Wazazi wengi hupata fahari mtoto akitimiza umri wa miaka mitatu - baada ya shughuli nzito za kumuangalia akijifunza kukaa, kutambaa na sasa anamudu kutembea hata kuruka kama 'mtu mzima! Anaonekana mjuzi wa mambo mengi si katika kutembea tu hata kuongea, kufanya maamuzi na ni rahisi kwa mzazi / mlezi kujisahau na kuanguka katika mtego wa kutarajia mengi zaidi kutoka kwake akidhani tayari huyu ni mtu mzima. Lahasha!

Ukuaji ni hatua za taratibu. Ingawa watoto umri huu wanaonekana wana uwezo wa kufanya mengi, ukomavu wao kimahusiano na kihisia huchukua muda kuendelezwa - na hii ina maana uvumilivu kwa upande wa mzazi / mlezi. Bado uelewa wake katika mambo u-mdogo mno, hivyo makala haya yatajaribu kukupa baadhi ya mbinu za kitaalamu kukusaidia kumjenga.
Mosi ni kujenga msamiati. Watoto umri huu hujifunza msamiati (neno) mpya kila wiki na wataalamu wa makuzi wanakubaliana kwamba kadiri unavyoongea na mtoto ndivyo unavyomjengea kasi ya kunasa maneno mapya. Tumia fursa hii kuzungumza na mtoto huku ukiendelea na kazi zako za siku tumia maneno tofauti tofauti. Namna hii utamwelezea unachokifanya, mfano, 'nakoroga uji' hapa atajua kumbe uji 'hukorogwa' na si 'kukaangwa', nk. Angalizo, ingawa runinga nayo inaweza kusaidia kujifunza msamiati, kwa mtoto umri huu haisaidii sana kwani matamshi husemwa haraka na mengi mno kiasi ambacho mtoto hupitwa. Vilevile mtoto umri huu atafaidika zaidi na majibizano ya moja kwa moja runinga haina hili.
Sifia bidii. Tofauti na imani iliyojengeka kuwa ukimsifia-sifia mtoto atafanikiwa, tafiti zinaonesha kuwa badala yake ukisifia bidii anayoiweka katika kufanikisha jambo itamsaidia zaidi kujengeka kujiamini. Lengo hapa ni kumuondolea mtoto mawazo mgando na potofu kuwa yeye anaweza. Badala yake unampa mawazo halisi kwamba anaweza kufanikisha jambo iwapo atatia nia na bidii kulifanya. Wataalamu wa malezi wanasema uzoefu unaonesha watoto wenye kujengwa katika misingi ya kusifiwa pindi wanapotia bidii hupata mafanikio baadaye masomoni hata maishani. Badala ya kuvunjika mioyo wanapoanguka na kufeli, wao huiona kama mojawapo ya changamoto na kuitafutia ufumbuzi.
Tumia vidole chako kuonesha jambo kwa ishara. Tafiti zinaonesha kwamba watoto hujifunza haraka zaidi kupitia ishara za vidole, mfano ukiwa unaonesha, 'ona mbuzi anakula majani' huku kidole chako kikielekeza aliko mbuzi huyo. Katika umri huu mtoto wako atafurahia sana 'mchezo' huu na mara kwa mara atakuonesha ama ni magari au nyumba kwa ishara ya kidole. Tumia 'kamchezo' haka kumjengea uwezo wa kujua mambo kama taa za barabarani, shamba la mahindi, rangi za vitu mbalimbali, nk. Tumia fursa hii pia kuonesha na kuelezea mwonekano wa vitu mnavyoviona. Mfano, 'nyumaba ina madirisha, milango, nk.'
Tunatumai umejifunza mambo kadhaa toka katika makala haya. Lengo hapa ni kumuandaa mtoto kupambana katika ulimwengu shindani. Malezi ni shughuli adhimu sana alokupa Mungu na kamwe usikome kujifunza. Ingawa mtoto pia hujifunza toka kwa majirani, ndugu na marafiki, sehemu kubwa ya elimu dunia katika maisha ya mwazo wa ubinadamu, mtoto hupata toka kwa mama na baba au mlezi wake. Tumia fursa hii kumjengea msamiati lugha ya staha na soni. Hapana shaka kwetu kwamba ukikutana na mtoto mdogo mwenye kutukana katika kila sentensi anayotamka, ni matokeo ya malezi aloyapota. Tuamke.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org