top of page
  • C-Sema Team

Mambo manne ambavyo mama unayenyonyesha unapaswa kuyazingatia

Ripoti iliyotolewa mnamo tarehe Mosi Agosti 2017 na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha kuwa unyonyeshaji wa watoto ni jambo muhimu sana kwa kuwa unamsaidia mtoto kuepukana na magonjwa ya kuharisha na yale ya mapafu ambayo ndiyo magonjwa sugu yanayosababisha idadi kubwa ya vifo kwa watoto wachanga kote Duniani. Ripoti hiyo ilibainisha kwamba maisha halisi ya mtu mzima huathiriwa na umri wake wa utotoni, mathalani kipindi cha miaka mitano ya awali ya ukuaji wa mtoto ina nafasi kubwa kwenye maendeleo na tabia ya mtoto. Hata hivyo, ripoti inasisitiza ukweli kwamba kila kipindi katika maisha ya mtoto kina umaalum wake.



Makala ya leo yataangazia mambo manne ambavyo mama anayenyonyesha anapaswa kuyazingatia ili mwanae akue vyema.


Kumpumzisha mtoto na kumlaza. Tafiti mbalimbali katika malezi zinafafanua kuwa mtoto anayenyonya anapaswa kulala masaa 16 hadi 20 kati ya masaa 24 ya siku hasa katika miezi minne ya mwanzo. Hata hivyo, inashauriwa kwamba ni muhimu sana mama kumuepusha mtoto na kelele zisizo na tija ili kumhakikishia usingizi uliotukuka. Aidha ni mahsusi pia kuhakikisha mtoto analala mahala salama na katika mazingira ambayo hayataweza kumuathiri kwa namna yoyote ile.


Kumkumbatia mtoto. Ni dhahiri kuwa idadi kubwa ya akina mama wanaonyonyesha mara nyingi hawaoni umuhimu wowote juu ya kuwakumbatia watoto kabla ya, wakati wa au hata baada ya kunyonya ingawa ukweli ni kwamba watoto wanaonyonyeshwa wanahitaji sana joto la mama zao. Kwamba joto hilo kitaalamu linajenga ukaribu kwa mtoto na humuonyesha kuwa anajaliwa. Kupitia joto la mama, mtoto hupata utambuzi wa kujenga mahusiano mama yake kirahisi kwa maana joto huambatana na harufu ambayo kwayo ndiyo sehemu ya utambuzi wa awali katika mahusiano.


Kumvisha mtoto mavazi yanayoendana na mazingira. Si jambo jema kwa mtoto anayenyonya kuvishwa nguo nyepesi katika mazingira ya baridi ama nguo nzito kwenye mazingira ya joto. Hii huweza kumsababishia mtoto uwezekano wa kupata magonjwa hatarishi yanayoweza kuathiri afya yake kila wakati. Ni jukumu la wazazi kumvisha mtoto mavazi yanayokidhi haja ya mazingira yanayomzunguuka, hata hivyo mavazi hayapaswi kuwa ya kubana sana bali yatoe uhuru mathalan yatakayomfanya mtoto ageuke kirahisi pale anapohitaji kufanya hivyo.


Kumuweka mtoto katika hewa safi. Pamoja na changamoto nyingi za kimazingira hususan katika nchi zetu za Ulimwingu wa Tatu, ifahamike kwamba mtoto anapaswa kuvuta hewa safi pindi anyonyapo au hata wakati wa kupumzika. Ni wajibu wa wazazi kuhakikisha kuwa mahali amuwekapo mtoto ni salama na hewa avutayo ni safi, mtoto asinyonyeshwe ama kupumzishwa mahali palipo na vumbi au upepo mkali kwani kufanya hivyo huweza kumsababishia mtoto mafua na maradhi mengine mara kwa mara.


Ni vyema wote kwa pamoja tukatambua kwamba mtoto kunyonya maziwa halisi ya mama ni jambo muhimu sana kwani maziwa ya Mama yana virutubisho muhimu vyenye mkusanyiko wa viini lishe vinavyofanya kazi kubwa katika kuimarisha afya ya mtoto. Vilevile wataalamu wa malezi wanashauri kwamba watoto wachanga sharti wanyonyeshwe mara 8 hadi 12 katika kipindi cha masaa 24 ndani ya wiki mbili hadi nne za mwanzo. Pia mtoto anapaswa kunyonya katika muda usiopungua dakika 20 hadi 45 kwa mlo mmoja huku utulivu na subira kati ya mama na mtoto vikizingatiwa. Malezi ya watoto kwa ujumla wake ni kazi ya masaa 24 kwa siku miaka yake yote hadi atakapotimiza utu-uzima.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

1 view

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page