Watoto wanazaliwa pasi na uelewa wa kutosha juu ya mahusiano ya kijamii na hivyo kila uchao wanatafuta kwa hamu mtu wa kuiga. Huyu anaweza kuwa mzazi mmoja ama wazazi wote wawili. Wazazi ni waalimu wa kwanza wa watoto na ndiyo hasa mfano wa kuigwa. Bahati mbaya watoto wanaathirika zaidi na kile wazazi wao wanachofanya kuliko kile wazazi wao wanachosema. Wanajifunza jinsi ya kuishi kwa kuona jinsi mama na baba zao wanavyofanya na kwa kufuata mfano wao.
Kuwa wa kutegemewa. Hutaki kukuza mtoto asiyejali wenzake kwa kutokua mkweli. Tunza ahadi ndogo ndogo hatimaye na kubwa pia. Mfano, "Niliahidi kwamba tungeenda mpirani baada ya kusafisha chumba chako, basi hebu twende!" Kamwe usiruhusu kazi na majukumu yako vikunyime fursa ya kutimiza ahadi zako kwa mtoto. Ikiwezekana toa ahadi chache kulingana na uwezekano wa kutimiza. Bora kutokuwepo kwa ahadi kuliko kuwepo kwa ahadi 'hewa'.
Kuwa mwaminifu. Tunaishi wakati ambapo kumuacha "rafiki" kutoka kwenye maisha yako kunaweza kutokea kwa kugusa kwa kitufe katika simu yako. Mfunde mtoto wako namna uaminifu wa dhati na kweli unavyoonekana. Uishi uaminifu. Hata mnapokuwa sokoni na bahati mbaya mkapewa chenji zaidi ya ilivyo-halali. Hebu mjuze muuzaji kuwa kazidisha chenji na mrudishie iliyo halali. Mwanao atajifunza kuwa dhulma si jambo jema.
Kuwa msikivu lakini makini. Watoto wanapoendelea kukua wanahitaji uhuru zaidi ("Mama, tafadhali usiingie chumbani kwangu!") Hii inatarajiwa. Lakini kama mzazi kazi yako sio kuwa 'swahiba wa kizembe' na mwanao. Kazi yako ni kuwa mzazi. Ambayo ina maana kuwa ingawa utamsikiliza bado unahitaji kumlea kwa umakini na kuhakikisha kuwa mtoto wako hapatwi na madhara unayoweza kumwepusha. Hii ina maana kuwa king'ang'anizi hata ambapo mtoto wako anadhani 'unamfuatlia' sana. Mweleze: "Wewe ni wa thamani sana kwangu na ni kazi yangu kuhakikisha kwamba nakulinda na kukujali, daima. Natumaini kwamba siku moja, utaelewa kwa nini ni kazi yangu kuwa makini na kuwajali watu ninaowapenda kama wewe. Natumaini kwamba siku moja ukibahatika kupata watoto, nawe utakuwa na makini namna hii."
Mfunde kuwa na kutetea wazo mbadala. Watoto kwa kawaida huamini watu wazima wanaowazunguka pasi na kujali mienendo halisi ya watu hao. Mapema mwandae mtoto wako kujua kwamba si watu wote ni wa kuaminika. Mjengee hamu ya kuhoji na kutetea wazo mbadala pasi na kugombana. Kwa mfano, katika ununuzi wa bidhaa sokoni, unaweza kumnong'oneza faraghani mtoto wako kwa kusema, "Mtu huyu anasema kuwa hii ndiyo bidhaa nzuri zaidi hapa mjini / kijijini, lakini nina wasiwasi anayotweleza si ya kweli. Hebu tuangalie maduka mengine. Tujihakikishie."
Simamia na toa adhabu stahiki pale mtoto anapokosea. Wazazi wengi wanachelea kutekeleza adhabu wakati mtoto atakapokuwa amekiuka taratibu ama kutenda kosa. Mtoto wako akifanya jambo lisilokubalika, lazima utekeleze wajibu wako kwa kutoa adhabu stahiki. Hii inamaanisha unatekeleza wajibu wako kama mtu wa kutegemewa. Namna hii watoto wanajua upo usawa na ubayana katika maisha na wazazi wao. Bila hivyo, wao hujiona wasio na 'mchango' wowote na wasio na kuthaminiwa katika familia na wana hatari ya kuendelea kuwa watu wazima wasiokuwa na nidhamu na kuwajali wengine.
Kumbuka - sisi wazazi sio wakamilifu. Tunapatwa na hasira na wakati mwingine tunasema mambo tunayojutia na tunatamani kuwa watu wema zaidi ya tulivyo sasa. Sisi ni wanadamu. Ni muhimu kukubali makosa yetu tunapowakosea watoto na kuomba msamaha ili kuonyesha kwamba tunajitahidi kuweka mambo sawa. Kuwa mfano wa kuigwa kwa watoto wako ni moja ya mambo muhimu zaidi na yenye manufaa unayoweza kufanya kwa mtoto wako.
Kommentare