top of page
C-Sema Team

Zijue kazi wanazofanyishwa watoto kinyonyaji

Sheria ya Mtoto inainisha juu ya haki ya mtoto kufanya kazi ili kumuandaa kujitegemea pindi awapo mtu mzima. Hivyo zipo taratibu na miongozo ya kufuatwa pale mtu yeyote anayehitaji kumwajiri mtoto sharti afuate. Makala haya yanalenga kuangazia taratibu hizi. Umri wa mtoto kuajiriwa. Mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka 14 ana haki ya kufanya kazi nyepesi na kupata malipo stahiki. Ieleweke kuwa, kazi nyepesi ni zile ambazo haziathiri afya ya mtoto, hazikwamishi maendeleo yake kielimu au makuzi yake.



Hii ni pamoja na kazi ambazo hazina madhara katika utendaji wa kazi za kimasomo zinazotolewa ili azifanye akiwa nyumbani, haki yake ya kucheza, au kazi ambazo haziathiri uhuru wake wa kushiriki katika mafunzo ya kijamii. Kwa hali hiyo, mtu haruhusiwi kumwajiri mtoto katika kazi yoyote ile ya kinyonyaji. Pia sheria inasisitiza kuwa, mtu haruhusiwi kumwajiri mtoto katika kazi yoyote ambayo ni hatari katika afya yake, elimu, akili, maumbile na hata katika maendeleo yake ya kiroho.


Kazi za kinyonyaji. Kazi itakuwa ya kinyonyaji kwa mtoto endapo kazi hiyo itakuwa inaathiri afya na makuzi ya mtoto, inazidi masaa sita kwa siku, hailingani au inazidi umri wake, inamlipa mtoto malipo kidogo na yasiyostahili au kazi hiyo inamhitaji mtoto kufanya kazi nyakati za usiku ambazo huanza muda wowote kati ya saa mbili za usiku hadi saa kumi na mbili za asubuhi.


Kazi hatarishi kwa mtoto. Hizi ni zile kazi zinazomfanya au kumlazimisha mtoto aingie baharini, zinazomfanya mtoto au kumlazimisha mtoto aingie mgodini au kwenye machimbo ya mawe, zinazomfanya au kumlazimisha mtoto kuponda mawe, zinazomwingiza au kumlazimisha aingie katika viwanda ambavyo madawa huzalishwa au kutumika, kazi za baa, hoteli, na mahali pengine popote pa starehe na mwisho ni kazi ambazo zinamweka mtoto katika mazingira ya jinsia ya mahusiano ya kingono au ukahaba bila kujali kama analipwa au halipwi.


Ulinzi wa mtoto kazini. Utakuwa ni wajibu wa kila mwajiri ambaye ameajiri mtoto, kuhakikisha kwamba kila mtoto aliyeajiriwa kihalali anapewa ulinzi dhidi ya mazingira yoyote ya unyanyasaji au vitendo vyovyote vinavyoweza kumwathiri kulingana na umri wake au uwezo wake wa kufanya kazi. Hii ni pamoja na kuhakikisha anamlinda na rushwa za ngono, n.k.


Kuhusu wasichana na wavulana wasaidizi wa kazi za nyumbani. Uzoefu tulionao unaonyesha kwamba familia nyngi zinazoishi mijini huhitaji wasaidizi wa kazi za ndani, wa kike (house girl) ama wa kiume (house boy/shamba boy). Wengi wa waajiri katika kundi hili pasipo kujua hujikuta wameajiri watoto wenye umri chini ya miaka 14. Hili ni kosa na katika sheria, haijalishi ulifahamu ya kuwa ni kosa au la.


Kundi la pili la waajiri hawa huwa makini kutaka kuajiri walau mwenye umri wa kuanzia miaka 14 na kuendelea. Hawa pia wanaweza kujikuta wanaingia katika kosa la unyonyaji na lile la kazi hatarishi. Unyonyaji huu unajikita katika masaa anayofanya kazi mtoto (hasa iwapo pana kazi anayotakiwa kuifanya kati ya saa mbili usiku na saa kumi na mbili asubuhi). Mifano ya kazi hatari ipo hapo juu. Kundi la tatu ni wale tunaompatia mtoto ajira bila ya kujua historia yake. Yaani amefikaje mjini, aliletwa na nani na je nyumbani kwao wajua aliko na anafanya nini huko? Hili ni kosa la usafirishwaji haramu wa watoto. Watoto wengi wakimaliza elimu ya msingi vijijini hurubuniwa na madalali kutafutiwa shule kujiendeleza au kazi mijini. Watoto hawa huishia majumbani mwetu pasi sisi kujua wamefikaje mijini.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org


2 views
bottom of page