top of page
  • C-Sema Team

Namna wazazi tunavyoishi na athari zake katika maadili ya watoto

Mwenendo wa maisha ya wazazi hujumuisha maneno, matendo, tabia na desturi za wazazi wanazotumia katika kuendesha maisha yao ya kila siku katika familia zao na jamii inayowazunguka kwa ujumla. Mahusiano kati ya wazazi, mahusiano na majirani, ndugu, jamaa na marafiki na jinsi unavyowakarimu wageni, nk. Vyote hivi huathiri makuzi na tabia za watoto katika nyanja kuu mbili tofauti; athari chanya na athari hasi. Sote tunajua watoto kwa kiasi kikubwa hujifunza kutoka kwa wazazi wao. Wanachokiona anafanya mzazi, wao pia hufanya.


Maadili ya watoto

Tafiti mbalimbali za saikolojia ya makuzi ya mtoto zinamtaka mazazi kuwa kiongozi wa familia (role model). Awe mfano wa kuigwa na watoto, ajiheshimu hasa awapo mbele za watoto kwa kutenda matendo mema yanayofaa kuigwa na watoto na yanayoipendeza jamii inayomzunguka. Achague maneno ya kusema mbele za watoto wake hasa awapo na hasira. Watoto hawazaliwi na msamiati wa matusi na kusema hovyo, wanapata toka katika jamii zinazowazunguka. Maisha ya kila siku, vitendo vidogo vidogo na misemo huunda taswira vichwani mwa watoto juu ya maisha, lugha na mahusiano.


'Maneno yako ndio matendo yako, matendo yako ndio tabia yako, tabia yako ndio desturi yako na desturi yako ndiyo maisha yako'. Hii ni nukuu ya Mwanafalsafa na baba wa Taifa la India Mahatma Gandhi. Kutokana na maneno ya mwanafalsafa huyu, basi tabia, desturi na matendo ni picha halisi ya mwenendo wa maisha ya mwanadamu yanavyoonekana mbele za macho ya watu wengine na hii hutokana na malezi aliyoyapata akiwa mtoto mdogo.


Ubongo wa mwanadamu umeumbwa kupokea na kutunza katika kumbukumbu yale yote uliyoyapokea. Wataalamu wa makuzi wanasema mtoto mdogo anao uwezo mkubwa sana wa kupokea taarifa na kutunza na kukumbuka alichokihifadhi kwa urahisi kuliko hata mtu mzima na hii ni kwa sababu mtoto hufikiria wakati mmoja tu, uliopo; tofauti na mtu mzima ambaye hufikiria nyakati tatu: uliopita; uliopo; na ujao. Haya anayoyatunza akilini hutumika kumsaidia kuchanganua changamoto mbalimbali katika maisha.


Tofauti na inavyoonekana kuzoeleka, malezi ya mtoto hayaishii katika kumpatia mahitaji muhimu tu: kama chakula, malazi, makazi, mavazi, elimu na afya; lakini hujumuisha kumjengea misingi ya maisha itakayomfaa sasa na baadae, awe amesoma ama hakusoma mzazi anayo nafasi kubwa mno ya kutekeleza jukumu hili muhimu katika malezi ya mtoto. Kuzaa si kazi, kazi kulea - walilijua mapema mababu zetu. Urithi adimu anaoupata mtoto toka kwa mzazi ni jinsi ya kuishi na walimwengu. Hivyo mzazi analo jukumu zito la kutekeleza hili.


Tuanze kuishi kama wazazi kwani kuna upepo wa kujisahau, ukaendelea kupiga soga-zembe na rafiki zako huku mkitumia maneno makali yasiyofaa masikioni mwa watoto ikiwemo vijembe mbele za watoto, kwa njia hii unaharibu mustakabali mzima wa makuzi na madili yao. Itagharimu muda mwingi kuwarekebisha kinidhamu watoto walio lelewa katika mazingira haya. Watoto hawa hawakosi majibu hovyo kwa watu wazima na huwa na matatizo ya nidhamu wakiwa shuleni. Mahusiano yao na waalimu huwa si mazuri na mara nyingi hawapati msaada wa karibu toka kwa waalimu na mwishowe hushindwa kuendelea vizuri kimasomo.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

0 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page