top of page
  • C-Sema Team

Malezi kwa watoto waishio na virusi vya ukimwi (VVU)

Katika Makala hii tutaangazia watoto wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa watoto walio katika umri wa kujitambua na kuweza kujihudumia na namna wazazi wanavyolichukulia suala hili katika harakati za kuwahudumia watoto wao.


Tunaposema watoto wenye umri wa kujitambua na kujihudumia tunamaanisha watoto wenye umri kuanzia miaka nane na kuendelea kwani kuanzia umri wa miaka nane hadi umri wa miaka 12, watoto huanza kuelewa, kufikiri na kuona mantiki katika jambo, aghalabu kwa uchahe tu hasa katika mambo wanayoweza kuona au vitu wavyoweza kugusa. Katika umri huu watoto huwa na uwezo mkubwa kuona mitizamo, maoni na kuzingatia hisia za wengine.


Watoto huweza kupata maabukizi ya VVU kwa njia tofauti ikiwemo kuambukizwa wakati wa kuzaliwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambayo ni njia kuu kabisa kwa watoto hasa wa umri mdogo kabisa. Wengine huambukizwa kwa kuchangia vitu vyenye ncha kali na waathirika wa VVU kama vile nyembe, vipini na sindano, kugusa damu ya mtu aliyeathirika endapo atakuwa na mchubuko sehemu ya mwili wake, kuongezewa damu ya mtu aliyeathirika au kwa kushiriki ngono bila kutumia kinga. Tukisema kushiriki ngono wengi watajiuluza mtoto wa umri mdogo inawezekana vipi akashiriki ngono? Takwimu zinaonesha kuwa watoto wanaanza kujihusisha na ngono kabla hata ya kutimiza miaka 10.


Mtoto anpofi­kisha umri wa miaka 4-6 anatakiwa aanze kupewa taarifa kidogo kidogo juu ya hali yake ya maambukizi. Anapo­fikia miaka 8-10 na anapoonekana ana uwezo wa kuelewa masuala mbalimbali ya maisha na uwezo wake wa kumudu masomo darasani umeimarika, mtoto huyo pia atakuwa na uwezo wa kuelewa masuala ya afya na jinsi kinga inavyofanya kazi mwilini hivyo anaweza kupewa taarifa kamili kuhusu hali yake ya maambukizi ya VVU


Ni jukumu la mzazi au mlezi kuhakikisha afya ya mtoto wake iko salama kwa kumpeleka katika kituo cha afya pale inapotokea mabadiliko ya kiafya na kuhakikisha mtoto anapata matibabu. Katika kutekeleza jukumu hili, wazazi wengi wamekuwa na dhana potofu ya kuwaficha watoto hali yao ya kiafya baada ya kugundua watoto wameathirika.


Kuna taratibu maalum za kuzingatia zinazo tolewa na wataalamu wa afya baada ya kugundua mtoto au mtu mzima kaathirika na virusi vya UKIMWI kama vile kuhudhuria matibabu ya dawa za kupunguza makali ya virusi, kuhudhuria kiliniki kwa ajili ya uchunguzi wa mara kwa mara, kuhudhuria semina za ushauri nasaha na kuelimishwa namna ya kujikinga na maambukizi mapya.


Namna ya Kumueleza mtoto:

Ni muhimu mzazi au mlezi kwa kushirikiana na mtoa huduma kuandaa mpango wa namna ya kumueleza mtoto hali yake ya maambukizi ya VVU, kabla ya mtoto huyo kupata habari hiyo kutoka vyanzo vingine. Kusikia habari kuhusu hali yake ya maambukizi toka kwa mtu mwingine, kunaweza kumfanya mtoto ajisikie vibaya na atingwe na msongo wa mawazo na hata kupelekea kuchukua maamuzi yasiyofaa kama vile kujiua, kuacha shule, kuacha dawa hata kutokuwa na imani na wazazi wake. Ni vizuri kuongea na kumwambia mwanao mambo yanayomuhusu na kumfariji.


Mtoto aelezwe ukweli kuhusu afya yake huku akifundishwa namna ya kujikinga na kuwakinga wenzake. Mtie moyo kukubaliana na hali halisi ya mabadiliko ya kiafya yanayoweza kujitokeza mara kwa mara na namna ya kujihudumia. Tujenge tabia ya kuamini watoto wetu kuwa wana uwezo mkubwa wakipatiwa muongozo mzuri wanaweza kufanya makubwa kujilinda na kuwalinda watoto wenzao.


Wazazi/walezi wanapaswa kuzungumza na watoto juu ya ugonjwa huu kwa njia inayolingana na umri wao ili isiwatishe. Watoto wanahitaji kujua kwamba sio kosa lao, wao ni wagonjwa na wanapaswa kumeza dawa kila siku. Mzazi amtie moyo mwanae kuwa hayuko mwenyewe katika kukabiliana na ugonjwa huu. Msaada wa kijamii, kifedha, na kimhemko/kisaikolojia kwa familia nzima ni muhimu pia.


Watoto wenye VVU na UKIMWI wanaweza kwenda shule salama. Ila wanaweza kukabiliwa na unyanyasaji na ubaguzi ikiwa wanafunzi wengine na waalimu hawana uelewa mzuri wa jinsi VVU vinavyosambazwa. Uhamasishaji na mipango ya elimu husaidia kuvunja unyanyapaa wa VVU ili watoto wawe na marafiki na kuhisi wanapendwa na wako sawa na watoto wengine.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

2 views

Recent Posts

See All

留言


bottom of page