top of page

Namna ya kukuza mtoto msomaji

C-Sema Team

Kama wazazi, tunapenda kuona watoto wetu wakijifunza mambo mapya. Si ajabu kumuona mama akimuuliza mtoto maswali huku akijua mtoto atatoa jibu la kufurahisha au baba akihadithia kwa fahari jinsi mtoto wake alivyo mdadisi.


Watoto wana akili sana; hugundua mambo mapya kila siku, huuliza maswali na kujaribu kusaidia shughuli za nyumbani. Tunawezaje kuwasaidia watoto wetu ili uelewa na uwezo wao wa kudadisi uweze kuongezeka? Kusoma ni mojawapo ya njia bora katika kufanikisha suala hili.


Tulifanya utafiti mdogo kwa kuzungumza na baadhi ya wazazi ili kujua mbinu wanazotumia kuwahamasisha watoto wao wafurahie na kupenda kusoma; zifuatazo ni baadhi ya mbinu walizotupatia:-


Panga kusoma na mtoto wako iwe ratiba ya kila siku. Endapo mtasoma pamoja, mtoto wako ataona kuwa kusoma kuna umuhimu na ataungojea muda huu kwa hamu hata kama umepanga kusoma kwa nusu saa tu. Mnapotaka kusoma, shirikiana na mtoto wako kuchagua vitabu. Maamuzi kama haya ni muhimu kwa mtoto wako na yatamuongezea shauku ya kusoma na kujifunza.


Msomee mtoto kwa sauti huku ukimwonesha unapopasoma. Unaweza pia ukapokezana kusoma na mwanao. Hii itamsaidia kujifunza maneno mapya kirahisi na kuyakumbuka.

Ipe simulizi mvuto unapokua unasoma. Unaweza kumuahidi mtoto kuwa mtaendelea siku inayofuata, hasa kama hadithi ni ndefu. Mtoto atakuwa na shauku ya kujua kitakachofuata.


Pia unaweza kumpa mtoto nafasi ya kukwambia ni jinsi gani yeye angehitimisha hadithi mnayosoma.


Yape uhai maneno unayosoma. Wape wahusika sauti mbalimbali za kuendana nao. Simba anaweza kuwa na sauti kubwa ya kunguruma na panya akawa na sauti ndogo. Jaribu kubadili sauti kutokana na hisia za wahusika kama hasira, furaha ama huzuni. Mpe mwanao nafasi ya kuiga sauti za wahusika pia. Hii itamsaidia mtoto kutunza kumbukumbu ya mlichokisoma.


Muoneshe mtoto picha mkiwa mnasoma. Hii itamsaidia kuelewa maneno mapya na magumu. Mnaweza kuangalia picha kabla ya kusoma hadithi na kukisia inahusu nini. Hii huleta tofauti katika simulizi na huweza kuchochea ubunifu wa mtoto.


Jadiliana na mwanao kuhusu hadithi baada ya kusoma. Muulize mtoto Amependa nini? Hajafurahishwa na nini? Amejifunza kitu gani? Jaribu kumuonesha uwiano uliopo kati ya hadithi na maisha ya kila siku. Ni vyema mtoto wako ajibu maswali haya kabla ya kumpa maoni yako lakini hakikisha unachangia mawazo yako pia.


Filamu na simulizi za redioni ni namna nyingine za kuleta tofauti katika kusimulia hadithi. Watoto hutofautiana na sio kila mtoto anapenda kusoma sana kwa hiyo kuangalia/kusikiliza simulizi wanazopenda huenda kukawapa hamasa ya kusoma hadithi hizo.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

2 views
bottom of page