top of page
C-Sema Team

Hebu tuwalinde watoto dhidi ya unyanyasaji wa kingono mtandaoni

Mwaka 2018 zilipatikana takribani tovuti 105,000 zenye maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto. Tovuti hizi huwa na picha na video nyingi zinazoonesha watoto wakifanyiwa unyanyasaji kingono na kwa mwaka jana peke yake, zaidi ya picha 340,000 zilipatikana katika tovuti hizi na kuondolewa mtandaoni. Takwimu hizi zinatokana na ripoti ya Internet Watch Foundation, shirika linalofanya kazi ya kutafuta na kuondoa maudhui yoyote ya unyanyasaji wa watoto kingono yaliyopo mtandaoni. Picha na video zenye maudhui haya huweza kuripotiwa na mtu yeyote kwa kutumia tovuti maalumu ambayo ipo pia katika lugha ya Kiswahili hapa Tanzania.



Tatizo la kuwepo na kutumika kwa picha za unyanyasaji wa kingono kwa watoto limeenea zaidi katika nchi zilizoendelea kuliko nchi zinazoendelea lakini tatizo hili lipo hata nchini kwetu. Ndani ya miezi mitatu ya mwaka 2019, tovuti inayopokea taarifa za maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto yanayowekwa mitandaoni imepokea taarifa 3 za unyanyasaji huu kutoka Tanzania na kuondoa maudhui haya.

Ni faraja kufahamu kwamba kumbe tunapokutana na picha zenye kuonesha watoto wakifanyiwa unyanyasaji wa kingono mtandaoni, tunaweza kuwasaidia kwa kutoa taarifa na picha hizi zikaondolewa. Lakini hii haitoshi kuwalinda watoto, ni jukumu letu kuhakikisha tunawalinda watoto kwa kuepuka maudhui haya kuwepo mitandaoni na katika vifaa vyetu vya kielektroniki. Fanya mambo yafuatayo ili kumlinda mwanao na watoto wengine dhidi ya maudhui ya kuwanyanyasa watoto kingono mtandaoni.


Mosi; epuka kumpiga mtoto picha akiwa mtupu awe wako ama wa mtu mwingine. Pamoja na kwamba tunapenda kuweka kumbukumbu za wanetu kadri wanavyokua, ni muhimu tujaribu kuweka mipaka ya kumbukumbu tunazohifadhi katika vifaa vya kielektroniki. Huwezi jua nani atachukua na kuona picha hizi 'kama ana nia njema na mwanao ama la' usimpe kisingizio. Lakini vilevile, kabla ya kumpiga mwanao picha akiwa mtupu jiulize, 'Je, baada ya miaka kumi, ataipenda picha hii ama itamfedhehesha na kumfanya ajisikie aibu? Je, utajisikiaje picha hii ikisambaa kwa bahati mbaya?'


Kumbukumbu nyingine tujitahidi kuzihifadhi katika mioyo yetu.


Pili; usisambaze picha za unyanyasaji wa kingono kwa watoto hata kama ni kwa minajili ya kuwaonya wazazi ama kuelimisha jamii. Mara nyingi tumeona picha na video za watoto wakifanyiwa ama kuhojiwa kuhusu unyanyasaji wa kingono zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Facebook na Instagram. Unapopokea picha ama video ya mtoto akifanyiwa unyanyasaji wa kingono, mlinde kwa kuifuta kabisa na kisha waelimishe na wengine waifute ili isisambae zaidi. Hata kama unataka kuwapa angalizo wazazi wengine kuhusu unyanyasaji wa kingono unaoweza kuwakuta watoto wao, tafakari kwanza, 'Ingekuwa picha ya mwanao, ungefurahia kuiona ikisambaa kama angalizo kwa wazazi wengine?'


Ukweli ni kwamba usambazaji wa picha na video hizi humuumiza mtoto anayeonekana humo zaidi na sio kumsaidia kama tunavyodhamiria. Kila picha ama video yenye maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa mtoto inapopakiwa, inaposambazwa, inapopakuliwa au inapotazamwa, mtoto huyo huathirika na unyanyasaji huo upya. Huyu ni mtoto aliye hai na amepitia unyanyasaji wa kutosha tayari. Tumuhurumie!


Tatu, toa taarifa katika tovuti ya taifa ya kuondoa maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto mtandaoni. Watumiaji wa mitandao wanaweza kusaidia kulinda watoto walioathirika na maudhui yanayowaonesha wakifanyiwa unyanyasaji wa kingono kwa kutoa taarifa za picha au video zenye maudhui haya katika tovuti hii: https://report.iwf.org.uk/tz. Namna hii picha ama video hiyo itaondolewa mtandaoni mara moja.

Kwa ustawi wa watoto wetu tunatoa wito kwa jamii nzima ya watumiaji wa mitandao kuelewa kuwa hayupo mtu mmoja au taasisi moja au hata serikali inayopaswa kusukumiwa lawama zote za matukio ya unyanyasaji wa watoto mitandaoni. Jukumu ni langu. Jukumu ni lako. Kunyoosha kidole kwa wazazi wa mtoto unayesambaza picha yake hakukufanyi wewe kutohusika kama sehemu ya unyanyasaji huu. Watoto hawa ni wetu sote. Tuwalinde.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

1 view
bottom of page