Je, Tumefikiri kulea watoto wanaojali mazingira?
- C-Sema Team
- Jun 16
- 3 min read
Watoto wetu ni zawadi lakini pia ni wajibu mkubwa. Tunapowaangalia wakicheka, wakicheza na kuuliza maswali ya udadisi kuhusu dunia inayowazunguka, tunajiuliza Je, tunawalea kwa namna itakayowawezesha kuilinda dunia yao?

Kesho ya watoto wetu haitakuwa salama kama hawatajifunza kutunza mazingira kuanzia umri mdogo. Na kama wazazi, hatuhitaji kuwa wataalamu wa mazingira na hali ya hewa au wanaharakati wa mazingira ili kuanza kuwalea watoto wanaojali mazingira. Safari hii inaanzia pale pale nyumbani kwenye nyumba zetu, bustani zetu, sokoni, kwenye fukwe na hata njiani tunapowapeleka shuleni.
‘’Siku moja tulikwenda kufanya usafi mtaani. Tulijitwika mifuko ya plastiki na glovu, tukatembea na watoto huku tukikusanya taka. Waliniuliza, “Mama, kwa nini watu wanatupa chupa barabarani?” Huo ulikuwa mwanzo wa mazungumzo muhimu. Tuliwaeleza kuwa chupa za plastiki hujaza mifereji, huharibu mito, na huchangia vifo vya samaki. Watoto walielewa zaidi kwa sababu waliona kwa macho yao.’’ Mdau mmoja alitueleza.
Kwa hiyo, kama wazazi tunaotaka kufundisha watoto kuhusu mazingira tufanyaje?
Kwanza, tuwafundishe watoto kutotupa taka hovyo. Tunaweza kuweka vyombo vya kutupia taka (kama “dustbin”) nyumbani na kuwa na utaratibu wa pamoja wa kuzitupa sehemu sahihi. Tunapokuwa sokoni au kwenye matembezi, tuwatie moyo wachukue hata kipande cha karatasi kilichoanguka na kukitupa mahali stahiki. Tueleze kwa lugha rahisi kuwa kutunza mazingira ni namna ya kuonesha utaratibu mzuri na ustaarabu wa maisha kwa wengine.
Mdau mmoja alitueleza hivi: “Nilivyo kuwa mtoto, mama yangu alinifundisha kuweka ganda la pipi au karatasi kwenye begi langu hadi nitakapoona pipa la taka au kufika nyumbani. Mpaka leo, siwezi kamwe kutupa kitu barabarani. Imenibadilisha kabisa.”
Pia, tuwashirikishe kwenye shughuli za bustani. Hata tukiishi mjini, tunaweza kutumia chupa tupu au ndoo chakavu kupanda mboga ndogo kama mchicha au sukuma wiki. Tukiwapa jukumu la kumwagilia mimea kila siku, wanajifunza kwamba uhai unahitaji uangalizi wa mazingira. Na mmea unaponyauka kwa sababu walisahau kumwagilia au ikidhoofu na kudumaa kwa kuurundikia taka ngumu, wanajifunza moja kwa moja kutoka kwenye matokeo ya matendo yao kuwa kuyatunza mazingira ni kutunza na kujali maisha ya viumbe hai.
Tusisahau kuwa mazingira siyo ardhi pekee ni maji, ni hewa, ni nishati pia. Tuwe na mazungumzo mepesi kuhusu matumizi ya umeme na maji. Tunapozima taa au kufunga bomba la maji vizuri, tuwaambie kwa upendo: “Hii inasaidia dunia yetu kuwa salama” Watoto wanapenda kuelewa “kwa nini,” na tunapowaeleza sababu, wanakuwa washirika wa kweli.
Hadithi nazo ni njia bora na rahisi ya mtoto kuelewa. Tuwasimulie hadithi za mti ulioota nje ya shule ukawa kivuli kwa watoto, au samaki aliyepoteza uhai kwa sababu ya plastiki. Tushiriki nao zoezi la kupanda miti, kusafisha mtaa, au kuchora picha zinazoelimisha kuhusu mazingira. Kwa njia hii, wanaelewa si kwa nadharia tu, bali kwa hisia, uzoefu na vitendo.
Zaidi ya yote, tuwape nafasi ya kuongoza kwa njia zao. Wanaweza kubuni bango la mazingira kwa kalamu zao, kuanzisha kikundi shuleni cha kupanda miti, au hata kuandika shairi linalohimiza usafi. Tuwasikilize hata pale wanaposema kitu kinachoonekana kidogo kwa sababu ndani yake kuna mbegu ya mabadiliko makubwa.
Tukiwalea watoto wanaojali mazingira, tunawafundisha pia kuwa na huruma, kuwa na maono ya mbali, na kutenda kwa uadilifu. Ni kweli, dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira, lakini pia tuna nafasi kubwa ya kujenga kizazi kinachojali zaidi, kinachofikiri kwa upana, na kinachotenda kwa hekima.
Tuanze leo tukiwa na imani kwamba mabadiliko ya kweli yanaanzia nyumbani.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org