top of page
  • C-Sema Team

Kuthamini matarajio ya mtoto sio kumdekeza


Kuthamini matarajio ya mtoto sio kumdekeza

Matarajio ya watoto ni jambo ambalo limekuwa halipewi kipaumbele na wazazi ama walezi walio wengi kwa kudhani kwamba watoto ni viumbe wadogo wasio na fikra zenye mashiko. Makala haya yatazungumzia umuhimu wa mzazi kuyathamini matarajio ya mtoto na namna ambazo mzazi anaweza kufanikisha suala hili.


Ukiachilia mbali kwamba wazazi hudhani watoto hawawezi kuwa na mawazo chanya na yanayofikika, pia hufikiri kuwa kumsikiliza mtoto na kuyapa kipaumbele matarajio yake ni kumdekeza au kumvimbisha kichwa na kumpa kiburi, jambo ambalo si sahihi. Ili mzazi aweze kumjenga mtoto anayejiamini na anayeelewa muelekeo wa maisha yake ya baadae, lazima kwanza aweze kuthamini matarajio ya mtoto na kumthibitishia mtoto kadri anavyokua kwamba kinachomsibu yeye mtoto moja kwa moja kinamsibu mzazi pia na kwamba anachokiwaza mtoto juu ya maisha yake ni jambo la maana kama anachokiwaza mzazi.


Mzazi anatakiwa kuyatambua matarajio ya mtoto na kuyapa kipaumbele kwa kumshauri na kumpatia muongozo bora ili kumuwezesha mtoto kufikia malengo yake, jambo ambalo huongeza ukaribu na mtoto katika kubadilishana mawazo na kuwa pamoja. Mara nyingi tunaona watoto wanapoteza muelekeo wa maisha na kupoteza vipawa vyao kwa sababu ya wazazi kupuuzia matarajio yao kwa kigezo kwamba ni watoto. Wazazi wengi wa kiafrika wamekuwa na mfumo wa kidikteta wa kuwalazimisha watoto kufanya maamuzi amabayo siyo vipaumbele vyao katika mambo mbalimbali ikiwemo masomo, michezo, uchoraji, taaluma na mengine kadha wa kadha.


Mfano; mtoto anaweza akawa anafaulu masomo ya sanaa kwa kiwango cha juu na masomo ya sayansi kwa kiwango cha chini sana, lakini mzazi anamgombeza na kusema kwanini haufaulu hesabu na baiolojioa kama wengine? Kwani waliofaulu wana vichwa viwili? Siku nyingine ukirudi na matokeo ya hivi utanitambua! Sipotezi ada yangu ili ufaulu Uraia na Kiswahili, nataka uwe daktari au muhandisi baadae. Au utakuta mzazi anamuadhibu mtoto anayependa kucheza mpira, kukimbia riadha au kuchora kwa kumwambia anafanya mambo ya kipuuzi na kupoteza muda pasipo kufanya jambo la msingi.


Wazazi huyasema haya bila kujali kwamba ni mawazo yao binafsi na si ya watoto wenyewe. Hata kama una matarajio maalum kwa mtoto wakojaribu kuonyesha ushirikiano wako katika kumsaidia, mueleze mtazamo wako juu ya maisha yake una faida gani kwa baadae ili akuelewe na aweze kuamua kufanya mabadiliko. Huenda hajui kwa nini unamtaka afuate mapendekezo yako juu ya maisha yake.


Kumbuka pia masomo anayofaulu mtoto ndipo uwezo wake ulipo na hakuna taaluma isiyokuwa na manufaa bali namna unavyoiendeleza na unavyowekeza katika taaluma husika huweza kuzaa matokeo hasi au chanya. Mzazi unapaswa kuwa makini katika kufanya maamuzi juu ya matarajio ya mtoto wako kwa kuwa ukimlazimisha bila kuweka uchambuzi yakinifu juu ya mtazamo wako, matokeo yake mtoto anafeli akifika mbele ya safari kwa sababu njia aliyoichagua haikuwa matarajio yake na pengine hakikuwa kipaji chake.


Kuna mifano mingi ya watu waliofanikiwa katika maisha kwa sababu tu ya kuendeleza vipawa vyao kwenye michezo na taaluma za sanaa hapa nchini na duniani kwa ujumla wakiwemo mtanzania Hasheem Thabeet mchezaji wa mpira wa kikapu nchini Marekani, Masoud Kipanya mchoraji na muandaaji maarufu wa vipindi vya redio na televisheni na wengine wengi.


Wazazi na walezi hawana budi kuwasiliana na watoto kwa lugha nyepesi inayoashiria kumuelewa mtoto na matarajio yake nani vyema waviendeleze vipawa vya watoto wao na si kuwakatisha tamaa. Pia Mzazi unapaswa kumpongeza mtoto pale anapofanya vizuri halafu baadae ndipo unakaa nae na kushauriana nae kuhusu matarajio uliyonayo juu yake.


Tunaposema watoto wapewe kipaumbele juu ya matarajio yao binafsi, hatumaanishi matarajio ya mzazi juu ya mwanae ni mabaya au hayana maana. La hasha! Mawazo ya mzazi yana umuhimu mkubwa pia ila suala la msingi ni kumshirikisha mtoto katika kufanya maamuzi yanayogusa maslahi yake kama mtoto na kwa kuhakikisha unakuwa mzazi bora kiasi cha kutambua udhaifu na vipawa vya mwanao ili kumpatia mwongozo bora katika kufanya maamuzi yenye tija kwenye maisha yake ya sasa na ya baadae.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Instagram: @sematanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

4 views

Recent Posts

See All

留言


bottom of page