top of page
C-Sema Team

Afya na usalama wa mfanyakazi wa nyumbani ni jukumu lako mwajiri

Ongezeko la umasikini vijijini na ukosefu wa soko makini la mazao vimepelekea idadi kubwa ya watoto kuingia katika soko la ajira la kazi za nyumbani katika miji mbalimbali nchini. Wasichana na wavulana wenye umri mdogo wamejikuta wakiingia katika ajira hii kama njia mbadala ya kujipatia kipato katika harakati za kujikwamua kimaisha.


Afya na usalama wa mfanyakazi wa nyumbani

Kimsingi, wanajamii tutakubaliana kwamba katika kazi yoyote ile, iwe rasmi kama zile kazi za ofisini au isiyo rasmi kama usaidizi wa kazi za nyumbani, nk. - ulinzi wa afya na usalama wa mfanyakazi ni jambo muhimu sana katika mazingira yake ya kazi. Swali la kujiuliza ni kwamba je, waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani tunawajibika vipi katika kulinda afya na usalama watoto hawa wanatusaidia kazi?


Ukweli ni kwamba waajiri wengi 'baba au mama mwenye nyumba,' hudhani kuwa nyumba zao zina usalama, la hasha! Nyumba hizo hizo zinaweza kupelekea matatizo kadhaa ya kiafya na kiusalama kwa wasaidizi hawa wa kazi za nyumbani pindi wanapotekeleza majukumu yao.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa wafanyakazi wa nyumbani kwa kiwango cha juu wanafanya kazi katika mazingira yanayohatarisha afya pamoja na maisha yao kuliko wafanyakazi walio katika ajira rasmi. Hebu tujiulize je, huwa inakuaje kama ikitokea wakaugua? Au wakaumia? Na hivyo kushindwa kufanya kazi? Uzoefu unaonyesha kuwa, hali kama hii inapotokea waajiri walio wengi huchukua hatua za kutowalipa mishahara wasaidizi hawa au hata kuwafukuza kazi pasipo kujua kwamba awali ya yote, chanzo cha ugonjwa au kuumia kwao ni hiyo kazi yenyewe. Hapa ndipo ambapo wengi tunafanya makosa na kusahau kwamba jukumu la kulinda afya na usalama wao upo mikononi mwetu.


Katika maeneo mbalimbali tunapoishi, imekua ni jambo la kawaida kuona wafanyakazi wa nyumbani wakipewa jukumu la kuwahudumia wanafamilia wenye magonjwa mbalimbali, ikiwemo wenye magonjwa ya kuambukiza kama vile virusi vya ukimwi(VVU)/UKIMWI pamoja na kifua kikuu(TB). Cha ajabu ni kuwa wasaidizi hawa hawapewi elimu yoyote ya kujikinga na magonjwa haya na hivyo baada ya muda kujikuta na wao wakiugua. Wazazi tusichukulie kigezo cha kwamba wasaidizi hawa hawajui haki zao na hivyo mambo kama haya yanapotokea hawawezi kuhoji.Kitendo hiki ni tafsiri ya ukandamizaji na kuhatarisha maisha yao.

Siyo ajabu kuona baba au hata mwanae wa kiume wakijihusisha na mahusiano ya kimapenzi na binti mfanaya kazi wa nyumbani mwao wakati mmoja, ama kwa kujua na pasi kujua. Huu ni unyanyasaji wa kingono ambao unaonyesha ni jinsi gani wafanyakazi wa nyumbani hukosa amani na usalama wawapo katika kazi zao. Kutokana viitendo hivi, wengi wao hufikia hatua ya kutoroka na hivyo kuhatarisha maisha.

Ni nadra sana kuona wazazi wakiwapatia wafanya kazi wa nyumbani vifaa maalumu vya kujikinga kama vile glavu na vinyago (Masks) vya kuvaa usoni ili kijikinga pindi wanapofanya kazi zenye magusano baina ya sehemu za miili yao na mchanganyiko wa kemikali ambazo ni sumu. Je, kama jamii tunafurahi kuona wafanyakazi hawa wakiendelea kukumbana na adha za namna hii? Ni matumaini yetu kuwa jibu ni 'hapana' na hivyo ni jukumu letu kufanya juhudi za dhati katika kulinda afya na usalama wao pindi wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Jamani tutambue kuwa, kila mfanyakazi wa nyumbani anayo haki ya kufanya kazi katika mazingira salama na yasiyo hatarisha afya yake. Tubadilike!


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

2 views
bottom of page