top of page
  • C-Sema Team

Watoto wa Kitanzania wanatumia mitandao sawa na wenzao kutoka mataifa yaliyoendelea


Maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano hasa inteneti, simu na mitandao ya kijamii yamekuwa na athari chanya na hasi kwa watumiaji wakiwemo watoto. Tumezungumza na mtaalamu wa malezi Dr. Hezron Onditi wa Kitivo cha Elimu na Saikolojia, Chuo Kikuu cha Dar es salaam na makala haya yanatokana na mazungumzo hayo.


Anasema tafiti mbalimbali kutoka nchi zilizoendelea zinaonesha kuwa vijana na watoto ni watumiaji wakubwa wa simu na mitandao. Kwa ujumla watoto wa kizazi hiki wanatambuliwa kama wakazi wa ulimwengu wa ki-digitali na watu wazima ni walowezi wa ulimwengu wa kdigitali.


Matokeo ya utafiti wa karibuni uliohusisha jumla ya wanafunzi 780 wa sekondari (kidato cha I-IV) katika mkoa wa Mwanza na Dar es Salaam nchini Tanzania yamebaini yakuwa watoto wa Kitanzania wanatumia mitandao sawa na wenzao kutoka mataifa yaliyoendelea. Matokeo hayo ya utafiti yamebaini kuwa wanamiliki simu, wasikokuwa na simu wanamiliki laini ya simu, wasikua na wimu wala laini wanachangia simu au laini za wenzao. Watoto hawa wanatumia simu wakiwa majumbani, wengine hata wanaingia kwenye internet na kwenye mitandao ya kijamii mfano Facebook, Whasapp na Instagram.


Aidha, kati ya watoto wa kike wanaomiliki simu, nusu yao walisema yakuwa walezi / wazazi wao hawajui ya kuwa wanamiliki simu. Kwa uchache watoto wa kiume nao baadhi yao walisema wazazi / walezi wao hawana taarifa ya umiliki wao wa simu.

Watoto waliweza kutaja faida mbalimbali wanazozipata kwa kutumia simu, internet, na mitandao ya kijamii ikiwemo faida za kitaaluma, mawasiliano burudani (kusikiliza muziki, kucheza game), na kupata taarifa mbalimbali mubashara. Wengine walisema wanapata taarifa juu ya mada mbalimbali ambazo wanaona aibu kuuliza darasani mfano afya ya uzazi na mitindo ya kisasa. Mbali na faida, watoto waliweza kutaja changamoto na athari mbalimbali wanazo kumbana nazo kwenye mitandao na kwa kutumia simu.


Athari na changamoto kubwa iliyotajwa na watoto wengi ni unyayasaji / ukatili kwenye mitandao. Watoto walikiri kutukanwa, kudhihakiwa, kunyanyaswa, kudhalilishwa kwenye mitandao ya kijamii au kwa njia ya simu.


Udhalilishwaji hufanyika kwa njia ya jumbe fupi zenye maudhi, picha chafu zisizo na staha, video, kutumia taarifa binafsi, na kwa njia ya video fupi fupi. Miongoni mwa waliotajwa kushiriki vitendo hivi ni pamoja na watu wasiojulikana (online strangers), makundi rika, na wakati mwingine marafiki pale urafiki unapokoma.


Watoto hususani wa kike na wachache wa kiume walitaja kukumbana na ukatili na unyanyasaji wa kingono mitandaoni. Watoto walisema wanashawishiwa, kulaghaiwa au kurubuniwa kimapenzi na watu wazima na vijana wenzao wanaokutana nao kwenye mitandao. Kutokana na ufaragha mitandaoni na kuwa na idadi kubwa ya marafiki kwenye kurasa zao, baadhi ya watoto wamejikuta wakianzisha mahusiano na watu ambao hawajawahi kuonana nao uso kwa uso na hukutana nao bila ya walezi / wazazi kujua. Hii ni hatari sana kwa usalama wa watoto.


Changamoto nyingine iliyotajwa na watoto ni picha za ngono na usambazaji wa picha za utupu. Watoto walieleza kuwa kuna wenzao wanaopenda sana kuangalia picha za ngono na huwashawishi wenzao kuangalia picha hizo chafu. Hii ni hulka ya vijana ambao wako kwenye kipindii cha kubalehe ambao wengi wao hupenda kufanya kile kinachofanywa na kundi rika. Aidha, baadhi ya watoto walisema yakuwa wanaombwa kutoa picha zao za utupu na watu wasiowafahamau na marafiki zao wa kiume au wa kike na urafiki unapovunjika wengine hutumia picha za wenzao kuwanyanyasa.


Kutokana na faida za teknolojia ya habari na mawasiliano na sababu yakuwa kizazi hiki ni cha ulimwengu wa ki-digitali, kuna umuhimu wa kuwapa watoto wa rika zote elimu sahihi juu ya matumizi salama na bora ya simu na mitando ya kijamii. Kuna umuhimu wa kuwa na sera na sheria ya kumlinda mtoto wa Kitanzania kwenye mitandao.


Kutokana na sababu ya kuwa teknolojia ya habari na mawasiliano haina mipaka, jitiada za elimu na mikakati ya kitaifa zinatakiwa kwenda sambamba na mabadiliko katika sekta ya teknolojia.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

0 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page