na video za watoto wakifanyiwa ama kuhojiwa kuhusu ukatili wa kingono zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Facebook na Instagram. Sababu za kusambaza ni nyingi; wengine hudhani kusambaza ndio kumsaidia mtoto alieathirika na kitendo hiki, wengine husambaza maudhui hayo iwe angalizo na fundisho kwa wanajamii wakiwataka wawalinde watoto. Wapo pia wale ambao hurekodi na kusambaza maudhui haya ikiwa ni burudani na hata biashara.


Ingawa mara nyingi tumezoea kusambaza picha hizi kwa nia njema kabisa ya kuwasaidia watoto na kuionya jamii, usambazaji wa picha hizi humuumiza mtoto zaidi na sio kumsaidia kama tulivyodhamiria. Kila picha ama video yenye maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa mtoto inapopakiwa, inaposambazwa au inapotazamwa, mtoto huyo huathirika na unyanyasaji huo upya. Huyu ni mtoto alie hai na amepitia ukatili wa kutosha.


Watumiaji wa mitandao nchini Tanzania wanaweza kusaidia kulinda watoto walioathirika na unyanyasaji wa kingono kwa kutoa taarifa za picha au video zenye maudhui haya wanapokumbana nazo mtandaoni. Tovuti hii ya kutolea taarifa ya Internet Watch Foundation (IWF) itasaidia kuhakikisha kuwa watoto walioathirika na ukatili wa kingono hawapitii unyanyasaji zaidi kwa picha za unyanyasaji wao kusambazwa mitandaoni.


Tovuti ya kuripoti picha hizi ina kitufe cha kutolea taarifa kinachotuma taarifa hizi moja kwa moja kwa wachambuzi wataalam wa IWF, nchini Uingereza. Wachambuzi hawa huchunguza taarifa hizi na kuondoa maudhui yenye unyayasaji wa kingono kwa watoto (kinyume na sheria).


Iwapo utakutana na picha/video ya mtoto anaefanyiwa ukatili wa kingono, tafadhali usiisambaze kwa wengine na usiipuuze. Toa taarifa ya picha hii kwa kutembelea https://report.iwf.org.uk/tz na kujaza fomu fupi ya taarifa. Itakuchukua sekunde chache tu na utakua umesaidia wachambuzi kutathmini na kuchukua hatua dhidi ya maudhui yoyote yanayokiuka sheria kwa kuonesha unyanyasaji wa kingono kwa watoto.


Ikiwa picha au video ina maudhui yanayokiuka sheria, mchambuzi hushirikiana na mtandao wa washirika ili kuhakikisha maudhui hayo yanaondolewa mtandaoni duniani kote. Hii huhakikisha usalama wa watumiaji wa mtandao na huwalinda waathirika kwenye picha dhidi ya unyanyasaji zaidi kwa kusambazwa kwa picha zao.


Picha za unyanyasaji wa kingono kwa watoto ni tatizo la kimataifa linalohitaji ufumbuzi wa kimataifa ili kulitatua. Tunataka watumiaji wa intaneti Tanzania wasikutane na picha hizi zenye maudhui ya kutisha. Hata hivyo, ikiwa wamekutana nazo mtandaoni, tunataka wafahamu kuwa kuna mahali salama ambapo wanaweza kutoa taarifa juu ya picha walizoziona,” alieleza Susie Hargreaves OBE, Afisa Mtendaji Mkuu wa IWF.


Mwaka 2016 katika visiwa vya Cayman vilivyopo katika Bahari ya Caribbean, simu ya mtuhumiwa mmoja ilichukuliwa baada ya msamaria mwema kutoa taarifa kuhusu maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto katika tovuti yao. Vyombo vya usalama na IWF walishirikiana kutathmini taarifa hizi pamoja na simu ya mtuhumiwa. Hatimae mtuhumiwa alishtakiwa kwa makosa kadhaa ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto na kuhukumiwa kifungo cha miaka 12 na maudhui hayo yaliondolewa mtandaoni.


Uzoefu unaonyesha kuwa ripoti moja tu inaweza kusaidia kuondoa picha moja, au hata picha 1,000 zinazokiuka sheria. Wakati mwingine, taarifa ya picha moja tu inatusaidia kutambua na kumuokoa mtoto anaefanyiwa ukatili wa kingono. Kila taarifa ni muhimu sana na huweza kumsaidia mtoto aliepo Tanzania ama hata nchi nyingine yoyote duniani.


IWF inayo rodha ya picha zenye makatazo ili kuondoa na kuzuia picha zenye maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto mtandaoni popote pale duniani. Ikiwa picha iliyokwisha wekewa katazo itapakiwa sehemu yoyote ile duniani, taarifa huwafikia IWF haraka na kuwawezesha kuiondoa kwa mara nyingine kabla haijasambaa sana.


Mpango huu wa kimataifa utakuwa na matokeo chanya katika ukuaji na matumizi ya mtandao nchini Tanzania na utatusaidia kulinda watoto.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

2 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page