top of page
  • C-Sema Team

Je una malengo ya malezi ya mwaka mpya?


Tunapouanza mwaka mpya wengine tunaona kama Januari 2018 ilikuwa jana, si jambo la kushangaza namna muda unavyokwenda kasi. Ghafla unajikuta katika mwaka mwingine na watoto wanaongezeka kimo na umri kila mwaka. Je umejiwekea malengo gani ya malezi kwa mwaka ujao wa 2019? Kulea ni changamoto kwa kila mzazi, lakini siku hata siku tunajifunza kuwa wazazi bora zaidi ya jana!


Tumekuwekea hapa baadhi ya mambo unayoweza kuyajumuisha katika malengo yako ya malezi mwaka 2019:


Tenga muda wa faragha na watoto wako. Iwapo unao watoto zaidi ya mmoja, fanya kila uwezalo kupata wasaa wa kuketi na kila mmoja faraghani hata kama ni siku moja tu katika mwaka mzima. Hapa utampa mtoto fursa ya pekee na kujenga mahusiano baina yenu, akueleze mipango alonayo na wewe umshauri. Tumia muda huu adimu wa faragha kumsikiliza zaidi. Inashauriwa uwe rafiki wa kwanza wa kuaminika wa mtoto wako kabla hajajenga urafiki na mtu mwingine yeyote.


Azimia kutomlinganisha mtoto wako na watoto wa wengine. Watoto huzaliwa na vipaji na karama tofauti. Wapo wenye vipaji vya kuelewa kwa wepesi wawapo shuleni na hivyo kuongoza katika mitihani ya darasani. Kamwe usishawishike kutaka mtoto wako afanane na wa majirani zako katika uwezo wa kufanya au kuelewa mambo. Yawezekana kuwa anayo-karama tofauti na ile ya mtoto wa jirani. Mtie moyo kujijenga katika eneo analolimudu (alilokarimiwa na Mungu). Mafanikio maishani hutegemea juhudi katika stadi na fani anazozipendelea mtu.


Mfunde mwanao stadi mojawapo mwaka huu. Zipo stadi kadhaa muhimu katika maisha ya binadamu ikiwamo kupika, kufua, kutunza bustani, usimamizi wa fedha na kadhalika. Panga mwaka huu kumfunda mwanao japo mojawapo ya stadi za maisha ili baada ya mwaka 2019 awe amesogea hatua moja mbele kuelekea maisha ya kujitegemea. Nani asiyemkumbuka mama au baba yake kila anapoingia jikoni kupika ama kupasi nguo zake hasa kama walihusika kumuandaa katika haya?


Fundisha ukarimu na kuwa na moyo wa kujitoa kwa ajili ya wenye uhitaji. Hakuna binadamu anayezaliwa na roho ya korosho, na mwenye roho mbaya ya kuzaliwa nayo. Hizi tabia kama ilivyo ukarimu, watoto hufunzwa toka katika maisha ya watu wazima wanaowazunguka ikiwa ni wazazi, ndugu wa familia tandaa au majirani. Hata hivyo, sote tunapenda binadamu wakarimu na wenye kujitoa kwa ajili ya wenzao. Bahati nzuri tabia hufunzwa zaidi kwa maono na vitendo. Ukitaka kupanda ukarimu, anza wewe kuwakarimu watu na mtoto ataiga. Vilevile unaweza kumshawishi mtoto mwende mkatembelee kituo cha watoto yatima na huko atajifunza mengi kuelekea ukarimu.


Usiendekeze kazi za ofisini nyumbani. Hasa kwa wazazi wanaofanya kazi maofisini kupitia kompyuta na simu zao. Ukiwa nyumbani, uwe nyumbani uwe na wanafamilia. Unakuta mtu yuko nyumbani lakini simu haimtoki masikioni akipokea na kutoa malekezo ya namna kazi zinavyofanyika huko ofisni. Mwingine yuko tu kwenye kompyuta yake akiendelea na kazi huku mtoto akimshangaa kwa alivyo mbinafsi. Watoto wanatuhitaji sana kuwa nao tuwapo nyumbani, hebu na tupange kubadilika katika mwaka huu mpya wa 2019.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram: @sematanzania na www.sematanzania.org

0 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page