top of page
  • C-Sema Team

Je inawezekana mwanao kuepuka vishawishi vya makundi-rika?


Waingereza wanaita 'peer-pressure', yaani makundi-rika kwa lugha ya madafu. Watoto katika umri tofauti wa ukuaji wao wanakutana na vishawishi ama chanya au hasi kutoka kwa marafiki zao. Makala haya yanahoji iwapo wazazi/walezi tunaweza kupunguza uwezekano wa mtoto kuharibikiwa kutokana na msukumo wa makundi-rika. Namna gani unaweza kumsaidia mtoto wako kusema ndiyo kwa makundi rika chanya na hapana kwa makundi rika hatarishi. Mbinu zifuatazo zinaweza kukusaidia kumuongoza mtoto katika hili.


Mosi. Wajue marafiki na wote anaoshinda na mtoto wako. Hasa kama hujakutana nao ana kwa ana, fanya jitihada ya kuwafahamu na kwanini wanampenda au kumchukia na ujue ni vishawishi gani walivyonavyo kwa mtoto wako. Mwonyeshe mtoto unajali rafiki zake na namna hii utafungua milango ya urafiki na kuaminiana baina yako na mtoto. Usiwe mhukumu wa tabia, kuwa mshauri.


Zungumza na mwanao kuhusu tunu (Values). Mwambie ni nini kitu muhimu kwako, ajue kama ungependa kuona akifanya vizuri katika masomo yake, anajali na kuwa msaada kwa watu wengine na kutojihusisha na ngono katika umri mdogo. Kuwa muwazi juu ya tunu zako na kwa nini ni muhimu kuwa nazo ili imsaidie kufanya maamuzi sahihi.


Kwa mzazi mwenye mtoto kuanzia umri wa mwaka 1 hadi 5, mwanao akianza kufanya maamuzi yasiyofaa au kushawishiwa vibaya na makundi rika muepushe kwa kumpatia kazi/michezo chanya ya kumpotezea fikra za makundi rika. Ukiona habadiliki, mueleze kwa ufupi kwanini maamuzi yake au vishawishi ni hatari na kumpa mbinu mbadala za kufanya maamuzi sahihi. Kwa mfano mueleze mwanao kuwa si tabia nzuri kutumia lugha za matusi hata kama tumekasirika. Vilevile chunguza ni wapi kajifunza lugha hizo.


Kwa mzazi mwenye mtoto kuanzia umri wa miaka 6 hadi 9, waalike marafiki wa mtoto wako wacheze na mwanao nyumbani kwako ili upate fursa ya kujua tabia zao na mambo gani wanashawishiana. Wape muongozo pale utakapoona wanatoka nje ya mstari. Wajue wazazi wao vizuri (tunu zao pia), wajue majirani watoto/watu wazima wanaokuzunguka ili kujua kama lipo jambo hatarishi pasi wewe kujua. Shirikiana na wazazi (majirani) wenye maono kama yako kwani si rahisi kumlea mtoto pekee yako! Unahitaji timu ya marafiki na wazazi wenzako kukuza watoto wema katika jamii kamA wasemavyo wahenga, kidole kimoja hakivunji chawa.


Kwa mzazi mwenye mtoto wa miaka 10 hadi 15, hapa hatari ya kudumbukia katika vishawishi vya makundi rika ni dhahiri na vigumu kwa mtoto kujiepusha nayo hata kwa yule mwenye uwezo wa kukwepa vishawishi. Umri huu ni changamoto kwa mzazi kumshawishi mtoto kubadilisha maamuzi kwa kuwa kipindi hiki anapata dhana ya kujitegemea hasa kimaamuzi. Ili kuwasaidia watoto wa umri huu, jadili nao kuhusu changamoto za vishawishi wanazokumbana nazo wawapo shuleni au mtaani, kuwa mpole na mvumilivu kwa kuwa mtoto wa umri huu mara nyingi hueleza na kufanya mambo pasi na uoga wa matokeo/madhara yake.

Wazazi wenye watoto wa miaka 16-18, umri huu mara nyingi watoto hufikiri wameshakuwa wakubwa vyakutosha kuweza kujisimamia. Hapa makundi-rika humsukuma kutaka kujua pombe ina ladha gani? Sigara, bangi na huanza mara nyingi kudadisi mambo kama busu, ngono, nk. Hapa mtoto anwaamini marafiki zaidi kuliko wazazi. Mzazi unashauriwa kubadili namna ya kuwasiliana, mfanye ajisikie kuwa mtu mzima huku ukimuusia kuzikumbuka tunu na maadili mema. Jitahidi usitumie vitisho kama ukichelewa, usiingie kwangu.Bali kuwa muwazi juu ya tabia zinanzo kubalika na kumuonyesha mifano ya watoto wema na wenye mafanikio katika Jamii. Jenga ukaribu na waalimu na majirani ili kuweza kujua tabia zinazojitokeza akiwa nje ya nyumbani. Pia wazazi wanashauriwa kutoangalia mabaya tu bali kuwasifia watoto pale wanapofanya vizuri ili kuwapa moyo wa kuendelea kutenda mema.


Si rahisi kwa mtoto kuepuka vishawishi vya makundi rika, ni vyema wazazi kuwa wavumilivu, kuwa karibu na watoto na kuwashauri kadri wanavyobaini mabadiliko ya tabia kwa watoto.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.


13 views

Recent Posts

See All

コメント


bottom of page