top of page
  • C-Sema Team

Mwongozo wa kujenga mahusiano bora baina ya watoto wa tumbo moja

Mara nyingi tunapowaza juu ya kupata mtoto mwingine huwa picha zinazokuja vichwani mwetu ni kuwa sasa mwanangu/wanangu wanakwenda kupata mdogo wao. Watapata mwenzi wa kucheza wote. Watakuwa marafiki na ndugu wa kutegemeana. Ukweli ni kwamba watoto waliozaliwa tumbo moja, hasa wakafuatana, ni changamoto kubwa katika malezi kwani mara nyingi huwa na vijiungomvi visivyokwisha huku wanachogombea mara nyingi huwa hakionekani.Wataalamu wa makuzi wanakubaliana kwamba watoto wenyewe wakipewa nafasi pasi bugudha zetu wazazi wanaweza kujenga heshima, upendo, kuaminiana na kutegemeana kindugu. Mfano unapomwona mtoto mkubwa anamsukuma/kumkanyaga mdogo wake usiwe mwepesi kukemea. Mpe fursa ya kujifunza kumjali mdogo wake ambaye mara nyingi atapaza sauti kutaka ujue kakanyagwa/kasukumwa. Namna hii kaka/dada mtu atalazimika kumbembeleza mdogo wake na muda mchache baadaye watacheka pamoja. Hapa wanajenga mahusiano.


Mfano mwingine ni mara tu unapokuwa umempata mdogo mtu, watoto wengi hujenga 'chuki' kwani ghafla mapenzi ya wazazi huamishiwa kwa mdogo wake. Namna nzuri ni kumshirikisha toka ujauzito kwa kumueleza kwamba nyote mnatarajia kupata ujio wa mdogo wake. Mara tu anapozaliwa mfanye sehemu ya malezi kwa kumpa majukumu madogo madogo huku ukitumia kauli jumuishi, mtoto wetu analia, atakuwa anataka kunyonya, unapaswa kuwa mlinzi wa mtoto wetu, nk. Ajisikie sehemu ya familia na kwamba kumbe huyu ni wa kwenu.


Fursa nyingine ni wanapokuwa wametimiza umri wa kwenda shule mara nyingi mkubwa huanza kujua kusoma na mdogo wake huanza baadaye. Mpe fursa ya kaka/dada mtu kuwa mwalimu wa mwenzie kwa kumfundisha namna ya kushika kalamu, kumsomea hadithi na hata kuimba nyimbo za kiada pamoja. Namna hii unawafundisha kutegemeana na kuimarisha mahusiano ya kindugu.


Vilevile unaweza kuwajengea mazingira ya kushirikiana katika kazi kwa kuwapangia kufanya usafi, kufua, kuosha vyombo, nk. kwa kushirikiana. Namna hii watajifunza kutekeleza majukumu kwa pamoja kama familia. Ingawa viji-mambo vitakuwepo kama vile utegaji wakati wengine wanafanya kazi, zoezi hili pia litakupa fursa ya kuzipata ripoti za namna kazi ilivyotekelezwa na kutoa funzo juu ya utegaji kazini.


Watoto wakikua kwa kutegemeana hata changamoto baina yao na marafiki zao zitatatuliwa mara nyingi bila hata wewe kushirikishwa. Muda mwingine kama wamejengeka vizuri kidugu hata changamoto za mahusiano yao na waalimu zinaweza kutatuliwa kwa kushirikiana namna hii unaandaa binadamu makini wenye uwezo mkubwa wa kutatua matatizo yao wenyewe na kwa kushirikiana.


Tutakosea tukikuaminisha kwamba baada ya kufanya mambo haya basi watoto watapendana. Zoezi la kujenga familia kupitia malezi ni endelevu. Kila uchao bado utakutana na changamoto za kupigana, kufinyana na mambo kama haya. Tunachojifunza hapa ni kwamba kumbe hata watoto wenyewe wakipewa fursa ya kuhusiana bila ya kila wakati sisi kuwa mahakimu, wanaweza kujenga mahusiano mazuri tu. Tena kwamba fursa namna hii inakupa hata wewe mzazi nafasi ya kupumua toka katika kiti chako cha maamuzi ya vijiugomvi vya watoto.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org

3 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page