top of page
  • C-Sema Team

Mtambulishe mtoto kwa wazazi na ndugu wa familia tandaa


Tamaduni zetu za kiafrika zinaasa malezi ya watoto kufanywa na wazazi wote wawili, mama na baba. Majira sasa yameanza kubadilika na leo si jambo la kushangaza kuona watoto wakilelewa na mzazi mmoja mara nyingi akina mama huku wakigombana na wenzi wao juu ya umiliki wa watoto kila mmoja akitaka kuchukua jukumu la kulea kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutengana kwa wazazi, ujauzito ulokuja bila mipango ama utayari wa kulea, n.k.


Watoto wengi sasa wanakuzwa bila kujua wazazi na ndugu zao wa familia tandaa kwa sababu nyingi ikiwemo kutelekeza ujauzito, kutelekeza watoto na baadhi ya wazazi hasa wa kiume na kukimbia majukumu yao ya kuwahudumia watoto au familia kwa ujumla kama wazazi. Wazazi wamekuwa wakiwaficha watoto chimbuko lao bila kujua wanatenda kosa la jinai. Ingawa hili linawakuta wazazi wote wa kike na wakiume, kwa kiasi kikubwa wazazi wa kike wanaongoza kwa vtendo hivi labda kwa sababu wao ndio huachwa na ujauzito na mara kadhaa hutelekezewa watoto au mimba na wazazi wenzao wa kiume. Sheria ya Mtoto, 2009 inamtaka mlezi kumfahamisha mtoto wazazi wake wa kumzaa na ndugu zake wengine.


Wazazi vilevile katika kuhakikisha mtoto kamwe hapatwi na ndugu zake huwabadilisha majina ya baba zao na kuwaita ya wajomba zao au ya babu zao wa upande wa mama (maternal grandfather) na pengine huwaambia watoto kuwa baba zao walishakufa ingawa wanajua wako hai. Kwa mtazamo wa kawaida unaweza kuwalaumu sana wazazi wa namna hii kwa vitendo hivi, lakini ukifuatilia mlolongo wa matukio yaliyowapelekea wao kufanya hivi ikiwemo maumivu ya kutelekezwa na ujauzito, unaweza ukawaelewa kwa kiasi fulani, lakini hii haiwapi haki ya kumnyima mtoto kuujua ukweli wa wapi chimbuko lake.


Wazazi hawa hufanya hivyo kama kulipiza kisasi na kufikiri kwamba mzazi mwenzake wa kiume hana haki ya kuwa mzazi wa mtoto huyo kwa sababu alimkana na kumkataa toka akiwa tumboni au hakutaka kushiriki kumlea mtoto huyo tangu amezaliwa. Wengi wa wazazi hawa huathirika kisaikolojia na kuamua kuchukua uamuzi huo wakidhani ni suluhisho la tatizo lililopo kati yao kama wazazi. Kifungu cha sita cha Sheria ya Mtoto 2009, hakimruhusu mzazi yeyote kumnyima mtoto haki ya kujua chimbuko lake, Mtoto atakuwa na haki ya jina, utaifa na kuwafahamu wazazi wake wa kumzaa na ndugu wengine wa familia tandaa.


Vitendo hivi vinaonekana vya kawaida katika jamii bila kujua ni kwa kiasi gani humuathiri mtoto katika makuzi na maendeleo yake hasa kisaikolojia. Mtokeo ya athari ambazo hutokana na suala hili hubainika baadaye mtoto anapokuwa mkubwa kuanzia umri wa elimu ya msingi na kuendelea, hapo ndipo mtoto huanza kuhoji kuhusu chimbuko lake kwa kumuuliza mama kuwa baba yuko wapi au kumuuliza baba kuwa mama yuko wapi au pengine ndugu wanaomzuguka. Wakati mwingine wazazi huingia katika ugomvi mkubwa na watoto wao kiasi cha kujibizana kwa ukali kwa sababu tu mtoto anataka kujua chimbuko lake.


Wakati akiwa mdogo ni vigumu kugundua ni kwa kiasi gani mtoto anateseka kwa kutokujua wazazi ama mzazi wake. Hii ni kwa sababu wazazi ukiacha kuwaficha watoto juu ya chimbuko lao, pia huwaeleza kuhusu ugomvi uliopo au uliowahi kutokea baina ya wazazi. Kumhusisha mtoto katika ugomvi wa wazazi si jambo zuri kwani mtoto hahusiki kwa namna yeyote ile katika ugomvi wenu hasa unaohusu maamuzi na mipango ya kumleta duniani. Ni vyema kama mzazi mwenzako alikukosea kwa namna yeyote ile muwekee kinyongo yeye na si kupanda chuki kwenye akili ya mtoto juu ya baba au mama yake. Wahenga husema funika kombe mwana haramu apite, kwa hiyo kama mzazi jitahidi kumueleza mazuri juu ya mzazi wake hata kama alikukosea, makosa na maovu ya mzazi mwenzako jitahidi kuyaweka kifuani ili kumsaidia mtoto kukua bila kuwa na chuki juu ya mzazi wake. Ukipandikiza chuki hiyo kwa mtoto huweza kumuathiri mtoto na kumjenga kuwa mkatili juu ya watu wengine.


Watoto ambao wamefichwa ubini wao hupata wakati mgumu sana wakiwa katika mazingira ya shule, mara nyingine wanataniwa sana na watoto wenzao hasa pale minongono kuhusu chimbuko la huyu mtoto inapofika shuleni. Hali hii humuathiri sana mtoto kisaikolojia na kumpelekea kufanya vibaya kwenye masomo yake na wakati mwingine kuacha shule kabisa kwa kuogopa kutaniwa. Mtoto wa namna hii huwa na msongo wa mawazo anaposikia wenzake wakiongelea kuhusu baba, mama, mjomba na shangazi wakati yeye hajawahi kusikia watu wa namna hiyo katika maisha yake kwa sababu ya kufichwa chimbuko lake. Suala hili ni la kuzingatia sana ili kuwaepusha watoto na matatizo ambayo yanaweza kuwaathri hadi ukubwani kwa sababu saikolojia zao zinakuwa zimeharibiwa. Mwambie mtoto ukweli kuhusu chimbuko lake pamoja na kuwapa fursa ya kusalimiana na kutembeleana na wazazi wao walio mbali nao kama wazazi wametengana.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

1 view

Recent Posts

See All

コメント


bottom of page