top of page
  • C-Sema Team

Zifahamu haki tano muhimu za mtoto wako


Sheria ya Mtoto inamtafsiri mtoto kama mtu mwenye umri chini ya miaka 18. Watoto ni sehemu muhimu ya jamii na ndiyo tegemeo la uendelevu wa taifa lolote, hivyo hawana budi kulelewa vizuri na kuendelezwa. Aidha, watoto wanayo mahitaji ya msingi ambayo kote Duniani yanatengeneza haki zao. Kimsingi haki za mtoto huwa ni wajibu wa mtu mzima kutimiza mahitaji ya mtoto ili awe mwenye afya, apate elimu na ashiriki katika ujenzi wa nchi yake sasa na hasa atakapokuwa mtu mzima.


Haki ya Kuishi. Hii inaanza pale mama anapopata ujauzito. Kukua vizuri kwa mimba kunategemea afya, lishe na mazingira anamoishi mama. Pia kuishi kwa mtoto baada ya kuzaliwa kunategemea upatikanaji wa mahitaji ya msingi, ambayo ni chakula cha kutosha na chenye ubora unaotakiwa, huduma bora za afya na ulinzi toka kwa wazazi, jamii na Serikali. Vifo vya watoto wadogo hutokana na ukosefu wa moja ya mahitaji tajwa hapo juu.


Haki ya Kuendelezwa. Kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania, maendeleo ya mtoto yanahusiana na mtoto kuwa na kiwango kinachokidhi makuzi kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii. Ili mtoto aweze kukua vizuri anahitaji kutunzwa, kuongozwa na kulelewa katika misingi mizuri. Mathalani, kuendelezwa kwa mtoto kimwili ni kukua kimaumbile na uzito kwa uwiano wa umri. Hali hii inategemea lishe na huduma bora za afya ikiwemo kupatiwa chanjo zote muhimu na upatikanaji wa viinilishe vyote muhimu. Maendeleo ya mtoto yanahitaji jitihada toka kwa mzazi, jamii na Serikali kwa pamoja.


Haki ya Kulindwa. Inahusu kuzuia vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto katika hatua za ukuaji wao, kabla na baada ya kuzaliwa. Mathalani, mtoto anahitaji ulinzi dhidi ya kazi nzito zisizowiana na umri wake, kudhulumiwa mali hasa kwa watoto yatima, kutupwa au kutelekezwa na wazazi, utoaji mimba wa makusudi, kuonewa nk. Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania pia inasisitiza juu ya ulinzi dhidi ya unyanyasaji wa mtoto ikiwemo kukeketwa, kulazimisha kuolewa/kuoa katika umri mdogo, ubakaji, nk.


Haki ya Kushiriki. Ushiriki wa mtoto unapatikana pale mtoto anapopewa nafasi kikamilifu katika kutoa mawazo, kushiriki katika maamuzi ya masuala yanayohusu maendeleo yake, nk. katika hatua mbalimbali za ukuaji wake. Kitaalamu hatua za ushiriki wa mtoto huanza rasmi kuanzia umri wa miaka mitatu hadi anapokuwa mtu mzima. Misingi ya ushiriki wa mtoto huzingatia umri na aina ya masuala anayopaswa kushirikishwa.


Haki ya Kutobaguliwa. Ubaguzi wa mtoto umegawanyika katika makundi mbalimbali, katika yote yapo makundi makuu mawili. Ubaguzi wa kijinsia ambao mtoto wa kike au wa kiume anaweza kubaguliwa na wazazi, walezi au jamii. Upo ubaguzi unaotokana na hali yake ya kimaisha kama vile utajiri au umasikini, ulemavu, ugonjwa, uyatima na jinsi anavyoonekana mbele za watu. Mfano wa kuumiza ni ubaguzi wa kimfumo ambapo hapa kwetu takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia moja tu ya watoto wenye ulemavu wanoandikishwa kujiunga na elimu ya msingi. Hii inaathiriwa na mtazamo wa kijamii dhidi ya watoto hawa kwani wazai huwafungia ndani kuficha aibu hivyo kuwanyima fursa ya kupata elimu.


Kwamba zile tunazodhani ni haki za watoto kumbe ni fursa za kulea kwetu wazazi. Uporomokaji wa maadili kote Duniani kumefanya mataifa kutiana vitanzi kuhakikisha watoto wanastawi kupitia mikataba na matamko mbalimbali ya Umoja wa Mataifa na kwingineko. Yaani hata pamoja na kuwepo haki hizi bado wapo baadhi ya wazazi wanaodhani ni uzungu kumpatia mtoto mahitaji yake ili akue vizuri.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

1 view

Recent Posts

See All
bottom of page