Kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa watoto limekuwa tatizo kubwa katika jamii yetu. Pamoja na mambo mengi yanayochangia tatizo hili, kutokuwepo kwa ushirikiano kati ya walimu na wazazi katika kumlea mtoto kitaaluma ni kikwazo kikubwa ambacho makala hii itaangazia.
Wajibu na majukumu ya mzazi kwa mtoto wake anapokuwa nyumbani jioni baada ya shule (ama likizoni kwa wale wanaosoma shule za bweni) ni pamoja na kufuatilia kazi za mtoto za darasani na kudadisi maendeleo yake kitaaluma. Ingawa tafiti nyingi Duniani zinaelekeza kwamba watoto wanaoangaliwa kwa karibu na wazazi wao huwa na uhakika wa kufanikiwa masomoni kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wale wanaochwa kujipanga wenyewe, hapa Tanzania wazazi wachache sana wanafanya hivi na kuifanya kazi ya mwalimu darasani kuwa ngumu na kuchangia kufeli kwa wanafunzi walio wengi.
Tunajua binadamu hutengeneza kiasi kikubwa cha tabia kutokana na mazingira anayoishi hivyo mazingira mazuri nyumbani ni muhimu katika utengenezaji wa tabia za watoto. Mathalani kama mama na baba hamsomi vitabu, magazeti na hata vitabu vya dini itakuwa vigumu kwa mtoto wenu kuwa na tabia ya kujisomea. Mtoto anajifunza kwa wepesi zaidi kwa kuona unachofanya (vitendo) mzazi zaidi ya unayoyasisitiza kwa maneno. Ukitaka kuwa na Daktari, Mwanahabari ama Mhandisi kwenye familia yako unapaswa kuandaa mazingira sasa kwani mchicha hauzai mihogo. Unavuna unachopanda. Lawama kwa serikali haziwezi kutatua changamoto za elimu katika ngazi ya familia. Timiza wajibu wako kwani mzazi ni mwalimu nambari moja wa mtoto wake.
Aghalabu utasema mimi sijasoma vipi nimwongoze mwanangu kimasomo? Huitaji kuwa na elimu ili kuwa mzazi. Vilevile wewe kama kiongozi kwa mwanao (umeliona jua kabla ya mwanao), unayo mifano chanya ya watu katika jamii waliopata si tu kuondoa ujinga kwa kupata elimu bali pia kupambana na ukwasi uliozikabili familia zao baada ya kuwa wamefanikiwa kupata elimu mujarabu. Mwonyeshe na mweleze mwanao mifano hii. Pengine haoni na hajui kwa nini aende shule na kwa nini afaulu. Mifano hii itamsaidia kumtia moyo ya kwamba inawezekana. Kwamba hata kama yuko katika shule zenye walimu kiduchu na vifaa haba, akiweka nia anaweza kufaulu masomoni.
Jambo jingine ni mahusiano yako na waalimu wa mwanao. Tenga muda uende shuleni uwatembelee waalimu na kuzungumzia maendeleo ya mtoto wako. Kama wewe hujali, vipi mtu baki (mwalimu) yeye ajali maendeleo ya mwanao darasani? Kadiri unavyokiuka wajibu na majukumu yako katika malezi ya watoto na kuwaacha watoto wajilee wenyewe kama uyoga, waalimu nao watawapa huduma za namna hiyo. Inafika mahala mwalimu anamwagiza mtoto ili wewe mzazi uende shuleni kuzungumzia maendeleo ya mtoto wako lakini wewe unakaidi na wakati mwingine kwa kejeli za mwambie niko bize. Sasa kama wewe uko bize yeye mwalimu kwanini asiwe bize na wazazi wanaojenga ukaribu na kuitikia miito ya waalimu?
Baadaye utasema toto hili bure kabisa limenipotezea fedha na muda kwani limefeli mitihani. Kufaulu kuna gharama zake. Pamoja na fedha unazolipa kwa ajili ya ada na mahitaji mengine shuleni, unahitaji kufuatilia maendeleo ya mwanao ili kuhakikisha unatoa ushauri na kumtia moyo ili aweze kufaulu.
Tambua kwamba jukumu la kumpatia mtoto elimu haliishii katika kumuandikisha shule tu bali ni pamoja na kufanya ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo yake shuleni na kumsaidia kufanya mazoezi ya nyumbani (home work) aliyopewa na mwalimu (pale inapowezekana), kujenga ukaribu, urafiki na ushirikiano na walimu ili kumsaidia mtoto kuona umuhimu wa elimu na kulipa kipaumbele suala la elimu yake, kwa kutambua kuwa elimu ndiyo urithi pekee unaoweza kumwachia mwanao na ukawa na uhakika wa maendeleo yake ukubwani.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org