top of page

Tunawezaje kuthibiti hisia za hasira pale tunapochukizwa na matendo ya watoto wetu?

  • C-Sema Team
  • Jul 16
  • 4 min read

Juzi kati nilijikuta katika hali ambayo nadhani wazazi wengi wamewahi kupitia. Nilikuwa nimewaambia watoto wangu mara nyingi sana wasipande dirishani. Kama mzazi, unapoona dirisha halina grill na nyumba ipo ghorofa ya pili, unawaza tu jambo baya linaloweza kutokea. Nilipoona wamepanda tena, na sasa wamefungua dirisha, niliona picha kichwani ya mtoto akianguka na kuumia vibaya sana. Hofu hiyo ikazaa hasira. Bila kutafakari sana, nikanyanyua lapa na nikawachapa kwa hasira.


Baadaye, niliona watoto wakilia, na mimi bado nina hasira, na siku yetu nzuri ya Jumapili ikawa imeharibika. Niliingiwa na hisia za kujilaumu. Je, ningelituliza hasira yangu na kuchagua njia nyingine ya kuwaadhibu, mambo yangeendaje? Je, watoto wangeelewa kosa lao zaidi au walichojifunza ni kuniogopa?


Makala hii inalenga kutusaidia kujifunza namna ya kudhibiti hisia zetu kama wazazi ili tuweze kuwafundisha Watoto nidhamu kwa upendo si kwa hofu.

ree

Kwa nini tunakasirika sana? 

Tukumbuke kwamba sisi ni binadamu. Tunapochokozwa au kuona jambo la kutisha, kama mtoto kuwa hatarini, mwili wetu hujibu haraka kupitia mfumo wa neva unaoitwa "fight or flight response". Ubongo wetu, hasa sehemu inayoitwa amygdala, hupeleka ishara kwamba tuko hatarini, na mwili hujaza homon   ya hasira ijulikanayo kwa kiingereza  kama adrenaline na cortisol.


Hizi homoni hutufanya tuwe tayari kushambulia (kupiga, kufoka) au kutoroka. Hii ni biolojia ya asili ya mwanadamu. Ila tofauti yetu kama watu wazima ni uwezo wa kudhibiti mwitikio huo kwa kutumia sehemu nyingine ya ubongo inayoitwa prefrontal cortex, eneo la kufikiri, kupanga, na kutathmini.

Tatizo ni kwamba, tunapokuwa na hasira kali, sehemu hii ya kufikiri "huzimwa kidogo", na matendo yetu yanatokana na mihemko badala ya hekima. Ndipo tunapojikuta tunapiga, tunatukana, tunafoka na baadaye tunajutia.


Tufanyaje kudhibiti hasira zetu kabla ya kuwaadhibu/ kuwaadabisha vikali watoto wetu?

Kupumua taratibu kwa kina.

Pale tunapojikuta tumefika kilele cha hasira, mwili huanza kutoa ishara za tahadhari, mapigo ya moyo huongezeka, pumzi hufupika, na mawazo huchanganyika. Mara nyingi sauti ya ndani hutusukuma kuchukua hatua ya haraka, mara nyingine kwa namna ambayo baadaye hutufanya tujutie matendo yetu.

Katika wakati huo, pumzi ni msaada wa kwanza wa dharura. Tukivuta pumzi kwa kina kupitia pua, tukaiweka kwa sekunde chache, kisha tukaitoa nje taratibu kupitia mdomo na tukarudia hii mara kadhaa tunaongeza hewa safi (oxygen) kwenye ubongo na kuipa miili yetu nafasi ya kutulia, na akili zetu nafasi ya kufikiri kwa makini kabla ya kutenda.

 

Kujitenga kwa muda mfupi – “a moment of silence” kwa mzazi.

Kama vile tunavyoweka mtoto pembeni kwa muda ili atafakari matendo yake (timeout), sisi wenyewe tunahitaji muda kama huo. Tukihisi kwamba hasira imefika kiwango cha kutufanya tupige, tuseme maneno makali au kuchukua maamuzi ya ghafla, ni busara kujitoa kwenye eneo la tukio hata kwa dakika chache.

Tunaweza kujitenga na tukakaa sebuleni peke yetu, jikoni, au hata nje ya nyumba, popote ambapo tunaweza kupata kupumzisha akili. Hii siyo udhaifu, ni ujasiri. Inatupa nafasi ya kupanga mawazo yetu kabla hatujaharibu uhusiano wetu na watoto kwa maneno au matendo yasiyo na uzito wa busara.

 

Tujiulize: “Tunataka mtoto wetu ajifunze nini kutokana na hali hii?”

Kabla hatujachukua hatua yoyote, tujiulize, tunachotaka kufanikisha ni nini? Je, ni kutuliza hasira zetu? Kumdhalilisha mtoto? Au ni kumfundisha tabia njema kwa njia itakayomsaidia kujifunza, na sio kuumia?

Swali hili linatufanya tusimamie lengo letu na sio hisia. Kama nia yetu ni kujenga, basi tutachagua njia ya maelezo, mazungumzo, na adhabu mbadala zinazojenga badala ya kuharibu na kuumiza.


Tuzungumze nao kwa utulivu baada ya hali kutulia

Tunapokuwa tumetulia, na mtoto pia ametulia, hapo ndipo nafasi bora ya kuzungumza hutokea. Sauti yetu iwe ya upole lakini ya kusisitiza. Tuseme kile kilichotokea, kwanini hakikubaliki, na ni nini tunachotaka kifanyike tofauti siku nyingine.

Mfano: “Ulipopanda dirishani, tulihisi hofu kubwa sana. Dirisha lile ni hatari, na tusingependa ujeruhiwe. Ni wajibu wetu kukulinda na ni wajibu wako kucheza kwa tahadhari, na ni muhimu usirudie tena.”

Mtoto anapojua kuwa sisi tumekasirika kwa sababu tunamjali, si kwa sababu ya hasira tupu, anaanza kuona msingi wa maadili tuliyonayo.


Kutumia adhabu mbadala.

Badala ya kipigo, kelele au matusi, tunaweza kuchagua adhabu  chanya na zenye lengo la kujenga uwajibikaji: Mfano;

 

-Kumuweka mtoto pembeni au chumbani kwa muda mfupi, ili afikirie matendo yake (timeout)

 

-Kunyima muda wa michezo, simu au runinga kwa muda fulani

 

-Kumpa majukumu ya kusaidia nyumbani kama njia ya kutafakari tabia

 

-Kufanya tathmini ya kila wiki ya mienendo yao, kwa pamoja, na kuweka malengo mapya

 

Adhabu hizi haziumizi mwili wala moyo wa mtoto, bali zinamfundisha kuwa na uwajibikaji na kuelewa athari za matendo yake.


Tunapopiga au Kufoka , Je, Tunafundisha Nini?

Watoto wetu hujifunza zaidi kupitia vitendo vyetu kuliko maneno yetu. Tunapochagua kupiga au kufoka, mara nyingi wanajifunza kwamba matatizo hutatuliwa kwa nguvu na mabavu. Baadhi yao hufunga mioyo, hukua na hofu, au hujifunza kuwa wakali na wakatili kwa wengine.

Utafiti kutoka American Psychological Association unaonesha kuwa watoto wanaolelewa kwa kipigo cha mara kwa mara hukua na tabia za uasi, huzuni ya muda mrefu (depression), na msongo wa mawazo (anxiety). Wengine hupoteza uwezo wa kujithamini na kuiona dunia kwa jicho la hofu.


Tunachohitaji ni nidhamu Inayojenga, ile tunayoiita “positive discipline”. Ni ile inayoweka mipaka bila kuharibu uhusiano wetu na watoto. Tunaweza kusema "hapana", tunaweza kuadhibu, lakini kwa namna ambayo mtoto atajifunza kutokana na makosa yake, atahisi kuthaminiwa, na atakua akiwa na msingi wa maadili na sio hofu.


Sio rahisi kufanya mambo yote hayo, kwasababu wengi wetu hatujalelewa hivyo. Lakini tukumbuke kuwa, hata sisi hatukupenda kufokewa, kutukanwa wala kupigwa hivyo tujitahidi kutokuendeleza tabia hizo kwa hichi kizazi tunachokilea.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

 

 

 

 

 

bottom of page