top of page
  • C-Sema Team

Ijue sheria ya viboko mashuleni

Hivi karibuni na hasa juma hili kumekuwa na taarifa za matukio mengi ya walimu kuwaadhibu wanafunzi kwa viboko kiasi cha kupelekea vifo, maumivu makali, majeraha na hata ulemavu. Adhabu hizi zimekuwa zikitolewa na walimu bila kuzingatia miongozo ya kanuni na sheria za utoaji adhabu dhidi ya makosa mbalimbali zilizowekwa na serikali kwa mujibu wa sheria na hivyo kupelekea madhara makubwa si tu kwa watoto pekee bali wazazi na uongozi wa shule kwa ujumla.


Sheria ya Elimu Sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002 inampa mamlaka waziri wa elimu kutunga kanuni za masuala mbalimbali zitakazokidhi utekelezaji wa masuala ya sheria hiyo. Mojawapo ya kanuni zilizotungwa ni The Education (Corporal Punishment) Regulation G.N.294 ya mwaka 2002. Kanuni hizi zinatoa mwongozo ni wakati gani adhabu ya viboko inatakiwa kutolewa na kwa kiwango gani.


Kanuni ya 3 (1) inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhabu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya viboko itolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko 4 kwa tukio lolote.


Nani Ana mamlaka ya kumchapa mwafunzi kisheria? Sheria inampa mamlaka mwalimu mkuu wa shule husika kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo.Mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakuwa na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini ya mwalimu mkuu katika tukio husika.

Kanuni ya (5) inataka kila adhabu ya viboko inapotolewa kwa mwanafunzi kumbukumbu ya kutolewa kwa adhabu hiyo sharti iwekwe kwenye kitabu, ikitaja jina la mwanafunzi, kosa alilolifanya, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu. Na kumbukumbu hizo lazima zisainiwe na mkuu wa shule.


Sheria hii inataka uchunguzi na kujiridhisha kuwa mwanafunzi amehusika moja kwa moja na kosa analotuhumiwa nalo ndipo hatua ya kupeleka suala lake mbele ya mwalimu mkuu ili atumie mamlaka alopewa kisheria kutoa adhabu stahiki kwa mwanafunzi linafuata. Laiti sheria hii ingezingatiwa kusingekuwa na taarifa za vifo vya wanafunzi vitokanavyo na adhabu za viboko.


Ni vyema pia kabla hata adhabu haijatolewa mtoto apewe fursa ya kujieleza na kusikilizwa, ikiwezakana mzazi wa mtoto husika aitwe na afahamishwe juu ya tatizo na dahabu ijadiliwe. Wazazi na walimu tumekuwa tukiongozwa na jazba katika kuwaadhibu watoto na matokeo yake tunajutia jazba zetu. Ni vyema kujipa muda wa kufikiri na kushusha jazba kabla ya kutoa adhabu. Kwa mfano adhabu alopewa mtoto huyu hakustahili kabisa hata kupelekwa kwa mwalimu mkuu kwa kuwa ilikuja kugundulika mwalimu alisahau pichi lake kwenye pikipiki (bodaboda) iliyomleta shuleni hapo. Walimu tusiongozwe na hasira katika kuadhibu watoto kwa makosa ambayo pengine hayahitaji adhabu ya viboko.


Waaalimu wanatakiwa kufahamu vyema kanuni hizi za adhabu mashuleni na pia waifahamu vyema sheria ya mtoto nambari 21 ya mwaka 2009 ili kujiepusha na madhila haya. Ukiacha kumuumiza mtoto na familia yake, pia mwalimu ukikutwa na hatia ya kupiga hadi kuua hata wewe maisha yako unayaweka hatarini moja kwa moja. Wahemga wanasema fikiri kabla ya kutenda na majuto ni mjukuu, tuzingatie misemo hii kujiepusha na shari zinazoweza kuepukika.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

2 views

Recent Posts

See All

Comentarios


bottom of page