Matukio ya matumizi mabaya ya picha za watu mtandaoni yanaongezeka siku hata siku: Picha ya askari iliyochukuliwa katika mitandao ya kijamii ilitumika kumlaghai mwanamke mmoja huko Uingereza akatoa fedha zake nyingi na kuibiwa. Bloga mmoja alikuta picha ya familia yake inatumiwa kwenye tangazo la biashara Jamhuri ya Czech. Mama Mwingereza wa mtoto wa miaka minne alikuta picha ya mtoto wake iliyochukuliwa Facebook inatumika katika mtandao wa mapenzi nchini Brazil. ~ DailyMail
Mshawasha na wepesi wa kutaka 'kushea' picha za mtoto wako hasa kwa marafiki (na hata wasio marafiki) kwenye mitandao ya kijamii na blogu hauzuiliki kirahisi. Kwa bahati mbaya, athari za maamuzi hayo nazo haziepukiki. Kwamba picha zako mitandaoni zinaweza kuibiwa na kutumiwa na watu baki, lakini picha nyingi, hasa zile zilizochukuliwa na simu au vifaa vyenye teknolojia ya kuonyesha mahali ulipo (GPS), vinavyoonyesha mahala ambapo picha ilipigwa. Yaani, kama wewe hupiga picha ya mtoto akicheza nyumbani na kisha kuipakia mtandaoni, inawezekana kwa watu kujua eneo unapoishi.
Zifuatazo ni hatua sita ambazo kila mzazi anapaswa kuchukua ili kulinda watoto/mtoto wake na kwa kiasi kikubwa kupunguza uwezekano wa kuwa mwathirika wa matumizi ya mitandao - itasaidia ujue namna bora ya kupakia picha za mwanao mtandaoni.
Dhibiti matumizi ya faragha. Takribani mitandao yote ya kijamii huwapa watumiaji fursa ya kuamua linapokuja suala la nani anayeweza kuangalia picha zao na taarifa binafsi (mfano mwaka wa kuzaliwa, nk.). Facebook, kwa mfano inawapa watumiaji ruhusa kuamua iwapo wanataka "marafiki" tu kuona picha zao, au "marafiki wa marafiki," au "kila mtu."
Wajue ni nani marafiki zako. Kama una mamia ya marafiki kwenye mitandao ya kijamii, upo uwezekano kwamba huwajui wote vizuri. Pangilia muda upitie orodha ya marafiki zako kuhakikisha kama unawatilia walakini baadhi yao. Pengine ulikubali ombi la rafiki toka enzi za shule ya sekondari, lakini sasa unajua kwamba si mtu mwema. Unaweza kumuondoa katika orodha ya marafiki mtandaoni.
Zima teknolojia ya kuonyesha mahali ulipo (GPS) kabla ya kupiga picha kwa simu kama una mpango wa kuzipakia mtandaoni. Hata baadhi ya kamera za kisasa huwa na teknolojia hii, chunguza iwapo imezimwa kabla ya kupiga picha unazotarajia kuziweka mtandaoni. Ikiwezekana zima teknolojia hii hasa uwapo nyumbani kwani huwezi kujua ni wakati gani hasa utajikuta unapiga picha za 'tukio' linalokulazimu 'kushea' mtandaoni.
Chukua tahadhari ili kuepusha kutoa taarifa zako binafsi pasi kutarajia. Mfano picha uloipiga mbele ya nyumba yako inaweza kuonyesha makazi yako ni wapi, au T-sheti yenye nembo ya shule anakosoma mwanao inatoa taarifa za mtoto wako pasi wewe kupanga kufanya hivyo. Inashauriwa kuchukua tahadhari hizi iwapo malengo ya picha namna hii ni kutumika katika mitandao ya kijamii au blogu.
Picha za utupu ama mtoto akioga. Swali la kujiuliza ni iwapo mtoto wako akizikuta picha namna hii mika 10 au 20 baadaye zitamletea fedheha hasa ikifahamika kwamba zinaweza pia kuonwa na marafiki zake wa kiume/kike. Hii inakwambia kamwe usipakie picha za mwanao akiwa anajisaidia chooni, anaoga na akiwa mtupu bila nguo.
Simamia unachoamini kuwa sahihi. Iwapo ndugu au rafiki yako amepakia picha ya mtoto wako mtandaoni na wewe hujapenda kitendo hicho, muombe aiondoe. Hii ni kwa sababu huna hakika na umakini wao na hujui aina za marafiki alionao mtandaoni wanaoweza kuitumia picha ya mtoto wako kwa nia ovu. Hapa tunashauri pia iwapo unataka kuweka picha ya mtoto mtandaoni - omba ridhaaa kwanza.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
Comments