Je, tunawafundisha watoto wetu kuchagua chakula bora?
- C-Sema Team
- Jul 9
- 3 min read
Updated: Jul 24
Katika dunia ya leo iliyojaa vyakula vya haraka, vingi vikiwa havina virutubisho vya kutosha, swali la msingi ni hili: Je, tunawafundisha watoto wetu kuchagua chakula bora?
Habari njema ni kwamba, si lazima tuwe madaktari au wataalamu wa lishe ili kuanza. Tunachohitaji ni kutumia mazingira ya kila siku, nyumbani, sokoni, shuleni kuwa madarasa ya maisha ya afya za watoto wetu.
Siku moja nilikwenda sokoni na mwanangu Tumaini, mwenye miaka mitano. Alivutiwa na matunda ya rangi mbalimbali. Akaniuliza, “Mama, matunda yana umuhimu gani?”
Nilimweleza: “Matunda yana vitamini na madini muhimu kama vitamini C, A, na nyuzinyuzi ambavyo husaidia mwili kukua, kuongeza kinga, na kuimarisha mwili.” Tuliondoka sokoni na mfuko wa matunda aliyoyachagua mwenyewe. Ulikuwa ushindi mdogo wa kimalezi, lakini wenye uzito mkubwa kwa afya yake ya baadaye.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), lishe bora katika utoto wa awali hupunguza hatari ya utapiamlo, unene uliopitiliza, na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari baadaye maishani.
Watoto si wasikilizaji tu, wanapenda pia kusihiriki. Tunapowaalika jikoni kufanya kazi ndogo kama kuosha nyanya, kuchambua mboga au kuandaa na kuchanganya kachumbarihuku mkipiga soga juu ya kila viritubisho vilivyomo katika kila aina ya matunda na bidhaa za chakula mlichokiandaa, wanajifunza kwa vitendo.
Utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Alberta (Canada) unaonesha kuwa watoto wanaoshiriki maandalizi ya chakula nyumbani huwa na uwezekano mkubwa wa kupendelea mboga na matunda, na huendelea na tabia hizo hata ukubwani.
Wape nafasi ya kuchagua kwa kuelekezwa. Badala ya kuwachagulia kila kitu, tuwaulize: “Leo tununue nanasi au chokoleti?” Watoto wanapopewa nafasi ya kuchagua, lakini pia wakafundishwa tofauti ya virutubisho kati ya vyakula hivyo, wanajifunza kupima, kuelewa, na kuchagua kwa makusudi. Tukiwambia, “Karoti husaidia macho yako,” tunawasaidia kuunganisha chakula na kazi ya mwili. Hii ni mbegu tunayopanda mapema kwa ajili ya kesho yenye afya.
Kwa mujibu wa taasisi ya American Academy of Pediatrics, kuwapa watoto nafasi ya kuchagua chakula chenye afya huku wakielekezwa huongeza hali yao ya kujitegemea na kuwafanya wajihusishe zaidi na ulaji mzuri.
Mtoto hujifunza zaidi kwa kuiga. Kama sisi tunakunywa soda kila siku au tunakula chipsi kila jioni, ni vigumu kumzuia mtoto kufanya vitu hivyo. Utafiti wa mwaka 2016 uliochapishwa kwenye Journal of Nutrition Education and Behavior unaonesha kuwa tabia za wazazi katika kula na kunywa huathiri sana uchaguzi wa chakula kwa watoto wao. Kwahiyo, tukianza sisi wenyewe kula mboga, kunywa maji, kuepuka sukari kupita kiasi watoto watafuata. Hatuhitaji kuwa wakamilifu, bali waaminifu katika juhudi zetu.
Kula pamoja ni fursa ya kujenga utaratibu wa kula vyakula boora kwa watoto. Meza ya chakula ni jukwaa la mazungumzo, mafunzo na mawasiliano. Tafiti kutoka Stanford Children's Health zinaonesha kuwa, familia zinazokula pamoja mara kwa mara, watoto wao huwa na ulaji bora wa mboga, matunda, na protini, na pia hupata hisia za karibu na usalama wa kihisia. Tuulizane mezani: “Leo tumekula mboga gani?” au “Unajua tofauti ya wali na dengu?” Mazungumzo ya kawaida kama haya hujenga uelewa wa kina kwa mtoto kuhusu lishe bora.
Mwisho wa siku, tunapowalea watoto wanaojua kuchagua chakula bora, tunawapa zawadi ya maisha yenye afya, akili inayofikiri kwa makini, na mwili wenye nguvu. Na jitihada hizi zinaanzia jikoni na mezani kwetu. Pia kwa kufanya hivyo, tunajenga kizazi chenye kujali afya na kupunguza hatari ya magonjwa yasiyo ambukizwa.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org