Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo ni usemi ambao mara nyingi hutukumbusha wazazi umuhimu wa kulea watoto wetu katika maadili mema na yenye kuleta mafanikio. Ikumbukwe kwamba sisi wazazi ndiyo wenye jukumu la kwanza la kulea watoto huku walezi wengine kama walimu na jamii, wakichukua nafasi ya pili, n.k.
Misingi imara ya maisha ya binadamu huanza kujengwa pale tu mtoto anapozaliwa. Hii inamaanisha kuwa iwapo mzazi utamlea mtoto wako vizuri katika umri mdogo basi tambua kuwa mwanao atakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa. Iwe masomoni na hata maishani. Ifahamike vilevile kuwa katika umri mdogo namna hii ndipo ambapo wazazi tuna mtihani mkubwa kwani ndicho kipindi ambacho tunaweza kuwaharibu watoto wetu. Wakapoteza fura azote maishani.
Inawezekana kabisa kumfundisha mtoto wako juu ya mambo kama upendo, utu, kutunza muda / kutunza fedha, n.k. Mengi ya mambo haya mtoto hujifunza kwa kuona na kutenda. Ukiwa muungwanna katika kuwajibu wakubwa na hata wadogo, naye atapata uungwana huo kwako. Ukiwa mkorofi naye atapata toka kwako ukorofi. Inaanza na wewe mzazi.
Ishi kile unachotaka mtoto wako awe. Hii ni njia rahisi katika kujenga msingi imara wa maadili mema kwa mwanao tokea akiwa bado mdogo. Kama unahitaji mwanao awe na maadili mema lakini wewe unakosa maadili hayo itakua vigumu sana kwa mtoto kufuata kile unachomfundisha. Mfano, kama kila wakati unamfundisha mtoto wako kuwa mwaminifu lakini pale inapotokea mgeni anagonga mlango halafu unamwambia mtoto mwambie anayegonga kuwa Baba au Mama katoka, hii itamfanya mtoto ajenge picha ya kuwa muongo dhidi yako mzazi na kwa jamii inayomzunguuka.
Mfunde kukubali na kutekeleza majukumu angali mdogo. Tabia hii anatakiwa afundishwe mtoto pindi angali mdogo hasa kupitia kazi za kila siku za nyumbani kuanzia usafi wa nyumba na mazingira yake pamoja na maandalizi ya chakula. Kila mtoto ndani ya familia anatakiwa kufahamu majukumu yake ni yapi kila iitwapo leo na pale atakaposhindwa kutekeleza ni muhimu akumbushwe. Tusiwalee watoto katika mazingira yatakayowafanya wakwepe majukumu muhimu ya maisha yao kwani mwishowe watakua ni watu wa kusubiri misaada kwa ajili ya kufikia hatua wanazokusudia, watu tegemezi na walalamikaji.
Mapema mtoto ajue kuwa kuna wakati mambo huwa hayaendi kama yalivyopangwa. Katika kumfundisha hili, subiri kipindi ambacho mtoto anataka kitu fulani na pengine kitu hicho huwa unampatia kila anapokihitaji, kwa makusudi kabisa mnyime. Kama tujuavyo tabia za baadhi watoto ni dhihiri kuwa anaweza kulia na mara zingine hata kugaragara chini muache tu. Zikipita siku kadhaa mnunulie kitu hicho halafu mpe somo atambue kuwa kuna wakati mambo hayaendi moja kwa moja kama sisi binadamu tunavyopanga. Fanya hivi kwa mtoto ambaye ameshaanza kujitambua, rudia mara nyingi kadri iwezekanavyo mpaka ifike mahala mtoto ajue kwamba mategemeo na uhalisia ni vitu viwili tofauti.
Kila mtoto ndani yake kuna upendo, tumaini, akili, utu, uaminifu na sifa kadha wa kadha. Jukumu letu kubwa kama wazazi ni kuwatazama watoto wetu kwa jicho la ndani ili tufanikiwe kuzitambua sifa hizi na hatimaye tuwaongoze mtoto katika kuziendeleza kwenye kila hatua ya maisha yao. Onyesha njia nae ataifuata! Â Malezi ya watoto kwa Bahati mbaya hayafundishwi darasani bali kwa mazoefu na mazingira sie wazazi nasi tulimokulia. Tuendelee kuelimishana ili hatimaye tukuze wazazi makini wa vizazi vijavyo. Ama kwa hakika, ukipanda mabua lazima utavuna mabua.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
Comments