Mara nyingi huwa tunasisitiza umuhimu wa kumsikiliza mtoto.
Kwanini tunasisitiza sana suala hili? Simu nyingi tunazopokea katika Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto kupitia namba 116, zinazohusu ukatili wa kingono huusisha mzazi / mlezi aliepuuza pale mtoto alipojaribu kueleza anachotendewa. Ukimuuliza mtoto, 'Je, ulimuambia mtu yeyote?' Mara nyingi jibu linakua, 'Nilimwambia mama / baba akaniambia, 'Unanisumbua. Toka hapa!' Wazazi hupuuza mashitaka ya watoto hadi wanapogundua watoto wamepata madhara na kujeruhiwa kwa sababu ya ukatili huu.
Watu wengi wamejijengea dhana kuwa watoto ni wasumbufu na wana maswali mengi na stori zisizo na maana. Ni kweli watoto wana maswali mengi kwa kuwa bado wanakua na wanagundua mambo mapya kila siku. Ni kweli pia kuwa kuna baadhi ya stori wanazohadithia watoto ambazo ni za kufikirika. Lakini hii haikunyimi nafasi wewe mzazi kumsikiliza mwanao hata kama ni makelele maana watoto, hasa wadogo, bado hawajajua kujieleza vizuri. Mara kwa mara, watoto hutueleza mambo ya maana yanayohitaji umakini au utatuzi wetu kama wazazi / walezi.
Kulea mtoto hasa katika dunia ya sasa kuna changamoto nyingi na watoto wetu wanakabiliwa na mazingira hatarishi kila siku. Mzazi/mlezi unaposhindwa kumsikiliza mtoto na kumjengea dhana kuwa yeye siku zote anakusumbua, mtoto anashindwa kukushirikisha hata pale anapokuwa na shida au anapohitaji utatuzi na ushauri wako wa haraka. Usipomsikiliza wewe, nani wa kumsikiliza?
Wewe kama mtu mzima unapomsemesha mtu mzima mwenzako na haonyeshi kukujali wala kutilia maanani yale unayomwambia unajisikia vibaya na pengine utaacha kumueleza kile ulichokusudia. Vivyo hivyo, watoto hujisikia vibaya pale wazazi wasipowasikiliza mara kwa mara na baada ya muda wanaacha kuwashirikisha wazazi hata pale wanapofanyiwa mambo mabaya na kujikuta katika mazingira hatarishi.
Ukimsikiliza mtoto unampa kujua kuwa yeye ni wa thamani kwako na unamjali na kujali mawazo yake. Wataalamu wanaeleza kuwa mzazi akimsikiliza mtoto hujenga mahusiano ya karibu sana na kumfanya mtoto awe muwazi akiwa mdogo na hata akiwa mtu mzima. Utakuwa na rafiki wa karibu wa kumwamini ambaye ni mwanao hata akiwa mtu mzima. Jenga kumsikiliza hata ikiwa ni makelele. Jali mawazo yake na umjibu sio tu kwa kumfurahisha ila kwa kumaanisha.
Kama siku zote una majukumu mengi, jitahidi kupanga muda wa kuongea na mtoto uwe ni muda wa kuongea nae tu na sio jambo lingine. Msikilize kwa makini pale anapokuwa anaongea na utumie lugha rahisi kumuelewesha kwa ufasaha pale anapozungumza jambo ambalo haliko sahihi. Wataalamu wa makuzi ya watoto hueleza kuwa watoto wanaosikilizwa hujengeka na kuwa watu wazima wanaoheshimu mawazo ya wengine na kutoa mawazo yao kwa kujiamini na kujithamini.
Endapo utajenga tabia ya kumsikiliza mtoto, utamuepusha na mengi katika jamii na kuepuka yale majuto ya 'Ningejua'. Wazazi / walezi wengi hushtuka baada ya mtoto kukatiliwa sana kiasi cha kuumizwa vibaya na ndipo neno, 'Ningejua' huja. Waswahili husema, 'Majuto ni mjukuu' ila kwa nini ujute wakati unaweza kumuepusha mtoto wako na mabaya mengi kwa kumsikiliza na kumfanya awe rafiki wako wa karibu? Ukimsikiliza mtoto umemlinda pia.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.