Ni ukweli usiopingika kuwa kuenea kwa tehama (teknolojia ya habari na mawasiliano) vimeathiri jinsi tunavyolea watoto wetu. Runinga, redio, simu za mkononi, kompyuta, na intaneti; vyote vina mchango katika malezi yetu siku hizi.
Mijini, runinga ni sehemu kubwa ya maisha ya kila siku ya familia. Bila uangalizi, watoto huweza kukaa mbele ya runinga siku nzima wakikodolea macho vipindi vinavyowafurahisha na wakati mwingine hata kukataa kula wasije pitwa na kipindi chochote. Wengi wetu tumeshuhudia wanetu wakigombana hadi kununiana pale wanaposhindwa kufikia muafaka juu ya kipindi cha kuangalia kwa wakati huo.
Leo tutaangazia athari za watoto kutazama mno runinga na njia za kuwafanya wapunguze muda wanaotumia mbele ya runinga.
Tafiti mbalimbali zimebaini kuwa vipindi vya runinga husababisha madhara mbalimbali kwa watoto. Muda ambao watoto wanakaa mbele ya runinga huathiri maendeleo ya ubongo na matokeo yake ni watoto kutokuwa makini, wenye fujo, kutofaulu vizuri katika masomo, unene uliopitiliza na hata woga usio na msingi. Vilevile, watoto wanaotizama sana runinga huwa na tabia ya kutaka kitu hiki na kitu kile ikiwa ni matokeo ya matangazo wanayoona katikati ya vipindi vyao.
Dk. Jay Martin wa Chuo Kikuu cha Southern California alifanya utafiti kwa watoto 732, na kugundua kuwa kadiri watoto walivyotumia masaa mengi kuangalia runinga, ndivyo walivyozidisha migogoro na wazazi, kupigana na wenzao, na tabia za kihalifu. Kwa bahati mbaya sana, hata vipindi vinavyotakiwa kuwa vya familia au vya watoto huwa na kiasi fulani cha lugha chafu, vurugu, anasa na tamaa.
Hatusemi kila kipindi kwenye runinga ni kibaya. Kuna vipindi vinavyovutia na vinavyoweza kumuelimisha mwanao, katika nyanja za Sayansi na Maarifa kwa lugha ya Kiingereza au Kiswahili. Shirika la Kimarekani la Afya ya watoto, American Academy of Pediatrics, limependekeza kwamba watoto wenye umri wa miaka miwili au zaidi wasiangalie runinga kwa zaidi ya masaa mawili kwa siku.
Si vyema kumnyima kabisa mtoto kuangalia runinga wakati wenzake wanaruhusiwa kuangalia makwao na una runinga sebleni kwako. Ukimnyima, hutakuwa umemsaidia. Atajifunza kuibia. Badala ya kumnyima kabisa, jaribu mbinu zifuatazo ili kumsaidia mwanao kuwa makini na muda anaoutumia mbele ya runinga. Wasaidie wanao kuchagua vipindi vya kuangalia.
Epuka vita na wanao kuhusu vipindi, kwa kuwa hatua moja mbele yao. Jaribu kufahamu vipindi vya watoto, hata kutoka kwa wazazi wengine, na jitahidi kuviangalia kabla ya wanao ili kuelewa maudhui. Tafuta vipindi vinavyoburudisha lakini vyenye maadili mema na vyenye kufundisha. Ukiridhishwa na kipindi, muwahi mwanao na upendekeze mkiangalie pamoja badala tu ya kumnyima kuangalia kipindi kingine.
Tenga muda wa kuangalia runinga na wanao. Inawezekana kufanya hivi kila siku ni vigumu kutokana na majukumu kuwa mengi. Hata hivyo, kama mtoto wako bado ni mdogo na ndo kwanza ameanza kupenda runinga, kuangalia naye itamsaidia kuchagua vipindi vizuri vya kuangalia hata wakati ukiwa haupo. Vilevile, ukiangalia vipindi na watoto, utawasaidia kusisitiza mambo mengi wanayoweza kujifunza kutokana na vipindi vyao.
Usiweke runinga wala kompyuta vyumbani. Vikiwa chumbani, utapata wakati mgumu sana kufuatilia kwa ukaribu wanachokiangalia watoto. Hali kadhalika, watatumia muda mwingi zaidi kuangalia runinga na kuchezea kompyuta. Matokeo yake, wanao watakua wavivu na watakosa usingizi wa kutosha hasa kama watakua na tabia ya kukodolea macho vifaa hivi hadi usiku wa manane. Runinga na kompyuta viwekwe sebuleni na sio katika vyumba vya kulala.
Mbinu nyingine, ambayo inaweza kuwa ngumu kidogo lakini husaidia ni mfungo wa kutoangalia runinga mara moja moja. Jaribu kukubaliana na wanafamilia wote kutoangalia runinga kwa wiki nzima. Bando la king'amuzi linapoisha, ngoja wiki moja ama siku kadhaa kabla ya kukilipia. Tumia muda ambao mngekua mnaangalia runinga kama muda wa familia ili muweze kushirikiana wote katika mambo mbalimbali. Hii itajenga ukaribu baina ya wanafamilia wote huku mkipumzisha akili (na macho yenu). Ving'amuzi na runinga za siku hizi pia zinamuwezesha mzazi kuzuia baadhi ya vipindi na idhaa zisizofaa kwa watoto.
Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba kadiri watoto wanavyokuwa ndivyo wanavyopata maeneo mengine ya kuangalia vipindi ambavyo umehangaika kuvizuia nyumbani.
Watoto wanahitaji muda wa kutosha na wazazi wao, mwingiliano na watoto wenzao na muda kwa ajili ya michezo ya ubunifu; ambavyo vyote huwajengea uwezo mkubwa wa kufikiri. Hivyo, ingawa hatukushauri uondoe kabisa runinga katika maisha ya wanao, jitahidi kuwaelekeza na kupunguza muda wanaotumia kwenye runinga na unaweza ukashangazwa na mawazo chanya pamoja na ubunifu utakaoibuka.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.