Makala haya yametokana na mazungumzo baina yetu na mtaalamu wa malezi Dr.Nkuba Mabula (PhD) wa Kitivo cha Elimu na Saikolojia Chuo, Kikuu Cha Dar Es Salaam. Dr. Nkuba ameeleza kuwa wazazi wengi wanaotumia adhabu ya viboko huamini kwamba adhabu hizi humjengea mtoto tabia sahihi, maadili, uwezo wa kujitawala - kwamba tabia njema hujengwa kwa kumnyanyasa mtoto ama kumpa maumivu, humfunza uwajibikaji, humtengenezea tabia njema na pia humuongezea kujithamini.
Dr. Mabula hakubaliani na nadharia hizi kwa kuwa tafiti mbalimbali kote duniani zinaonyesha kuwa adhabu za viboko huleta matokeo ya muda mfupi na sio ya kudumu. Viboko huwa havitoi suluhu juu ya hatua za kufata ili kumjenga mtoto kuwa mtu bora zaidi.
Dr Mabula anasema kitaalamu ili mtoto apate uelewa juu ya maadili na kutambua lipi jema na lipi baya kwa kina - hawezi kujifunza kwa kupitia maumivu au mateso. Matokeo ya vipigo ni kumjengea tabia za udanganyifu, kushidwa kujisimamia mwenyewe na hupelekea kukosa mbinu mbadala zinazomuwezesha kushirikiana na jamii inayomzunguka kikamilifu pasi ugomvi.
Viboko hukuaminisha juu ya mabadiliko ya tabia ya mtoto na lakini mabadiliko hayo huwa ni ya muda mfupi. Mara nyingi mtoto hulazimika kufanaya hivi ili kuepuka adhabu kutoka kwa wazazi iwapo watagundua hakuna mabadiliko yoyote ya kitabia. Unamfundisha usanii mara moja anakuwa na tabia mbili mbili. Tabia akiwa mbele yako na tabia akiwa nje ya uwepo wako. Vilevile Dr. Mabula anasisitiza kuwa tafiti zake hapa nyumbani zmegua kwamba mara nyingi adhabu hizi hujenga chuki na kutoelewana baina ya mzazi na mtoto, mwalimu na mtoto, nk. Kwamba adhabu hizi ndio chanzo cha uwepo kwa watoto watukutu na wasiofundishika katika jamii kwa kujenga usugu kwa viboko.
Dr. Mabula alieleza kuwa asilimia kubwa ya wazazi wanaotumia njii hii ya urekebishaji tabia hudai kwamba ni njia rahisi isiyotumia muda wala nguvu nyingi tofauti na njia nyingine. Lakini ukweli ni kwamba njii hii hugeuka kibarua kwani mtoto hujikuta akirudia makosa yale yale kwa maana hakufundishwa njia mbadala za kutumia kuepuka kurudia makosa. Njia mbadala wa viboko na ambazo sio za kikatili, anasema Dr Mabula kwamba ingawa mzazi hutumia nguvu nyingi na muda mwingi mwanzoni katika kurekebisha tabia, njia hizi hupunguza uwezekano wa makosa kujirudia kwa kiwango kikubwa na hivyo kuokoa muda wa mzazi.
Wataalumu wa malezi wanasema jambo la muhimu katika malezi mbadala wa viboko ni kuuliza maswali. Maswali kama: je nataka mtoto wangu akikua awe mtu wa namna gani? Vipi awe mkarimu na mwenye mchango muhimu kwa jamii? Mwenye hekima-katika-maamuzi? Asiwe mgonvi. Anipende na aipende familia yake - mwenza wake na watoto akijaaliwa. Iwapo una matamanio kufikia walau moja ya malengo hayo, huihitaji kiboko kama nyenzo. Unachohitaji ni mkakati. Kwamba mikongoto itakusaidia kutoa hasira zilizokujaa wakati huo wa kosa la mtoto. Mazungumzo yatakusaidia kumfanya mtoto sehemu ya mipango ya kufanikisha kujenga tabia ya mtu mzima wa matamanio yako.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
Comments