Ukavu na kupasuka kwa chuchu. Unapaoanza kunyonyesha unaweza kukumbana na ukavu na hata kupasuka kwa chuchu. Ili kuepuka adha kama hizi na kufanya unyonyeshaji wako uwe wenye utulivu epuka matumizi ya krimu au losheni zilizo na kemikali ya kileo (alcohol). Vilevile acha kuzipaka chuchu zako sabuni.

Unaweza kupaka lanolini halisi kwenye chuchu zako baada ya kunyonyesha ila kumbuka kuziosha kabla ya kunyonyesha au la sivyo usipake kitu kabisa. Matumizi ya sindiria nayo yanaweza kuwa moja ya sababu kama hubadilishi sindiria mara kwa mara na unapobadili pendelea sindiria za pamba.
Vidonda kwenye chuchu. Mama anaweza kupata vidonda kwenye chuchu katika wiki za kwanza za kunyonyesha. Tambua mbinu za kumweka mtoto vizuri kwenye ziwa ili kuhakikisha mwanao amekaa vizuri kwenye ziwa. Baada ya kunyonyesha tumia kidole chako kuondoa mdomo wa mwanao kwenye ziwa. Hii husaidia kuepuka kupata vidonda kwenye chuchu kwa kubanwa na fizi za meno ya mtoto.
Hata kama una vidonda endelea kumnyonyesha mwanao tena maziwa yote hata lenye vidonda mpaka maziwa yaishe kwani usipofanya hivyo ziwa hilo litazidi kujaa na kuuma zaidi. Kama huwezi kumnyonyesha likamue. Unaweza pia kuweka mfuko wenye mbaazi zilizoganda kwenye chuchu inayouma hii husaidia kuleta nafuu kwa muda. Jitahidi kuweka chuchu zako kuwa kavu au ziache zipigwe na upepo ili zikauke zenyewe kabla hujaendelea kumnyonyesha kwani hii husaidia pia.
Usiwe na hofu kuwa unaweza usiwe na maziwa ya kutosha. Baadhi ya wanawake hufikria kwamba wanaweza wasiwe na maziwa ya kutosha kwa sababu ya matiti madogo. Hiyo si kweli kwani hata wenye matiti madogo nao huwa wana maziwa kama ilivyo kwa wenye matiti makubwa.
Kadri unavozidi kumnyonyesha mwanao mara kwa mara ndivyo maziwa nayo yanvyozidi kutoka. Usimpatie mwanao maziwa ya kopo isipokuwa kwa sababu maalumu ulizozijadili na daktari. Usimpatie hata maji ya kunywa mtoto aliye na umri wa chini ya miezi 6. Endelea tu kumnyonyesha mwanao nae atapata maziwa ya kutosha.
Pale hofu ya kutokuwa na maziwa ya kutosha inapodhihiri ni vyema umuone daktari atakusaidia cha kufanya. Hata hivyo, usisahau kuwa kupata lishe muafaka, maji na usingizi wa kutosha huchangia kupata maziwa ya kutosha kwa ajili ya mwanao.
Je, naweza kukamua na kuhifadhi maziwa?
Unaweza kukamua maziwa na kuyahifadhi. Itakuchukua muda kwa mwanao kuzoea maziwa ya kwenye chupa. Unaweza kukamua kwa kutumia mkono au kwa kutumia chupa maalumu. Hii ni njia nzuri kwa akina mama wanaohitajika kazini mapema kama kazini kwao hakuna chumba maalumu cha kunyonyeshea na hawawezi kwenda na mtoto.
Hivyo anza kujizoesha mapema na wakati ukifanya hivyo mtoto nae atakuwa taratibu anazoea. Maziwa ya mama yanaweza kutumika ndani ya siku 2 baada ya kuhifadhiwa kwenye jokofu. Pia maziwa ya mama yanaweza kugandishwa na kutumika mpaka miezi 6. Usichemshe maziwa yako kwenye mikrowavu (microwave) kwani kufanya hivyo joto lake litaua viini kinga vinavyoboresha kinga ya mwili. Maziwa ya mama yakigandishwa na kukaa muda mrefu unaweza kuyapasha joto kwa kuyaweka kenywe maji ya vuguvuvu.
Chuchu zilizobonyea. Chuchu zilizobonyea ni zile ambazo hazirudi katika hali yake baada ya kubinya chuchu. Tembele kliniki ya mama na mtoto na mtaalamu wa kunyonyesha anaweza kukusaidia kukupatia ushauri wa nini cha kufanya.
Matiti kujaa. Usihofu pale ambapo maziwa yako yamejaa laini na yanayobonyea unapoyabinya kwani hili ni jambo la kawaida kabisa. Hata hivyo una haja ya kupata wasiwasi pale ambapo maziwa yako yamejaa halafu ni magumu, hayabonyei na yanauma. Hii hutokana na damu kurundikana kwenye matiti yako na kwa kufanya hivyo damu hujaa kwenye mishipa yako ya damu na kuyafanya matiti yavimbe, yawe magumu, yenye maumivu.
Katika hali hii unaweza kupunguza maziwa yako kwa kukamua kwa mkono au pampu maalumu. Pia unaweza ukapunguza uvimbe huo kwa kuweka barafu kisha ukimaliza weka maji ya moto. Jaribu njia hizi moja baada ya nyingine na si njia zote kwa mkupuo.
Mifereji ya maziwa iliyoziba. Kuziba kwa mifereji ya kutolea maziwa kunaweza kusababisha kutotoka kwa maziwa kwa ufanisi. Kidoa kimoja cha kidonda kwenye ziwa ambacho ni cheupe na cha moto kinaweza kuashiria kuziba kwa mrija wa kutolea maziwa kwenye titi. Hali hii inaweza kupunguzwa kwa ukandaji na uchuaji wa sehemu yenye kidoa hicho.
Maambukizi ya kwenye ziwa. Huu ni ugonjwa wa matiti unaosababishwa na vimelea vilivyoingia kwenye ziwa kupitia sehemu ya chuchu iliyopata mchubuko wakati wa kuchonyesha. Hali hii huambatana na homa, uchovu pamoja na kuwa na kidonda kwenye ziwa. Pale unapoona dalili kama hizi muone daktari. Unaweza kuendelea kunyonyesha na huku ukitumia dawa za vijiua sumu (antibiotics). Kupunguza maumivu kwenye ziwa weka kitu chenye joto kwenye kidonda kwa takribani dakika 15 mpaka 20 mara nne kwa siku. Kamwe usitumie dawa pasipo ushauri wa daktari wakati ukiwa unanyonyesha.
Watoto waliozaliwa kabla ya umri. Mara nyingi watoto hawa huwa wana changamoto ya kunyonya wenyewe. Hivyo wakati mwingine inabidi mama amkamulie mwanae maziwa na kumnyonyesha kupitia kijiko na kikombe au kupitia mrija maalumu wa kulishia.
Msongo. Je ushawahi kujiuliza kwanini mama anayenyonyesha anapokuwa amekasirika hushindwa kutoa maziwa ya kutosha kunyonyesha? Hii ni kwa sababu msongo huwa unatokea katika ubongo wa kufikri ambao una mahusiano na sehemu inayoruhusu maziwa kutoka. Kuathirika huku kwa ubongo husababisha sehemu hii ya kuamrisha maziwa kutofanya kazi vizuri na matokeo yake ni kutotoka kwa maziwa.
Hii huathiriwa na ubongo wa utambuzi basi inaweza kuathiriwa na taarifa kupitia milango ya fahamu mingine kama kusikia, macho na n.k. Hii ndiyo sababu mama anayenyonyesha anapomkumbuka mwanae maziwa huanza kutoka. Hii ndiyo sababu ni muhimu kutulia na kukaa kwa utuvu kabla ya kunyonyesha kusaidia maziwa kutoka kwa urahisi na kwa uzuri. Matokeo yake ni mwanao kupata maziwa ya kutosha.
Dalili za hatari. Licha ya kuwa unyonyeshaji ni mchakato wa asili wa kumlisha mtoto zipo nyakati unyonyeshaji huleta madhara. Pale utakapoona dalili zifuatazo nenda hospitali au kwenye kituo cha afya:
Kama kuna majimaji yasiyo ya kawaida kutoka kwenye matiti yako ama matiti yako yana wekundu, yamevimba, magumu au yana kidonda au vidonda.
Kama mwanao haongezeki uzito au una wasiwasi hapati maziwa ya kutsha.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org