top of page
  • C-Sema Team

Ujue waraka wa elimu kuhusu adhabu ya viboko shuleni Tanzania Bara

Kuvunjwa mikono, kuachwa na makovu mwilini pamoja na athari hasi za kiwango kikubwa zaidi kwa maana ya vifo ni matukio mbalimbali yaliyotendwa na yanayoendelea kutendwa dhidi ya wanafunzi mashuleni huku sababu kubwa ikihusisha adhabu ya viboko. Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa, utolewaji wa adhabu hizo haufuati taratibu, kanuni pamoja na miongozo husika iliyowekwa.



Tunapenda kuwakumbusha wazazi, wanafunzi, walimu, washika dau pamoja na wananchi wote kuwa mnamo mwaka 2002, Serikali ya JMT kupitia Wizara ya Elimu ilitoa Waraka wa Elimu (Na.24) Kuhusu Adhabu ya Viboko na kuweka utaratibu mahususi wa utolewaji wa adhabu ya viboko. Adhabu hiyo inaweza kutolewa endapo kutatokea utovu wa nidhamu uliokithiri ama kwa makosa ya jinai yaliyotendeka ndani ama nje ya shule yenye muelekeo wa kuishushia shule heshima. Waraka huu pia unaongeza kuwa adhabu ya viboko itakayotolewa sharti izingatie ukubwa wa kosa, umri, jinsi na afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja.


Nani mwenye mamlaka ya kumuadhibu mwanafunzi kwa viboko? Waraka wa Elimu (Na.24) Kuhusu Adhabu ya Viboko umeweka bayana kuwa ni Mwalimu Mkuu wa shule husika ama mwalimu mwingine atakayeteuliwa na mwalimu mkuu kwa maandishi, kila mara kosa linalostahili adhabu hii linapotendeka. Aidha, waraka huu unaonya kuwa mwanafunzi wa kike anapaswa kupewa adhabu ya viboko na mwalimu wa kike tu isipokuwa isipokuwa kama shule haina mwalimu wa kike.


Waraka umeweka wazi kuwa kila mara adhabu ya viboko inapotolewa sharti iorodheshwe katika kitabu kilichotengwa kwa kusudi hili, la kujaza taarifa zihusuzo adhabu husika, hii ikiwa ni pamoja na jina la mwanafunzi aliyepewa adhabu, kosa alilotenda, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu hiyo. Kwa kuwa waraka unamtambua Mwalimu Mkuu kama mtu mwenye mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko kwa mwanafunzi husika basi unamtaka pia atie saini yake katika kitabu hicho maalum kila adhabu ya viboko inapotolewa.


Waraka unasemaje pale mwanafunzi / mzazi anapokataa adhabu ya viboko? Waraka wa Elimu (Na.24) Kuhusu Adhabu ya Viboko unasema mwanafunzi anapokataa adhabu ya viboko sharti asimamishwe shule ili kupisha hatua zingine za kinidhamu juu ya kosa lake.


Mwisho kabisa waraka huu unawaonya waalimu kuwa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya yeyote ambaye atakiuka utaratibu ulioidhinisha na waraka huu. Kwamba kupitia Waraka wa Elimu (Na.24) Kuhusu Adhabu ya Viboko ni marufuku kwa mwalimu yeyote kuonekana na fimbo mkononi kwa lengo la kumuadhibu mwanafunzi.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org


Picha:- kwa hisani ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

7 views

Recent Posts

See All

Commentaires


bottom of page