top of page

Je, malezi ya sasa yamekuwa magumu kuliko zamani?

  • C-Sema Team
  • Apr 30
  • 3 min read

Kila kizazi kina changamoto zake. Wazazi wa jana walikuwa na vikwazo vyao, nasi wa leo tunavyo vyetu. Lakini swali linabaki: Je, kuwa mzazi katika ulimwengu wa leo ni kazi ngumu zaidi kuliko ilivyokuwa zamani? Katika makala hii, tunachambua kwa undani hali ya malezi ya sasa, tukitazama mabadiliko ya kijamii, kiteknolojia, na kiuchumi yaliyoathiri namna tunavyowalea watoto wetu hasa katika muktadha wetu wa Kitanzania na Kiafrika kwa ujumla. Lakini zaidi ya yote, tunakumbushana kuwa hakuna mzazi mkamilifu bali wote tunajifunza kila uchao kutokana na uzoefu wa malezi ya kila siku.

Miaka ya nyuma, mtoto hakuwa wa mzazi mmoja tu alikuwa wa kijiji kizima. Majirani walikuwa ni sehemu ya familia. Bibi, babu, shangazi, mjomba, hata mama mwenye duka wa mtaa wa pili, wote walihusika katika kumkuza mtoto. Kulikuwepo na mfumo usio rasmi wa msaada; mzazi hakuhitaji kujua kila kitu kwa sababu jamii ilimsaidia kulea. “Mtoto ni wa jamii” Lakini je, jamii hiyo bado ipo kwa sura ile ile?


Leo, mazingira ya maisha yamebadilika sana. Wazazi wengi wanaishi mijini, mbali na familia zao za asili. Wengine wamehamia maeneo mapya kwa ajili ya kazi au masomo, na hawana ushirikiano na umoja  wa kijamii wa kuaminika. Majirani hawajuani. Na katika miji mikubwa, hata kuomba jirani akusaidie kumchunga mtoto kwa dakika kumi ni kazi.


Wakati huohuo, watoto wetu wamezaliwa katika dunia yenye taarifa nyingi kuliko uwezo wao wa kuzichakata. Wana simu mikononi, televisheni chumbani, na marafiki wa mtandaoni wanaowapa ushauri ambao mara nyingine hauendani kabisa na maadili ya familia. Ukweli ni kwamba, “Hatuwezi tena kuwalea watoto wetu kwa namna tulivyolelewa na wazazi wetu kwa maana wazazi wetu walitukuza kwa ajili ya dunia tofauti na ya sasa.”


Wengi wetu tulilelewa kwa adhabu kali, maneno makali, na hofu kama njia ya nidhamu. Lakini sasa tunajifunza kuwa malezi yenye kuzingatia utu, mazungumzo, na usikivu yanazaa matunda bora zaidi. Na hiyo si kazi ndogo ni kujifunza upya na kubadili njia tulizojifunzia wenyewe.


Mfano halisi: Baba mmoja mwenye mtoto wa miaka 14 aligundua kuwa kijana wake hana hamasa shuleni. Badala ya kumtishia au kumpiga, alianza kwa upole: “Umechoka au kuna kitu kinachokusumbua?” Katika mazungumzo haya, alijifunza kwa mara ya kwanza kuhusu afya ya akili ya kijana wake na mzizi wa tatizo lake. Ni ushuhuda wa wazi kwamba sauti ya mtoto haipaswi kukandamizwa bali kusikilizwa.


Changamoto zinazotukumba wazazi wa sasa ni pamoja na:

●       Kuelimisha watoto kuhusu usalama wa mtandaoni (hasa ukatili wa kingono mtandaoni na ushawishi wa watu wasiojulikana juu ya tabia kadha wa kadha hatarishi).

●       Kupata muda wa kuwa na watoto huku tukipambana na majukumu ya kazi na maisha.

●       Kujifunza teknolojia na ulimwengu wao wa kidijitali bila kuwahukumu au kuogopa mabadiliko yatokanayo na teknolojia.


Ingawa hatuna tena kijiji cha kihalisia, bado tuna nafasi ya kujenga kijiji kipya cha kusaidiana kinachoendana na muktadha wa mazingira yetu ya sasa. Hii inaweza kuwa: vikundi vya wazazi kwenye WhatsApp, jumuiya za wazazi shuleni, marafiki wanaoshirikiana na kusaidiana, au hata mahusiano ya karibu na majirani wa karibu.


Katika miji mikubwa, mahusiano haya hayaji kwa urahisi, lakini yanahitaji kujengwa kwa makusudi. Maana mzazi anayebeba kila kitu peke yake, huchoka haraka kimwili, kihisia, na kiakili na hali hii huathiri hata uhusiano wake na mtoto na huweka maisha ya mtoto hatarini. Inahitaji kijiji kumlea mtoto, lakini katika zama hizi inahitaji dhamira ya kweli kukijenga kijiji upya.


Hakuna kizazi kilicholea bila changamoto. Lakini tofauti ya sasa ni kwamba dunia inabadilika kwa kasi ya ajabu na imegeuka kuwa kijiji. Na mzazi asiye tayari kubadilika, hujikuta akipotea katika wimbi la mabadiliko hayo.


Ni muhimu tukumbuke kwamba si lazima tuwe wakamilifu, kukosea ni sehemu ya safari, upendo, uelewa, na usikivu na uvumilivu bado ni silaha kuu za mzazi. Kama kuna jambo moja tunaweza kurithi kutoka kwa vizazi vilivyopita, ni hili: Upendo wa kweli na nia njema ya mzazi vinaweza kubadili kabisa maisha ya mtoto bila kujali tamaduni na mazingira.


Na kwa kila hatua tunayochukua leo, tunatengeneza kesho yenye msingi bora zaidi kwa watoto wetu.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

 

 

bottom of page