Miaka ya hivi karibuni kumetokea mfumuko wa vituo vingi vya kulelea watoto waishio kwenye mazingira magumu. Hii ni kutokana na mfumo mzima wa malezi ya kifamilia kuingiwa doa na pia kuongezeka kwa vifo vya wazazi, ama kwa magonjwa (mfano Ukimwi), ajali za barabarani, nk. na kuacha watoto wengi yatima.
Leo tuzungumze kuhusu malezi ya watoto wa ndugu na jamaa zetu wa karibu wanaotangulia mbele za haki au ambao wazazi wao wameshindwa kuwalea kwa namna moja ama nyingine.
Ufinyu wa vipato ni changamoto kwa wanandugu kushindwa kuchukua majukumu ya kuwalea hawa watoto na kupelekea watoto wengi kulelewa katika vituo. Hata hivyo, upo ushahidi kuwa baadhi ya ndugu huwanyayasa sana watoto wanaowalea; jambo linalowafanya watoto hawa kukimbilia mtaani au kwenye vituo hivi.

Hatukatai kuwa vituo hivi vina umuhimu wake. Kwa upande mwingine, vinasaidia sana kupunguza idadi ya watoto kuwepo mitaani na kuhifadhi wale wanaofanyiwa ukatili majumbani. Lakini tujiulize; je huu ndio mfumo wetu wa mababu zetu wa zamani wa kuwalea watoto wetu?
Zamani ndugu walikaa pamoja na kugawana majukumu ya malezi ya watoto pindi walipofiwa na wazazi. Watoto walilelewa katika mfumo mzima wa familia; walipata kuwa karibu na wapendwa wao na kukua katika maadili ya familia. Walijua wanakotoka kwa kujifunza mila na tamaduni za jamii zao. Leo hii, watoto kutoka familia mbalimbali waliokosa walezi huchanganywa kwenye vituo ambapo wanalelewa na watu baki. Kipi kimeharibu mila na desturi zetu za kiafrika za kuwalea watoto wa wapendwa wetu pale wanapotangulia mbele za haki?
Sisi kama wataalamu wa masuala ya malezi tunapenda kutoa motisha kwa jamii kuchukua majukumu ya kuwalea watoto wa ndugu pale wanapotutoka. Tuwahifadhi kwa hali na mali na sio kuwachia serikali au wadau wengine wabebe jukumu hili.
Mtoto anapolelewa katika kituo kuna madhara mengi yanayoweza kumpata kisaikilojia na kimwili. Mtoto huyu hukosa hisia za familia na familia tandaa, huwa mpweke na mara nyingine hushindwa kujua chimbuko lake. Kila mtu hujivunia chimbuko lake na hili humjengea mtoto kujiamini lakini tunapowasukuma watoto wakalelewe kwenye vituo, wanakosa kujiamini kwani hawajui cha kujivunia. Watoto hawa pia wanaweza kukutana na ukatili wa namna moja ama nyigine kutoka kwa walezi wao na hata watoto wenzao kwani kwenye vituo hivi wapo watoto wengi wenye tabia na mienendo tofauti.
Ifike mahali jamii tuamue kuwatunza watoto wa ndugu zetu na kutokuruhusu waende mitaani au kwenye vituo. Kabla haujaamua kumpeleka mtoto wa ndugu yako kwenye kituo jiulize; je, wewe ungepelekwa kwenye kituo, maisha yako yangekuwaje?
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org