Kama wewe ni mzazi au mlezi wa mtoto wa miaka mitano, huenda tayari umeshaona kwamba wana shauku isiyoisha ya kudadisi na kujifunza na kugundua dunia na wana maswali mengi mno. Katika umri huu, watoto hupitia hatua kubwa za ukuaji za kimwili, hatua zenye harakati nyingi zinazotufurahisha na pengine kutukwaza sana wazazi.
Katika umri huu, watoto hukua kwa kasi na uwezo wao wa kutumia misuli ya miili yao kufanya vitu mbalimbali pia hukua. Kwa mujibu wa wataalamu wa Chama cha Madaktari wa Watoto Marekani (AAP), mabadiliko haya husababishwa na ukuaji wa sehemu ya ubongo iitwayo cerebellum, inayohusika na uratibu wa mwili.
Shughuli kama kuogelea, kupanda/kukwea vitu, na kukimbia kimbia huchochea ukuaji huu wa kifiziolojia na kuimarisha uwezo wa mwili. Madaktari wanapendekeza watoto wawe na shughuli tofauti zinazochangamsha mwili ili kuimarisha misuli yao na kukuza tabia za kiafya ambazo zitadumu kwa maisha yote.
Hata hivyo, ukuaji huu mara nyingi huambatana na hali ya kutotulia maana dakika moja mtoto amekaa chini na nyigine amepanda juu ya kochi au dirisha au amekimbilia chumbani nk. Dkt. Angela Duckworth, mwanasaikolojia maarufu wa watoto, anabainisha kuwa watoto wa miaka mitano wanakuwa hawatulii sehemu moja kwa sababu sehemu za ubongo zinazodhibiti utulivu hazijakua kikamilifu. Ubongo wao unawaelekeza watembe tembee, wakimbie, waruke n.k.
Tafiti nyingi zinaonyesha umuhimu wa watoto kuwa na shughuli tofauti za kifiziolojia katika ukuaji wao. Utafiti uliochapishwa katika jarida la Pediatrics unaonyesha kuwa shughuli hizo hupunguza msongo wa mawazo, huongeza umakini, na hata kuboresha uwezo wa kutatua matatizo kwa watoto. Chama cha Moyo cha Marekani kinapendekeza watoto washiriki angalau dakika 30 kwa siku katika shughuli za kuchangamsha mwili ikiwemo michezo.
Katika umri huu wa miaka mitano, watoto huanza kujenga mahusiano na wenzao, na wakati mwingine hupenda kukutana na watoto wenzao ili wacheze. Sasa pata picha una watoto sita nyumbani kwako wa umri huu na wote wanakimbia kimbia na kuparamia vitu na kuuliza maswali kwa wakati mmoja. Unaweza hisi kuchanganyikiwa na kukosa uvumilivu. Hivyo, kuepukana na hali hii na kuwawezesha watoto wetu kucheza vizuri na wenzao, wataalamu wa maendeleo ya watoto wanapendekeza mbinu zifuatazo:-
Tuchague Idadi ya watoto wanaokuja kucheza nyumbani. Watoto wawili wanapocheza pamoja wanapata nafasi nzuri ya kujifunza kushirikiana kuliko wakiwa katika kundi kubwa, ambapo kuna uwezekano wa wengine kujiona wamesahaulika.
Tuweke muda wa kawaida wa kucheza: Dakika 60 au 120 ni muda mzuri wa kucheza, Ikiwa mambo yanaenda vizuri, unaweza kuongeza muda kidogo, lakini ni bora kumaliza wakati watoto bado wanafurahia na hawajachoka sana.
Tutoe mwongozo wa sheria za nyumbani: Tuhakikishe kuwa, watoto wanaokuja kucheza wanaheshimu sheria za nyumba yetu. Tuwahimize watoto wetu kuwa mfano hai na mzuri kwa marafiki zao, kama sheria ni kwamba watoto hawapandi juu ya meza au hawakimbii ndani basi watoto wote wanapaswa kufuata sheria hiyo. Hii inasaidia kudumisha usalama, nidhamu na heshima kwa wote.
Kingine cha kufahamu ni kwamba watoto wa umri huu wana nguvu (energy) sana ndiyo maana wanaweza kuwa wamechoka ila bado wataendelea kucheza na wakati mwingine wao wenyewe hawatambui kwamba wamechoka, hii ni sifa moja maarufu kwa watoto wa umri huu. Kwa mujibu wa Dkt. Stephen Porges, mtaalamu wa neva, hali hii inahusiana na ukuaji wa ‘interoception’, uwezo wa kutambua hisia za ndani za mwili kama uchovu au njaa.
Ili kuwasaidia watoto katika hili, Tunapaswa kuwa na ratiba thabiti ya kupumzika na kulala, kuwapatia watoto shughuli ambazo zinachangamsha ubongo kama kusoma vitabu na kuchunguza mienendo ya watoto ili kutambua kama wmechoka na kuwahimiza wapumzike.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org (http://www.sematanzania.org/)