top of page
  • C-Sema Team

Hivi ndivyo unaweza kumrithisha mwanao tabia njema


Malezi - tabia njema

Katika mchakato wa kutekeleza jukumu la malezi kuna changamoto nyingi lakini kila mzazi ampokeapo mwanae mikononi kwa mara ya kwanza huwa ana matarajio ya kukuza mtoto mwenye tabia njema. Imekuwa ni vigumu kwa wazazi wengi kupata jibu wanapoulizwa je, ungependa wanao warithi tabia zako? Swali hili litakuwa rahisi sana kulijibu endapo utafanya mambo 8 yafuatayo.


Ukiingia ndani ya nyumba bisha hodi, waslimie wanao na kuwakumbatia kwa upendo. Namna hii itawasaidia watoto kukuza dhana ya upendo na kujiamini baina yao na ndugu wengine wa familia.


Kuwa mtu mwema kwa majirani zako na usiwe mtetaji. Usiwazungumzie vibaya majirani zako na watu wengine huku watoto wanasikia, kumbuka ukifanya hivyo watoto wanaiga na kuiishi tabia hiyo wakijua ni ustaarabu wa maisha wa kawaida.


Wapigie simu au watembelee wazazi wako mara kwa mara na wahimize watoto kuzungumza nao, pia fanya hima watoto wajenge tabia ya kuwatembelea wazazi wako (bibi/babu zao), kwa kufanya hivi watajifunza kutoka kwako umuhimu wa kuwajali na kuwatunza wazazi na vivyohivyo kwako watafanya wakiwa wakubwa.


Jenga tabia ya kuwahadithia hadithi za kuwajenga, jadiliana nao masuala mbalimbali ya msingi ukiwa unawaendesha kwenda shule, mkiwa nyumbani siku za mapumziko, mkiwa jikoni mnapika au shambani badala ya kuwapigia mziki, kuangalia televisheni au kwa kukaa kimya na kuweka mpaka kati yenu mnapopata fursa hizi za kukaa pamoja, hii itawajenga sana kifikra na kitabia pia.


Kuwa na tabia ya kuwasomea hadithi fupi kwenye vitabu mbalimbali, wasomee pia vifungu vya neon la Mungu kutoka kwenye vitabu vya dini. Sali nao na uwafunze jinsi ya kusali ili waige kutoka kwako, hii itawasaidia kuwa na imani ya dini lakini pia kuwajengea kumbukumbu nzuri ya mahusiano mazuri na mzazi wakiwa wakubwa. Vyema sana kumkuza mtoto mwenye uoga wa Mungu kwa kuwa inasaidia sana kuepuka changamoto za malezi.


Kuwa mtanashati muda wote, oga,safisha kinywa, chana nywele zako vizuri, vaa nguo safi na nadhifu hata unapokuwa umeketi tu nyumbani ili kuwajengea watoto tabia ya usafi na kujipenda muda wote si pale tu wanapokuwa wanatoka kutembea.


Jaribu kujizuia kutoa lawama au kutoa maoni juu ya kila jambo wafanyalo au neno wasemalo kila wakati. Wakati mwingine kujipa muda wa kuwaacha huru na kutizama matendo na maneno yao kwa kina inasaidia kuzisoma tabia zao na kuwapa muda wa kujifunza na kujiamini. Usiwe mtu mwenye gadhabu na kuwakatisha tamaa wanapotoa wazo au hisia, hii itawaumiza hata kama unatania.


Hakikisha unabisha hodi kabla ya kuingi chumbani kwa wanao, usizame tu chumbani bila ruhusa yao, hii itawapa fursa ya kujifunza kufanya hivyo pale wanapotaka kuingia chumbani kwako. Thamini faragha ya wanao, waombe msamaha wanao pale unapowakosea ili kuwafunza upole na huruma na kuwajengea dhana ya utu na kujithamini.


Yote haya hayafanikiwi kwa siku moja bali ni juhudi za kila siku. Inabidi kama mzazi kuishi tabia na mienendo ambayo ungependa mwanao awenayo. Usikate tamaa katika hili kwani watoto hawasikii na kuelewa siku moja bali yakupasa kuwa mvumilivu na mwenye upendo kufanikisha suala hili.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

0 views

Recent Posts

See All
bottom of page