top of page
  • C-Sema Team

Kwa nini tunapswa kuimarisha ulinzi wa watoto kuelekea siku kuu ya Iddi?

Msimu wa sikukuu huambatana na furaha zisizo na kifani, furaha ambazo huwapunguzia wazazi uchovu unaotokana na mihangaiko yao katika kutafuta mkate wa kila siku. Furaha ambazo huiweka sawa miili na akili za watoto hususan mara baada ya kutoka masomoni na vilevile, furaha ambazo hujumuisha utolewaji na upokeaji wa zawadi kedekede miongoni mwa wazazi na watoto ndani ama nje ya familia.


Hata hivyo pindi furaha za sikukuu zibubujikapo miongoni wa wazazi na watoto, kamwe hatupaswi kuziacha zipitilize na mwishowe zikakengeusha ukweli kuhusu maisha; zikaharibu misingi na utu ama kuacha kovu la kudumu katika maisha ya watoto. Ingawa furaha ya mzazi ni mtoto kufurahia ila tusisahau pia kuwa majuto ni mjukuu, huja kinyume.Tuwape watoto wetu ulinzi wakati wa sikukuu. Sote kwa pamoja tunakubaliana kuwa watoto wanapaswa kulindwa wakati wote ingawa wakati wa sikukuu, ulinzi sharti uimarishwe zaidi. Bahati mbaya uzoefu unaonesha kuwa watoto hutendewa matukio ya kikatili mara nyingi zaidi wakati wa siku kuu na zaidi iwapo siku kuu hizo zitaambatana na likizo zao. Yaani tafiti zinasema nyumbani si sehemu salama tena kwa watoto wetu kwani ndipo kitovu cha ukatili.

Hatushangai Jeshi la Polisi nchini kutoa angalizo, nukuu na maonyo kadhaa dhidi yetu wazazi juu ya mwenendo na mapokeo yaliyozoeleka ya kuwaacha watoto watembee peke yao, wakimbie huku na kule, kucheza pembezoni mwa fukwe za bahari, barabarani, maeneo ya wazi yaliyosheheni michezo ya watoto na kunako kumbi za starehe. Hii ni kwa sababu mida kama hii ya shamrashamra za likizo matukio ya kihalifu huzidia.

Tumepata kushuhudi ama kusikia vitendo vingi vya kikatili vinavyofanywa dhidi ya watoto na idadi kubwa miongoni mwao wakipitia unyanyasaji wa hali ya juu, ajali barabari, watoto kupotea na kurupushani kadha wa kadha zifikapo nyakati za sikukuu. Kwa mantiki hiyo, kuimarisha ulinzi dhidi yao ni jambo la msingi sana.


Aidha, wazazi wengi hususan wanaomiliki simu janja watatamani kutupia picha na video mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonesha wakiwa na watoto wao 'viwanja' tofauti vya kujivinjari. Tuwe makini kwani kusambaa kwa picha na video hizo huenda kukawa ni chanzo kimojawapo cha unyanyasaji mpya wa watoto mtandaoni endapo maudhui yake yatapata katafsirika vibaya miongoni mwa wanajamii humo mtandaoni.


Kwakuwa leo tunakumbushana masuala adhimu ya kuwalinda watoto kipindi hiki cha siku kuu, ni muhimu pia kukumbushana matukio yaliyowahi kutokea na kukatisha uhai wa idadi kubwa ya watoto katika nyakati hizi za siku kuu. Mnamo mwaka 2008 watoto 19 waliripotiwa kupoteza maisha mkoani Tabora walipokuwa ndani ya ukumbi wa Bubbles Night Club wakisherehekea siku kuu ya Iddi Mosi huku watoto wengine 60 wakidaiwa kuzimia kutokana na kukosa hewa na kukanyagana wakati wa hekaheka la kutafuta mlango wa kutokea.

Taarifa zilizotolewa zilidai kuwa ukumbi huo haukuwa maalum kwa ajili ya sherehe bali ulikuwa mahsusi kwa shughuli za mikutano. Tukio hili lilipelekea wingu zito la hofu kutanda miongoni mwa wazazi na jamii wakati ule. Hata hivyo, kwa kuwa asili ya mwanadamu ameumbiwa kusahau, huenda baadha yetu hatuna kumbukumbu tena kuhusu madhila yale ambayo kimsingi yalibeba funzo kubwa ndani yake. Kosa haliwezi kuwa kosa hadi pale litakaporudiwa, kunako siku kuu hii, hatupaswi kurudia kosa.

Hatupaswi kusubiri maafa yatokee ndipo tuone umuhimu wa kuchukua tahadhari kwani kinga ni bora kuliko tiba! Tunapaswa kutambua kuwa watoto wanahitaji uangalizi wa hali ya juu kwakuwa miili na akili zao bado havijakomaa. Tuwatakie maandalizi mema ya Sikukuu ya Iddi, yenye kheri na fanaka tele ndani yake!


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

2 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page