top of page
  • C-Sema Team

Ubongo wa mtoto hutengamaa ndani ya siku 1000 za mwanzo

Hivi ni kina mama, kina baba na walezi wangapi wanafahamu namna siku 1,000 za mwanzo za utoto zilivyo muhimu kwa maisha ya mtoto na namna gani tunaweza kufikisha ujumbe wa umuhimu wa siku za mwanzo utotoni katika jamii zote nchini.


Wataalamu wanasema ubongo hukua kwa kasi kubwa katika siku 1,000 za mwanzo wa uhai wa binadamu. Hiki ni kipindi kinachoanzia kutungwa kwa mimba hadi umri wa miaka miwili. Kila mara mama au baba anapocheza na kucheka, kusoma kitabu au kushiriki mchezo na mwanawe, ujue kuna maelfu ya hisia chanya zinazojengeka kwenye ubongo wa mtoto huyo mchanga, zinazojenga uwezo wake wa kujifunza, utendaji, kuendana na mabadiliko na hata kukabiliana na changamoto.


Ripoti mpya ya ulimwengu iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) iitwayo Siku za Mwanzo za Maisha ya Kila Mtoto ni Muhimu (Early Moments Matter For Every Child).

Inasema kipindi cha tangu kutungwa mimba hadi kuanza shule ni muhimu. Ni fursa adimu katika kuandaa vema ubongo wa mtoto. Huu ndiyo wakati wa kuujenga ubongo wake. Ikiwa watoto watalelewa kwa namna inayojenga vema akili zao, wataweza kujifunza vema, hivyo wataweza kuchangia na kupata kipato bora zaidi. Hii itawasaidia wao, familia zao na uchumi wa Taifa kwa ujumla.


Watoto wanahitaji huduma bora za afya na lishe, kuchangamshwa, fursa za kujifunza utotoni na mazingira salama ili ubongo wao uweze kukua vema. Kwa bahati mbaya duniani kote, mamilioni ya watoto wanakosa fursa hii. Watoto milioni 155 wamedumaa, watoto milioni 230 wanaishi katika mazingira yaliyoathiriwa na machafuko na wanakabiliwa na msongo wa mawazo; wengine milioni 300 wanaishi katika maeneo yaliyoathirwa na uharibifu wa mazingira, haya mambo yote yanaathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto.


Tanzania pia ina maelfu ya watoto wanaokosa vichochezi hivyo vinavyolea ukuaji wa kiwango cha juu cha ubongo wao. Kwa mfano, lishe duni miongoni mwa watoto nchini imefanya asilimia 34 ya walio na chini ya miaka mitano kudumaa. Wataalamu wanasema kudumaa humkosesha mtoto fursa ya kukua akiwa na afya bora, kumkosesha uwezo wa kujifunza kikamilifu na hata kupunguza nafasi ya kupata ajira akifikia umri wa kuajiriwa.


Tunawezaje kubadili hali hii. Wafanyakazi wa afya na lishe waliopatiwa mafunzo stahiki, wanafanya kazi kubwa vijijini kwa kutoa mafunzo kwa wazazi juu ya malezi bora na namna ya kuelewa tabia za watoto wachanga. Vikundi vya kina mama wanapewa mafunzo ya namna ya kutengeneza vifaa vya kuchezea vya watoto vya gharama nafuu kutokana na malighafi zinazopatikana katika mazingira yao.


Mambo yote haya yanasaidia kuboresha malezi ya watoto. Hivyo basi, mara nyingine utakapopata fursa ya kumwangalia mtoto mchanga, tafadhali kumbuka kuwa ukuaji vema wa ubongo unahitaji lishe bora, huduma bora ya afya, mawasiliano chanya na mazingira salama. Inaweza kuonekana kuwa ni kitu kidogo, lakini maendeleo ya nchi yanategemea watu wenye uwezo kiakili. Inawezekana Tanzania kuwa na mamilioni ya watu wenye uwezo wa kiakili- wakiwamo wale watoto niliowaona mkoani Kigoma wiki iliyopita.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

4 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page