top of page
  • C-Sema Team

Je, ni chakula gani umlishe mwanao katika mwaka wake wa kwanza?

Anza vyakula vya kulikiza kuanzia mwezi wa 6.

Kumbuka kabla ya kuanza vyakula vigumu mwanao anatakiwa awe ana uwezo wa kukaa, awe ameweza kukaza shingo, kugeuza kichwa chake na baadaye sasa anaweza kufanya kitendo cha kutafuna. Anapaswa awe amekwisha kuvuka hatua ya tendohisisa (reflex) lililokuwa likimfanya kutema kila kitu ikwemo na vyakula vya maji maji.Endelea kunyonyesha au kutumia maziwa mbadala (yenye kanuni ya unyonyehaji).

Watoto mara nyingi huwa hawaanzi kula vyakula vingi vya kulikiza kwa mara moja. Kumbuka kwamba vyakula hivyo vya kulikiza haviwezi kuwa mbadala wa kunyonyesha au maziwa ya kopo yenye kanuni ya unyonyeshaji. Kumbuka unamuanzishia mwanao vyakula vya nyongeza na siyo kwamba ndiyo unamuachisha kunyonya au kusitisha maziwa ya kopo moja kwa moja. Hilo la kumuachisha huwa linakuja taratibu kadri muda unavyokwenda anazoea.


Hivi ni lazima kuanza na nafaka?

Kusema kweli huwa hakuna kanuni ya chakula kipi kianze. Inashauriwa uanze na chakula cha aina moja ili uweze kujua ni chakula gani kinachomletea mwanao mzio (allergy). Siyo lazima uanze na nafaka ila inapobidi kuanza na nafaka bado si jambo baya. Unaweza kuchanganya na maziwa uliyomkamulia au maziwa ya kopo yanayotumia kanuni za unyonyeshaji kulingana na umri ili jambo hilo lisiwe la kushitukiza. Ongeza ugumu taratibu kadri anavyoendelea kuzoea na hatimaye atazoea kula.


Lini ataweza kula kwa kijiko?

Kula kwa kutumia kijiko siyo jambo ambalo ni la kawaida kwa mwanao kwani mpaka sasa amekuwa akitumia vyakula vya majimaji. Hivyo vuta subiri atahitaji muda ili kuzoea kulishwa kwa kutumia kijiko achilia mbali kulishwa vyakula vigumu ambavyo hajavizoea pia. Ataweza kula kijiko kimoja au viwili mwanzoni na kadri muda unavoendelea ataweza kuongeza kiwango.


Anza aidha na matunda au mboga za majani.

Watoto wanaweza kukataa chakula. Kumbuka kusema mtoto huyu amekataa chakula fulani ni lazima awe angalau amekikataa mara 5 mpaka 10. Uweza kumuanzishia mwanao chakula kimoja baada ya kingine kuona kama vitamletea shida mfano mzio (allergy). Pia fuatilia kuona anapenda chakula gani chenye ladha gani. Nafaka, matunda, mboga za majani na hata nyama za kusaga zinaweza kuwa sehemu ya menyu yako. Pale unapohisi mwanao ana mzio na chakula chochote kile basi wasiliana na daktari wa watoto.


Epuka maziwa ya ng'ombe na asali.

Madktari wengi wa watoto wanapendekeza wazazi kusubiri mpaka watoto wao watakapofikisha mwaka mmoja ndipo waanze kuwapatia maziwa ya ng'ombe. Hii ni kwa sababu maziwa ya ng'ombe hayashabihiani na maziwa ya mama kwa ubora wa virutubisho vilivyomo. Maziwa ya ng'ome yametengenezwa mahususi kwa ajili ya mtoto wa ng'ombe aliye na mahitaji tofauti na mahitaji ya mtoto wa binadamu. Asali kwa mtoto wa chini ya mwaka mmoja siyo nzuri kwa sababu ya hatari ya kupata (ubotuli) botulism ambayo inayofanya kinga ya mtoto kutoshuka.


Utajuaje mtoto wako ameshiba unapomlisha?

Utajuaje kwamba mtoto wako ameshiba? Swali zuri sana. Utajua baada ya kuwa mtoto mwenyewe ameacha kula, anasukumia mbali chombo unachomlishia, amefunga mdomo wake, anatema pale unapoendelea kumlisha au hata anageukia upande mbali na chakula - na ukimlazimisha anaweza hata kulia. Watoto huwa wanakula wanapokuwa na njaa na wanaacha pale wanaposhiba. Kamwe usimlazimishe kula zaidi ya kile anachohitaji. Ukizangatia kanuni na kuheshimu hizo silka zake (instincts) utamsaidia kujenga tabia ya kutokula kupita kiasi hata atakapokuwa mtu mzima.


Una mtoto asiyependa kula? Usikonde

Vuta subira iwapo mwanao hapendi vyakula vyako vipya. Kwani haimaanisha atakuwa hivyo kila siku. Subiri kwa muda mchache kisha mjaribu tena, na tena, na tena. Kumbuka usikate tamaa wewe kionje chakula kile na ukifurahie na mwanao akiona wewe unakifurahia nae atakipenda. Usitumie nguvu kumlazisha mwanao kula wala usiumie kuona mwano hapendi chakula. Kwani itamchukua muda mpaka atakapoanza kuvizoea na kuvipenda. Atakushangaza!


Atajichafua atakapokuwa anakula mwenyewe.

Ni jambo la kawaida kwamba mtoto anapokuwa anaanza kula mwenyewe huwa anajichafua. Kujifunza kula kwa mwanao huambatana na karaha. Weka mkeka mdogo chini anapokalia ili kuweza kusaidia kutochafua sehemu zingine. Mvalishe vazi maalumu hata ukiweza aproni ili kusaidia kutochafua nguo zake nzuri. Mwisho tambua pia huyo ni mtoto anajifunza kula na hali hii itaisha mwishowe.


Anza kumlisha vyakula kwa mkono pale mwanao anapokuwa tayari.

Jaribu kuanza kumuachia mwanao kushika na kula peke yake. Tegemea kuanzia mwezi wa 9 mwanao ataanza kuokota mabaki ya chakula na kupeleka mdomoni kwa mikono yake mwenyewe. Anza kumuanzishia vyakula laini kama ndizi, karoti zilizopikwa, yai la kukaanga na vingine utakavyoona vinafaa. Hata hviyo bado utahitajika kuendelea kumnyonyesha bila kuacha. Epuka vyakula vigumu kama vile chips, viazi vibichi, soseji n.k.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org

0 views

Comments


bottom of page