Jumapili ya leo tunasherehekea maisha na mafanikio makubwa aliyotukarimu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Mwalimu ambaye kimsingi alianza harakati za ukombozi wa taifa letu toka akiwa mwanafunzi, mwalimu na hata kiongozi wa chama cha TANU, alikuwa na sifa nyingine lukuki nje ya siasa. Mwalimu alikuwa baba makini wa familia yake. Alikuwa baba makini wa taifa hili.
Alianzisha taasisi ya chakula na lishe. Mapema kabisa wakati dunia ikiwa bado haijui mchango wa lishe bora kwa watoto na hapa Afrika Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kabisa kuanzisha kituo maalumu cha kutafiti na kuishauri serikali juu ya lishe ya watoto na watu wake kwa ujumla (Tanzania Food and Nutrition Centre). Mpaka leo Tanzania inaheshimika duniani kote kwa kuwa na wataalamu wabobezi katika lishe. Mataifa mengi duniani kote huja hapa nyumbani kujifunza namna kituo chetu cha chakula na lishe kinavyochagiza mipango makini ya afya ya ulaji serikalini na kwa wananchi.
Aliaelewa umuhimu wa kilimo kama uti wa mgogo wa makuzi ya taifa la kesho. Mwalimu mapema kabisa alianzisha vituo vya kutafiti kilimo kulingana na hali ya hewa ya maeneo karibu yote nchini. Vituo hivi ingawa havipewi tena vipaumbele lakini mchango wake ulipaswa kuwa mkubwa katika kuhakikisha tunacho chakula kwa ajili ya mahitaji ya ndani na hata kusafirisha nje ya nchi kwa biashara. Kagera walitafiti miwa, ndizi (migomba), mahindi, nk. Wakati Pwani wao walijikita katika utafiti wa kilimo cha maembe, korosho, nk. Vituo hivi pia viliandaa vijana wataalamu wa ushauri wa kilimo kwa wananchi wa eneo husika. Mwalimu alijali watoto wake, ama kweli alikuwa mzazi makini.
Mwalimu alizingatia usawa kwa watoto wote. Mara tu baada ya kujikomboa toka kwa Uingereza mwalimu aliyamaliza matabaka hasa katika elimu. Shule za wenye nacho za wakati ule zilifanywa kuwasajili watoto wa makabwela na wa wakulima toka kote nchini. Mwalimu alitoa fursa kwa watoto toka vijijini kabisa kuja kusoma jijini Dar es salaam, Arusha, Mwanza na miji mingine. Hii ilisaidia kumaliza ubaguzi wa kipato. Baba makini huwapenda watoto wake pasi na ubaguzi, huyu ndiye Mwalimu Nyerere.
Hakutaka watoto waende jela kutumikia kifungo mara wanapokinzana na sheria. Labda tufafanue maana ya kukinzana na sheria kwanza. Hii hutukea pale ambapo mtoto atatenda kosa kama vile kuiba, kuua, n.k. Sheria ni msumeno na hivyo mara kadhaa haijali sana umri wa mtenda kosa na hivyo inawezekana kabisa mtoto kuhukumiwa kutumikia kifungo jela. Mwalimu kwa kuliona hili na kwa kushauriana na wataalamu wa sheria wa wakati huo, aliona vyema kuwepo na shule maalumu (approved schools) ambazo watoto hawa walipelekwa badala ya kwenda jela. Hapa walipata wasaa wa kurekebishwa tabia huku wakipata elimu ya darasani.
Mwalimu alidhamiria watoto wote kuchangamana kwa lugha moja, Kiswahili. Hakuna taifa Afrika ambalo linayo makabila mengi kama hapa kwetu Tanzania, takribani makabila 158 na bado likazungumza lugha moja. Mchango huu wa mwalimu katika kukikuza na kukitapanya Kiswahili kote nchini ulilenga kuunganisha vizazi vya wakati ule, vizazi vya sasa na vizazi vijavyo katika taifa moja. Leo hii tunazo taasisi makini za vyuo vikuu na hata katika serikali zilizojikita kuboresha lugha hii adhimu iliyofanywa ya taifa kwa juhudi binafsi za Mwalimu Nyerere.
Mwalimu hakupenda umangi-meza. Mwalimu alichukia ubwanyenye na ukuu-ukuu na hivyo aliishi maisha ya kawaida na kujichanganya na wazee, vijana na hata watoto. Hii ilimtofautisha sana na maraisi wengi wa Afrika wa wakati wake ambao wengi walirithi serikali za kikoloni na makucha yake. Tuendeleze jitihada za mwalimu katika malezi kwa vitendo.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania